Mwandishi Wetu
Bandari ya Dar es Salaam imeandika
historia mpya kwa kupokea meli kubwa kuliko zote zilizowahi kutia nanga Bandarini
ikiwa na urefu wa mita 261.
Meli hiyo inayoitwa MV
Hammonia Grenada ambayo ina uwezo wa kubeba makasha 4,256 imetia nanga katika
bandari ya Dar es Salaam ambapo imeshusha makasha 483 na kupakia makasha 656
kabla ya kuelekea nchini Thailand.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA,
Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kwamba ujio wa meli hiyo ni ushahidi tosha
kwamba bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa za aina hiyo ambazo awali
zilikuwa zikiishia bandari ya Mombasa tu.
Kakoko amesema kwamba wapo
waliokuwa wakifikiri kwamba bandari yetu sasa haifanyi kazi lakini ukweli ni
kwamba bandari yetu ipo sawa na inaendelea kupokea meli kama kawaida.
Na kuwathibitishia hilo,
amesema kwamba hata Mhe. Rais John Pombe Magufuli wakati alipokuja kufanya
ziara katika bandari ya Dar es Salaam kulikuwa na meli nyingine saba zimetia
nanga.
“Napenda niwatoa hofu
wateja wetu kwamba bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa bila shida
yoyote na ujio wa meli hii umefungua milango ya meli nyingine kubwa kuja katika
bandari yetu,” alisema Kakoko.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mkuu, bandari ya Dar es Salaam ina gati zenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za
namna hiyo ambazo ni pamoja na gati namba 8,9 na 10.
Naye Rubani Mkuu wa Mamlaka,
Capt. Abdullah Mwingamno ambaye ndiye aliyeengiza meli hiyo amesema kwamba hii
ndio meli kubwa kuliko zote ambazo zimewahi kuingia katika bandari ya Dar es
Salaam.
Mwingamno amesema kwamba
hapo mwanzo mlango wa bandari yetu ulitengenezwa kuweza kuhudumia meli zenye
urefu wa mita 234 tu lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia na jinsi meli
zenyewe zinavyojengwa imeweza kuingiza hata meli za urefu mkubwa zaidi.
Pamoja na suala la
teknolojia, Capt Mwingamno amesema kwamba kwa sasa TPA ina wataalamu wa kutosha
ambao wamepata mafunzo sehemu mbalimbali Duniani ili kuweza kuingiza meli kubwa
za namna hiyo.
“Tumepeleka kundi la kwanza
la vijana wetu nchini Afrika Kusini kupata mafunzo ya jinsi ya kuingiza meli
kubwa katika bandari yenye lango kama la kwetu na kundi la pili la vijana hawa
tumelipeleka Copenhagen, Denmark,” amesema.
Amesema kwamba kundi la
tatu la vijana hao tulilipeleka Nantes nchini Ufaransa kupata mafunzo kama hayo,
kwahiyo napenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba tunao wataalamu wa kutosha
kuifanya kazi hii.
Hapo awali, TPA ilishawahi
kuingiza meli nyingine kubwa yenye urefu wa mita 250 na baadae ikaingiza meli
nyingine yeenye urefu wa mita 255.
Kwa mujibu wa Capt.
Mwingamno, meli zenye urefu wa mita 261 mara nyingi huishia Bandari ya Mombasa kutokana
na udogo wa lango letu lakini ujio wa meli hii umefungua rasmi milango ya
kibiashara.
“Ujio wa meli hii umefungua
rasmi njia kwa meli nyingine kubwa za aina hii ambazo zilidhani zisingiweza
kuingia katika bandari ya Dar es Saam na hivyo kufungua rasmi ushindani na bandari
nyingine,” amesema.
Mwisho.
IMETOLEWA NA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI
TANZANIA
S.L.P
9184
DAR
ES SALAAM
Barua Pepe: maoni@tanzaniaports.com
Simu za
Bure: 0800 110047 na 0800 110032
Post a Comment