Salaam za rambirambi za Rais Kikwete kwa msiba wa Bi. Hawa Ngulume
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Familia ya aliyepata kuwa Mkuu
wa Wilaya ya Mbarali, Mama Hawa Ngulume kufuatia taarifa za kifo chake
kilichotokea katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, Jijini Dar es Salaam
alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa Saratani.
Mama Hawa Ngulume amefariki leo tarehe 30 Agosti, 2012.
Katika
Salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema Marehemu Hawa Ngulume, enzi za
uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia maamuzi yake katika
majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo
katika sehemu zote alizotumikia akiwa Mtumishi wa Umma, na baadaye
alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya alioutumikia katika Wilaya za
Singida Mjini katika Mkoa wa Singida, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na
mara ya mwisho katika Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.
“Nilimfahamu
Marehemu, enzi za uhai wake, kama Kiongozi Mwanamke shupavu
aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, na hivyo kuthibitisha ukweli
kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza”, amesema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo chake.
“Kutokana
na msiba huo mkubwa, natuma Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo
wangu kwa Familia ya Marehemu, Mama Hawa Ngulume kwa kuondokewa na
Mhimili muhimu na Kiongozi wa Familia. Natambua machungu mliyo nayo
hivi sasa kwa kumpoteza Mama wa Familia, lakini nawahakikishia kuwa niko
pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais
Kikwete amewataka wanafamilia ya Marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na
ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa wao kwani yote ni
Mapenzi yake Mola. Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema
aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Mama Hawa
Ngulume, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.
Dar es Salaam.
30 Agosti, 2012