Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Temeke wamehamasika na kuamua kuunda
vikundi vya usafi wa mazingira, ‘Usafi Clubs’, ikiwa ni moja ya matunda ya
mradi wa kuwawezesha wakazi wa mijini, ‘Urban Legal Empowerment’ unaolenga kusaidia jamii ya watanzania kupata haki zao za
kuishi katika mazingira salama na safi, haki
za kiuchumi na za kijamii.
Kupitia mradi huu, unaotekelezwa na shirika la LEAT kwa ufadhili
wa LSF, wakazi wa Temeke pamoja na kata zake, viongozi wa serikali za mitaa na jamii kwa
ujumla wamehamashishwa kutunza mazingira katika maeneo wanayoishi au kufanyia shughuli zao za kila siku.
“Kama sehemu ya utekelezaji
wa mradi huu, LEAT tumetoa elimu kwa wananchi, viongozi wa kata, madiwani, na wanafunzi, kuhusu sheria za
mazingira, kanuni, na namna gani elimu hii itakavyowezesha
wananchi kutunza na kuboresha mazingira yao,” amesema Bi. Glory Kilawe, Mratibu
wa mradi kutoka LEAT.
Baada ya kupata elimu, wakazi
wa Temeke wameunda vikundi vya mazingira, maarufu kama “Usafi Clubs”—ambavyo vinatumika kama vyombo vya
kuhamasisha usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali wilayani Temeke.
“Tunawashukuru LEAT kutupatia elimu hii
nzuri ya mazingira, kujua sheria na taratibu mbalimbali zinazohusu mazingira,”
anasema mmoja wa wakazi wa
Temeke, Hassan Juma, katika kikao maalum cha kutathmini utekelezaji wa mradi wa
LEAT wilayani humo.
Hemed Pazi, Mwenyekiti wa
Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria-Temeke (Temeke Paralegal Centre), anasema wamefanikiwa kuunda
vikundi (Usafi Clubs) vinne—viwili viko kata ya Mbagala and 2 kata ya
Mianzini–kama sehemu ya utekelezaji wa mradi huo.
“Kinachotufurahisha zaidi ni
kwamba hata viongozi wa serikali za mitaa ni sehemu ya vikundi ni wajumbe wa
Usafi Clubs. Hii inatia moyo, kwa sababu uwepo wa viongozi hawa unafanya vikundi hivi viaminike kwa jamii, na kuongeza
ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake,” kwa mujibu wa Pazi.
Diwani wa Kata ya Mianzini,
Abdallah Kipende amesema elimu inayotolewa na Usafi Clubs mitaani imebadilisha
tabia na mitazamo ya wakazi wengi kuhusu maswala ya mazingira, hata kuwawezesha
kununua vyombo na mapipa ya taka kwa ajili ya majumbani na mitaani,
kuacha kabisa tabia ya kutupa taka ovyo, kama walivyozoea siku za nyuma.
“Sasa hivi, jamii ya
Temeke iko makini sana katika maswala ya mazingira; kila mtu sasa anajua usafi
wa mazingira maana yake nini. Kama kuna mtu (leo hii) anataka kujenga kiwanda
au kuleta uwekezaji wowote Temeke,
lazima ajiandae kujibu maswali magumu ya wananchi kama vile ‘mbinu gani atakazotumia
kutunza na kulinda mazingira’,”
alisema Kipende.
Mbali na kuwezesha uundaji wa
vikundi vya mazingira, LEAT imesaidia kutatua migororo ya mazingira 19,
kuelimisha wanafunzi zaidi ya 600, kusambaza machapisho mbalimbali yanayohusu
mazingira kwa jamii, kuandaa midahalo na vipindi maalum vya television na radio
–kujadili maswala ya mazingira—kama sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Urban
Legal Empowerment katika
wilaya
ya Temeke.
Mradi huu umebuniwa na
kufadhiliwa na shirika la Legal Services Facility (LSF) na lengo kuu la mradi huu ni kuwezesha watanzania waishio mijini, hasa wasiojiweza kifedha, katika maswala mbalimbali ya kisheria,
kijamii na kiuchumi.
Legal Services
Facility (LSF) imeyawezesha mashirika sita yasiyokuwa ya kiserikali kwa ajili
ya utekelezaji wa mradi wa ‘Urban Legal Empowerment’ katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam
Post a Comment