Pichani Juu na Chini ni Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi zilizopo wilayani Tarime mkoa wa Mara wakifurahia msaada wa madawati zaidi ya 1,000 kutoka mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG).
Wanafunzi wa shule za msingi za serikali za wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara, wakikaa sakafuni kabla ya kupata msaada wa madawati zaidi ya elfu moja kutoka mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG).
Msaada wa pikipiki tatu maarufu kama Bajaj ambazo mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) ulitoa kwa baadhi ya wananchi wa jamii zinazoishi karibu na mgodi huo uliopo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.
 
TARIME
Mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) umetoa msaada wa madawati zaidi ya 1,000 kwa shule za msingi zilizopo wilayani Tarime, mkoa wa Mara.Msaada huo utakaoenda kwa shule 10 za msingi, utawanufaisha karibu wanafunzi 6,000 ambao kwa sasa wanalazimika kusoma wakiwa wameketi chini kwenye sakafu ya udongo.
Madawati hayo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 76.5 yametolewa na kampuni ya ABG kupitia mfuko wake wa maendeleo.
 
Shule zitakazofaidika na msaada wa madawati hayo ni Nyangoto, Marare, Nyamongo,Nyabhigena, Kerende, Genkuru, Bung’eng’e, Nyaisangero, Nyamwaga, Nyakunguru A na Nyakunguru B.
 
Shule hizo zina jumla ya wanafunzi wanaozidi 5,800, huku wanafunzi wengi wakiwa wanakaa sakafuni kutokana na kukumbwa na upungufu mkubwa wa madawati.
Akipokea msaada huo juzi, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, aliishukuru kampuni ya ABG na mgodi wake wa North Mara kwa madawati hayo.
 
Henjewele alisema kuwa madawati hayo yatasaidia kuondoa kero ya muda mrefu ya shule hizo ya wanafunzi kukaa sakafuni na hivyo kusoma katika mazingira magumu.
“Hili ni tukio la kihistoria ambalo linaonesha jinsi mgodi na watu wanaoishi eneo hili walivyokuwa na mahusiano mazuri,” alisema.
 
Walimu pamoja na wanafunzi wa shule za Tarime walifurahia msaada huo na kusema kuwa utasaidia kuboresha mazingira ya elimu.“Tunafuraha kubwa kukabidhi zaidi ya madawati 1,050 kwa shule zinazozunguka mgodi wa North Mara na hii inadhihirisha jinsi ambavyo jamii zinavyopata manufaa kutoka kwenye mgodi wetu,” alisema Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Gary Chapman.
 
Msaada huo wa madawati ulienda sambamba na kuzinduliwa kwa program ya Can Educate ambayo inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye uwezo ambao wanatoka kwenye jamii maskini.Mgodi huo pia ulitoa msaada wa pikipiki za Bajaj kwa wanakijiji watatu wenye ulemavu wa viungo.Mgodi wa North Mara umekuwa ukitoa misaada mingi ya jamii zinazozunguka mgodi huo kwenye sekta ya elimu, afya, maji, miundombinu na uwezeshaji wa kiuchumi.
 
Uongozi wa kampuni ya ABG pamoja na mgodi wa North Mara umekuwa ukifanya jitihafa kubwa kuboresha mahusiano na jamii zinazozunguka mgodi huo.