KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi imeyaondoa majina ya wabunge wote waliokuwa wanawania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho waliokuwa wameunga mkono azimio la kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kama mawaziri wasingejiuzulu.

Chanzo cha habari kilichoomba kutoandikwa jina kilisema kazi kubwa ambayo imefanywa na Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama hicho iliungwa mkono na CC huku wajumbe wa vikao hivyo viwili wakimpongeza Rais Kikwete kwa kufanya uamuzi mgumu.

Inadaiwa Kamati ilikata majina yote ya wabunge waliowania nafasi hiyo, ambao walihusika katika utiaji saini “Azimio la kumn’goa Waziri Mkuu”, Mizengo Pinda lililoanzishwa katika kikao kilichopita cha Bunge na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto, endapo hakungefanyika marekebisho ya Baraza Mawaziri.

Wabunge hao walisaini fomu maalumu iliyolenga Pinda kuwaondoa mawaziri ambao wizara zao zilitajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati za Bunge ambapo ilikuwa ikihitajika sahihi za wabunge 70.

Wabunge hao ni Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini ambaye anawania nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa; Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye anagombea ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Ludewa.

Kwa mujibu wa wabunge hao, walikuwa wakishinikiza kuondolewa kwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Viwanda na biashara, Cyril Chami.

Habari hizo zilidai kuwa walioenguliwa na Kamati Kuu ambao pia Kamati ya Maadili ilipendekeza waenguliwe, yumo Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyekuwa akiwania uenyekiti wa Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja ambao wote walikuwa wakiwania uenyekiti wa mkoa wa Shinyanga.

Wengine walioenguliwa na CC ni Mbunge wa Nzega, Dkt. Khamis Kigwangallah na kada maarufu wa CCM, Hussein Bashe, ambao wote walikuwa wakiwania ujumbe wa NEC kupitia wilaya ya Nzega. Pia Mbunge wa Viti Maalum, Sara Msafiri ambaye alikuwa akiwania ujumbe wa NEC na Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe ambaye alikuwa akiwania uenyekiti wa Umoja wa Wanawake, mkoa wa Tabora.



Habari hizo zilisema sababu ya kuondolewa kwa wabunge Munde na Sara ni kutokana na kashfa ya rushwa kwa wabunge inayoendelea kuchunguzwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Vick Swai ambaye alikuwa akitetea nafasi yake. Katika Jumuiya ya Vijana (UVCCM), walioenguliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Anthony Mavunde, Mbunge wa Ilala Musa Azzan ‘Zungu’ aliyekuwa akiwania uenyekiti Wazazi.

“Wengi walioondolewa kwa kuwa wengi wao ni mizizi ya ufisadi, na kwa kuwa ukishaondoa mizizi unabaki mti lazima mti ukauke, tuliona hakuna haja ya kuleta kishindo kikubwa kwa kuondoa waliotajwa sana kwa ufisadi, ila matokeo mtayaona baadaye,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo via wavuti
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.