Na Damas Makangale, Bulyanhulu, Kahama
Baadhi ya mameneja na wafanyakazi wa
kampuni ya migodi Bulyanhulu na North Mara wakifuatilia mada kwenye warsha ya
mafunzo kuhusu maudhui ya ndani (Local content ) na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR)
iliyofanyika mwishoni mwa wiki Bulyanhulu katika kitongoji cha Kakola, Wilaya
ya Msalala
Tume ya Madini nchini imeiopongeza kampuni ya AKO kuwa moja ya makampuni ya wazawa inayofanya vizuri kwenye utaoji wa huduma kwenye migodi hapa nchini.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Tume
ya Madini, Bi Janet Lekashigo alipokuwa akijibu maswali kwenye semina ya
mafunzo ya siku moja kuhusu utekelezaji wa maudhui ya ndani (Local content) na
uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kuhusu ushiriki wa wakandarasi na wasambazaji wa
huduma na bidhaa wa ndani kwenye sekta ya madini hapa nchini.
Bi Legashigo alisema kwamba kwenye
utekelezaji wa maudhui ya ndani (Local content) kampuni ya AKO imekuwa ikifanya
vizuri na nia ya serikali kuona na kuwawezesha watanzania kushiriki katika kufanya
biashara na makampuni ya uchimbaji madini, uwekezaji kwenye sekta husika na
kuboresha ustawi wa jamii na uchumi kwenye maeneo yanayozunguka migodi hapa
nchini.
Bi Janet Lekashingo alisema kuwa
lengo la serikali kuanzisha kanuni za muadhui ya ndani (Local Content) na
Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ni jitihada za kuhimiza uendelevu, ushirikishwaji
na kutoa sehemu ya faida kwa jamii inayozunguka migodi husika.
“Hii sio tu kutimiza majukumu, bali ni kuunda
mustakabali ambapo uchimbaji madini utakuwa na matokeo chanya na endelevu.
Tangu kuanzishwa kwake, Tume ya Madini imekuwa mstari wa mbele na imara katika
kuhakikisha kwamba bidhaa na huduma za watanzania zinapewa kipaumbele katika
sekta hii,” alisema.
Alisema kwamba kwa kuweka kipaumbele
kwenye maudhui ya ndani (Local Content) Tume hiyo imeona ongezeko kubwa la watanzania
wanaonufaika moja kwa moja kutoka kwenye sekta ya madini ni ishara wazi ya maendeleo ukilinganisha na
miaka iliyopita.
Alisema utekelezaji wa maudhui ya
ndani ni kuhusu kuiwezesha jamii – kutengeneza ajira, kukuza biashara za ndani
na kuboresha maisha ya watu wanaozunguka maeneo ya uchimbaji madini kwa
kuwashirikisha moja kwa moja na njia isiyo ya moja kwa moja katika shughuli za
biashara na uchimbaji madini.
“Tunapoanza semina hii, tukumbuke
umuhimu wa maudhui ya ndani (Local Content) katika kufungua uwezo wa Tanzania. Hizi kanuni ni daraja linalowaunganisha watanzania
kupata ujuzi wa kimataifa na za ndani, kuhakikisha kwamba sekta ya madini
inakuwa nguzo ya maendeleo endelevu ya kitaifa,” alieleza.
“Ni muhimu kwa kampuni kuwawezesha
wasambazaji wa ndani kama sehemu ya jitihada za serikali na makampuni ya madini
kujenga uwezo, kuunda na kukuza uelewa wa pamoja na ushirikiano.”
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi
wa Barrick Bulyanhulu, Bw Victor Lule alisema kwamba moja ya changamoto kwa
wasambazaji wa ndani, wazawa ni kushidwa kufikia malengo ya makubaliano katika
kazi tunazofunga mkataba na hiyo ni changamoto kubwa sana kwao.
Meneja Mkuu wa Bulyanhulu, Bw Victor Lule akieleza jambo wakati wa semina ya mafunzo ya siku moja kuhusu utekelezaji wa maudhui ya ndani na uwajibikaji kwa jamii kwa maafisa wa Tume ya Madini. Semina hiyo ilifanyika kwenye mgodi hivi karibuni kushoto kwake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Bi Janet Lekashingo.
“Shida ni kwamba wasambazaji wa ndani
ambao ni watanzania wenzetu ni uaminifu na kushidwa kumaliza kazi kwa muda na
kuleta bidhaa au huduma chini ya viwango hii ni changamoto ambayo tunakutana
nayo sana,”
“Ni kampuni ya AKO group ndio
wanafanya vizuri kwenye eneo la huduma na tunataka watanzania wengine wafike
viwango hivyo,” alisema Bw Lule
“Kwa sasa, tuko kwenye njia sahihi
kwani takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 82 ya manunuzi yetu ilifanywa na
wasambazaji wa ndani, wakati asilimia 12 iliyobaki ilifanywa na wasambazaji wa
kigeni. Tunaendelea kutekeleza kile tunachosema kuhusu utekelezaji wa maudhui
ya ndani.”
Alisisitiza kuwa kampuni ya uchimbaji
madini itaendelea kuwaelimisha wafanyabiashara na wasambazaji wa ndani jinsi ya
kufanya biashara na makampuni ya madini jinsi ya kusajili kampuni zao na
kushiriki katika semina, warsha na mikutano ili kujenga uelewa na uhusiano wa
pamoja na endelevu.
Bwana Lule alieleza kuwa kampuni hiyo
Barrick Twiga asilimia 96 ya wafanyakazi wake ni watanzania, baadhi yao wakiwa katika ngazi ya
uongozi, jambo ambalo ni Ushahidi tosha kwamba mgodi huo inakuza falsafa ya maudhui ya
ndani. (local Content)
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wasambazaji
wa ndani kuwa waaminifu, wachapakazi na kutekeleza kazi na kukabidhi ndani ya
muda wa makubaliano . aliongeza baadhi ya wasambazaji wa ndani walishindwa
kutimiza majukumu yao na wakati mwingine walileta bidhaa chini ya viwango.
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Madini na
Biashara kutokaTume ya Madini, Bw Venance
Kasiki, alisema kuwa Tume ya Madini imekuwa na mikutano kadhaa na taasisi za
kifedha nchini benki za ndani kuanza kuwawezesha wasambazaji wa ndani katika
sekta ya madini kama vile kutoa mikopo
kama hatua za awali za kurahisisha utekelezaji wa maudhui ya ndani.
“Tuna mikutano kadhaa na majadiliano
na benki mbalimbali nchini kama vile CRDB, NMB na nyingine ili kuanza kuangalia
sekta ya madini kama sekta inayokua kwa kasi na yenye matokeo Chanya na si
hatari tena,” alisema.
MWISHO.
Post a Comment