Na Mwandishi Wetu
Swissport Tanzania
Plc, ambayo ni kampuni inayoongoza kwa kutoa huduma bora za kupakia na kupakua
mizigo na kuhudumia abiria duniani, imeboresha huduma zake baada ya kujenga
bohari ya kwanza ya kisasa katika bara la Afrika iliyogharimu shilingi bilioni
26 za kitanzania.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania, Bw
Gaudence Temu jinsi sehemu ya kutolea mizigo ya ndani inavyofanya kazi kwa
ufanisi katika jengo hilo jipya la kisasa
|
“Matarajio ya ukuaji
wa huduma za usafirishaji kwa ndege yatakuwa ni ndoto kama hakuna huduma bora
za kupakia na kupakua mizigo nchini,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swissport
Bw Gaudence Temu wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembea ofisi za
Swissport zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es
Salaam.
Sekta ya usafiri wa
anga ni nyeti, ambayo uwepo na ukuaji wake unategemea huduma zinazoaminika—kama
vile pamoja na mambo mengine utunzaji na usimamizi wa mizigo, bohari, utunzaji
na usimamizi wa barua, utunzaji wa nyaraka zinazohusu mizigo iliyopakiwa au
kupakuliwa.
Bw Temu alisema
kwamba uzinduzi rasmi wa jengo hilo jipya la kuhudumia mizigo inayoingia na
kutoka nchini litazinduliwa rasmi mwezi ujao baada ya ujenzi wake wote
kukamilika rasmi.
Alisema kwamba
kampuni hiyo Swissport ni ya kimataifa ambayo inatoa huduma zake kwa takribani
nchini 58 duniani kwa kiwango cha ubora wa kimataifa ya kusafirisha, kuhifadhi
na kupokea mizigo ya aina zote na bidhaa mbalimbali.
Bw Temu aliongeza
kwamba kitengo cha bohari ya kupakia mizigo kimetengenezwa kwa teknolojia ya
juu kabisa katika kuhakikisha ufanisi na uharakishaji wa upakiaji mizigo ambapo
kinaweza kupakia tani 30 kwa siku.
Kwa kutambua umuhimu
wa huduma Kampuni ya Swissport inayotoa, Bw Temu alisema: “Tumeamua kuboresha
huduma zetu za kupakia na kupakua mizigo…kwa kweli, hizi ni nguzo muhimu kwa
ukuaji endelevu wa hii sekta nchini Tanzania.”
Akielezea uboreshaji
ambao umefanyika, Bw Temu alisema kwa sasa chumba maalum cha baridi cha
Swissport kimepanuliwa kwa kuongeza huduma mpya kama vile mfumo wa ukaguzi wa
mizigo ndani ya chumba chenye mitambo maalum. Alisema “chumba hiki maalum
kimegawanywa katika maeneo mawili: eneo moja lina ukubwa wa mita 200 za mraba
na lingine ni mita 100 za mraba.”
Akifafanua zaidi, ofisa mkuu huyo wa Swissport
alisema kampuni yao imefunga mizani ya futi 20 katika eneo lao kwa kutoa huduma
kulingana na mahitaji ya shirika la ndege husika.
Kwa upande wa
kuhifadhi mizigo, kampuni ya Swissport imejenga bohari ya kisasa na salama na
inayoweza kufiwa kwa urahisi. Imefungwa mitambo maalum ya CCTV na ya ukaguzi wa
magari. Pamoja na mambo mengine, bohari hii ina vifaa maalum kwa ajili ya
ukaguzi, uangalizi na utunzaji salama wa mizigo.
Uboreshaji uliofanywa
hivi karibuni umefanywa kwa lengo la kuisaidia serikali katika jitihada zake za
kuboresha huduma za usafiri wa ndege, ambao ni muhimu sana katika kukuza uchumi
wa nchi na kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi za ustawi wa mamilioni ya
Watanzania, kwa mujibu wa Meneja Mikataba na Masoko-Swissport, Bw James
Mhagama.
“Haiwezekani kwa
sekta ya usafiri wa anga ya nchi yoyote ile kukua kama hakuna uboreshaji wa
huduma zake,” alisema mtaalam wa vyombo vya anga Bw Andrew Msechu.
Shirika la Swissport
kwa hapa Tanzania linatoa huduma kwa mashirika ya ndege yafuatayo—Shirika la Ndege
Tanzania (Air Tanzania), Shirika la Ndege la Misri (Egypt Air), Emirates,
Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines), EWA Air, Fly Dubai, Shirika
la Ndege la Kenya (Kenya Airways), KLM Royal Dutch Airlines, LAM-Linhas Aereas
de Mocambique, Shirika la Ndege la Malawi (Malawian Airlines) na Shirika la
Ndege la Oman (Oman Air),
Mashirika mengine ni Shirika
la Ndege la Qatar (Qatar Airways), Shirika la Ndege la Rwanda (Rwandair
Express), Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA-South African Airways),
Shirika la Ndege la Kimataifa la Uswisi (Swiss International Air Lines) na
Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines).
Post a Comment