Na Mwandishi Wetu
Ikiwa imebaki miezi michache tu
kufanya uchaguzi mkuu, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi ya maendeleo katika sekta
mbalimbali za uchumi na kuboresha huduma za kijamii nchini. Katika yote haya,
imekuwa nyota inayong’aa si tu kwa Afrika Mashariki, bali pia kwa Bara la
Afrika kwa jumla.
Utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii umefanyika kwa kuongozwa na sera, sheria, kanuni, taratibu na utekelezaji wa mikakati mbalimbali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo endelevu.
Ukuaji
wa Uchumi:
Serikali yoyote duniani katika
ukusaji wa mapato ili kuimarisha uchumi wa ndani inategemea usimamiaji
madhubuti wa sera, programu na mikakati mbalimbali kwa kuhakikisha mapato
yanazidi kukua siku hadi siku. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21,
serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi trilioni 20.59 na katika mwaka wa fedha
2023/24, ilikusanya kiasi cha Shilingi trillioni 28.83, ambazo ni mapato ya
ndani. Pamoja na mambo mengine, katika ukusanyaji wa mapato, Shilingi trilioni
120.16 zilikusanywa kutoka vyanzo vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wizara,
wakala wa serikali na serikali za mitaa.
Katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu, serikali ya awamu ya sita iliamua kuondoa ada, na ilianza kusambaza vitabu, na kujenga madarasa, na pamoja na mambo mengine kufanya mapitio ya Sera ya Elimu, mafunzo ya ufundi na mitaala ili kuhakikisha wahitimu wanapata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Katika sekta ya elimu, ambapo mapitio
ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) yanalenga kuhakikisha wahitimu
wanakuwa na maarifa, ujuzi, na maadili ili waweze kupenya katika soko la ajira.
Serikali iliamua kujenga shule 26 za
wasichana za masomo ya sayansi kila mkoa, na shule 7 za wavulana kila kata nchi
nzima, shule za msingi na sekondari 191,708 zilijengwa hadi mwaka 2020, na
shule 254, 393 zimejengwa nchi nzima hadi mwaka 2025.
Pamoja na mambo mengine, shule za msingi mpya zilizojengwa mwaka 2025 ni 17, 986 na hadi mwaka 2020 zilizokuwepo shule 16,406. Idadi ya shule zote hizi ni matokeo chanya ya Ilani ya CCM.Vile vile serikali iliongeza vyuo vya ufundi stadi kutoka vyuo 662 mwaka 2020 hadi vyuo 860 mwaka 2024 kuendeleza ujuzi wa Watanzania katika sekta ya ufundi.
Msingi wa maendeleo ni pamoja na
kuboresha afya ya umma. Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan iliwekeza
katika sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya afya kutoka 8,783 mwaka 2020 hadi
vituo vya afya 12, 846, na kuboresha miundombinu ya majengo, kununua vifaa
tiba, kuboresha huduma za kibingwa na kusomesha madaktari na wahudumu wengine
katika sekta ya afya.
“Miaka minne iliyopita idadi ya vifo
vya akina mama wanaojifungua ilikuwa 556 kati ya 100,000, lakini kutokana na
uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, idadi ya vifo ilipungua hadi kufikia
104. Lengo la dunia ni vifo 70. Nina hakika tutafika huko na kuondoa kabisa
vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” alisema Dkt Samia Suluhu Hassan
wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya mojawapo nchini.

Miaka michache iliyopita akina mama
walikuwa wakiamka alfajiri na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo pia
walikuwa hawana uhakika kama wangeweza kuyapata. Hadi kufikia mwaka huu,
serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi ya usambazaji wa maji 2,331 katika
miji na vijiji. Miongoni mwa miradi hiyo, ni ile ya Same, Mwanga na Korogwe
ambapo wananchi wapatao 456,930 wamenufaika na miradi ya maji safi na salama.
Kilimo
Kwa miaka mingi kumekuwa na kauli
mbiu mbalimbali za uhamasishaji wa kilimo tangu serikali ya awamu ya kwanza
kama vile siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, na kilimo kwanza (ambayo
ilikuwa kauli mbiu ya serikali ya awamu ya nne). Kilimo ni uti wa mgongo, na
kauli mbiu hii inathibitisha utekelezaji wa sera ya kilimo kwa serikali ya
awamu ya sita kwa kuongeza bajeti yake kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka
2021/22 hadi Shilingi trilioni 1.24 mwaka 2024/25, na kuifanya sekta ya kilimo
kuchangia asilimia 26.2 kwa pato la taifa
Miaka ya nyuma Tanzania ilitofautisha
mazao ya chakula, na ya biashara, lakini kwa sasa mazao karibu yote ni ya
biashara, na mahitaji ni makubwa kwenye soko la nje, hata nyama kutoka Tanzania
ambayo ni fursa muhimu kwa wakulima na wafugaji, lakini pamoja na mambo
mengine, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17.1
mwaka 2021 hadi tani million 22.8 mwaka 2024, huku serikali ikitoa ruzuku ya
Shilingi billioni 300 katika kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo huajiri
takribani asilimia 65 ya nguvu kazi.
Serikali ya awamu ya sita imbadilisha
mfumo wa kizamani na kuweka mfumo wa kisasa kuhakikisha ajira za Watanzania
zinaendelea kuongezeka na usalama wa chakula una kuwa wa uhakika kwa kuongeza
uzalishaji wa chakula cha mifugo kutoka tani millioni 1.38 mwaka 2020 hadi tani
millioni 2.6 mwaka 2025, na kuongeza maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta
millioni 2.78 hadi hekta millioni 3.48. Ongezeko hili limepunguza migogoro ya
wakulima na wafugaji, huku mauzo ya nyama nje ya nchi yakiongezeka pia kutoka
tani 1,774 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 4.2 mwaka 2020
hadi tani 9,863.41 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 44 mwaka
2025.
Madini:
Sekta ya madini kwa muda mrefu
ilionekana kama urithi wenye laana, lakini kwa sasa sekta hii muhimu kwa
maendeleo ya taifa imeboreshwa kupitia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka
2019, na mwaka 2022 mchango wake katika pato la taifa umeongezeka kutoka
asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10.1 mwaka 2025. Masoko ya madini
yameongezeka kutoka 41 mwaka 2021 hadi kufikia 43 mwaka 2025 na vituo vya madini
vimeongezeka kutoka 61 hadi kufikia vituo 109. Uboreshaji katika sekta ya
madini umesogeza huduma kwa wananchi, na kuongeza uwazi katika sekta hii muhimu
kwa maendeleo ya taifa.
Katika kuhakikisha mchango wa sekta
hii unaendelea kukua kwa kasi, serikali ya awamu ya sita iliamua kununua
mitambo 15 ya uchongoraji kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisambaza sehemu
mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na kupanua uwazi
wa sekta ya madini.

Pamoja na mambo mengine, baada ya
kilio hicho cha muda mrefu na baadaye kwa kuwa na Sera ya Madini ya mwaka 2009
ya kuwawezesha Watanzania wazawa kushiriki katika sekta ya uchimbaji wa madini,
kupata kazi za ukandarasi, zabuni na kutoa huduma mbalimbali kupitia Kanuni ya
Maudhui ya Ndani (Local Content) Watanzania wamekuwa wakipata ajira ndani ya
migodi na nafasi za menejimenti kushikwa na wazawa.
Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa
na uchumi wa kijani kupitia viwanda, na kupunguza tatizo la ajira nchini
kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya viwanda 47,063 vilianzishwa. Kati ya
hivyo, viwanda vikubwa ni 428, vya kati ni 1,393, vidogo ni 11,847 na vidogo
sana ni 33,395, na pamoja na mambo mengine, kuendeleza kiwanda cha ngozi
(Kilimanjaro Leather International Company Limited) kinachomilikiwa na Mfuko wa
Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa asilimia 86, na Jeshi la Magereza kwa
asilimia 14 kwa uwekezaji wa Shilingi billioni 152.96. Kwa hakika sekta ya
viwanda ni injini kwa maendeleo ya taifa.

Makala haya hayawezi kutosha kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameisimamia kikamilifu ili kulinda na kuendeleza maliasili na utalii, uchukuzi, miundombinu, ardhi, nishati, mawasiliano na sekta zingine mtambuka kwa masilahi mapana ya nchini yetu.
Mwisho….
Post a Comment