Dar es Salaam.
Mkutano Mkuu wa Chadema, kwa kauli moja, umempitisha waziri mkuu wa
zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 25, papo hapo mwanasiasa huyo akasema Chadema itachukua nchi
asubuhi.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa (katikati) akiwa ameshikana mikono na mgombea mwenza, Juma Duni Haji (kushoto) baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kuwapitisha kugombea nafasi hizo, Dar es Salaam jana. Kulia ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Picha na Emmanuel Herman |
Lowassa alipitishwa kuwania urais kwa mwavuli wa Ukawa kwa kuungwa mkono na vyama vyote katika “safari ya uhakika”.
Mbunge
huyo wa zamani wa Monduli, aliyejiunga na Chadema Julai 28 akitokea
CCM, akiwa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji aliyejiunga pia na Chadema
akitokea CUF, walipitishwa kwa kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ na wajumbe wote
wa mkutano mkuu huo uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es
Salaam.
Kabla ya kujiunga na Chadema, Duni alikuwa
Makamu Mwenyekiti wa CUF – Zanzibar na Waziri wa Miundombinu na
Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kiongozi
huyo amelazimika kujiuzulu nyadhifa zote ili kuwa mgombea mwenza wa
Lowassa kutokana na sheria za vyama vya siasa na uchaguzi nchini kutaka
mgombea urais na mgombea mwenza watoke chama kimoja cha siasa.
Lowassa
aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi alifika ukumbini hapo
saa 5.25 asubuhi akiwa katika msafara wa magari manane na kupokewa na
mamia ya wajumbe wa mkutano huo huku wakiimba, ‘rais. rais, rais, rais”.
Katika
msafara huo, Lowassa akiwa na familia yake, aliambatana na waliokuwa
makada wa CCM ambao pia walijiunga na Chadema akiwamo aliyekuwa
mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai.
Wengine
ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga,
aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, huku Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu akisema kuwa viongozi
hao wamepewa kadi za chama hicho kwa niaba ya wenzao watakaojiunga na
Chadema siku chache zijazo.
Mkutano huo uliokuwa na
shamrashamra za kila aina, ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama
vinavyounda Ukawa; NCCR–Mageuzi, NLD na CUF isipokuwa Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa bado amewekwa kando wakati mchakato huo wa kwenda Ikulu ukiendelea.
Wengine
waliohudhuria ni mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali, viongozi
wa vyama vya siasa vya nchi jirani, wabunge na viongozi wa dini, akiwamo
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia
Kakobe na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima
pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambaye pia ni
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Gratian Mukoba.
Lowassa: Tutachukua nchi asubuhi
Akihutubia
mkutano huo mkuu wa Chadema kwa mara ya kwanza, Lowassa alisema chama
hicho kupitia Ukawa kitachukua nchi mapema asubuhi Oktoba 25.
Alisema Watanzania wanajua kuwa Chadema wamepania, wamejipanga na wana uhakika wa kukamata dola mwaka huu.
“Nilianza
na safari ya matumaini, lakini sasa nasema hii ni Safari ya Mabadiliko
nje ya CCM, tutakamata nchi mapema kabisa asubuhi,” alisema Lowassa.
Hata
hivyo, Lowassa alitahadharisha kuwa kuing’oa CCM ni kazi kubwa kama
hakutakuwa na mipango na malengo huku akisema hakujiunga na chama hicho
akiwaza kushindwa na kwamba hana msamiati wa kushindwa na wala hakwenda
kwa bahati mbaya, bali alijiridhisha na kukubaliana na familia yake hadi
kufikia uamuzi huo.
“Nimekuja Chadema nikijua kuwa
kazi ya chama ni kushika dola na kama si hivyo, hakuna sababu ya kuwa
chama, nimejiandaa vizuri kushika dola… watu wanasema Chadema haiwezi,
Tanu ilipewa nchi ikiwa na miaka saba, sasa ninyi mna miaka 23,” alisema
na kushangiliwa.
Aliongeza,“Najua kazi ni kubwa na
mnajitolea, ndiyo maana chama kina nguvu na moyo kama CCM ya zamani si
ya sasa, ndiyo maana tumeikimbia,” alisema Lowassa.
Alisema
atapita kila jimbo kutengeneza mipango ya ushindi kwa kufanya kampeni
za kistaarabu huku akionya... “Mradi wasiibe kura zetu.”
Duni aipiga kijembe CCM
Mgombea mwenza, Duni Haji aliirushia kijembe CCM kuwa inafanya wananchi wawe maskini ili iendelee kuwatawala.
Akizungumza
baada ya kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea mwenza, Duni alisema,
CCM haiwezi kuwasaidia wananchi kutoka kwenye umaskini kwa sababu sera
yao ni umaskini.
“Miaka ya 70 hatukuwa na neno
changudoa, jambazi wala panya road. Haya yamekuja kutokana na kushindwa
kwa utawala wa CCM. Ukawa tumedhamiria kuchukua madaraka ya nchi hii ili
kuleta mabadiliko,” alisema.
Alisema wananchi
wamejenga imani na matumaini kwa makubaliano yaliyofanyika jangwani,
walipotia saini hati ya makubaliano inayoruhusu vyama kukubaliana
kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila nafasi ya uongozi katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu.
Akimzungumzia mgombea urais, Duni
alisema: “Siyo jambo rahisi kufanya uamuzi mgumu kama aliofanya Lowassa.
Wengi bado wapo CCM licha ya kuwa hawapendi mfumo wa chama chao,
alichokifanya Lowassa ni ujasiri mkubwa.”
Hata kwake,
alisema halikuwa jambo rahisi kuihama CUF na kujiunga na Chadema.
Alisema kuwa alikubaliana na viongozi wake, Profesa Lipumba na Maalim
Seif Sharif Hamad aende Chadema ili Ukawa ilete ukombozi katika Taifa.
“Profesa
Lipumba ananipenda sana na ananikubali haswa… na anajua kuwa hiki ni
kifaa. Lakini alikubali nijivue uanachama wa CUF ili niende Chadema
kuongeza nguvu ya kuleta mabadiliko, nina imani Ukawa tutashika dola
ifikapo Oktoba 25,” alisema.
Alisisitiza kuwa Ukawa
ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania akisema umoja huo unaungwa
mkono na wananchi wengi, hivyo hana shaka kwamba utashinda katika
uchaguzi ujao.
“Nilikuwa mwanachama wa ASP nilipokuwa
kidato cha pili. Nilipoona mambo yanabadilika nami nilibadilika. Lengo
kuu la kupigania uhuru lilikuwa ni Mwafrika kumtawala Mwafrika mwenzake
ili amlinde, lakini lengo hilo sasa limepotea.
“Ninashangaa
kuona askari wa kimaskini aliyepewa bunduki kuwalinda wananchi,
anageuka na kuwapiga risasi maskini wenzake, huu ni udhalimu
uliotengenezwa na Chama cha Mapinduzi,” alisema.
Ajenda zabadilika
Awali,
Mbowe alitangaza kubadili ajenda za mkutano huo ili kuifanya siku ya
jana kuwa ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wajumbe wa mkutano
kama wanataka kupiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’ au kura ya siri
kupitisha mgombea urais na mgombea mwenza na kujibiwa, “Tunataka kura ya
ndiyo na hapana.”
“Tunapopigania ndoto ya Taifa lazima
tukubaliane kushirikiana na ili ndoto itimie tunamhitaji kila Mtanzania
ambaye yupo tayari kushiriki nasi kutafuta ndoto hiyo, waliopo CCM na
wasio na vyama vya siasa. Tunahitaji Watanzania wa makabila yote, dini
na rangi zote,” alisema Mbowe.
Alisema Mungu yupo na
Chadema na katika aina yake ya utendaji wa miujiza kila jambo
linalotokea katika chama hicho linatokana na mpango wake.
“Ili
tulibadilishe Taifa hili, hatuwezi kujenga uadui wa kudumu. Ili
tuyapate mabadiliko ya kweli tunamhitaji kila mmoja ambaye Mungu amempa
karata zake, nguvu zake na kupewa kidogo na kikubwa na kwa pamoja
tutaunda jeshi la pamoja,” alisema.
Alisema katika safari hiyo wakubaliane kuwa ndoto ya Taifa ni kubwa kuliko mahitaji ya kila mmoja.
“Ushirika
wetu una maana pale ambapo tutakubaliana kila mmoja wetu kwa nafasi
yake, kuanzia udiwani, ubunge na urais na kazi nyingine yoyote ya
kuongoza Watanzania.
“Haya mambo (ya kusimamisha
mgombea mmoja) yanahitaji kujitoa, ndoto ya Taifa haiwezi ikatimia kama
kila mmoja atatanguliza matakwa yake binafsi. Fursa ni nadra na hiyo
fursa inayopatikana kwa u-nadra huo isipotumika historia itatuhukumu,”
alisema.
Alisema viongozi wa Chadema ni lazima
wajitolee ili kwa pamoja, kupitia Ukawa waweze kufika safari yenye
malengo ya kutimiza ndoto ya Taifa.
“Lakini ndoto hii si ya mtu mmojammoja, familia mojamoja au ukoo. Ni ndoto ya Taifa,” alisema.
Alisema
Chadema kinapokea wanachama kutoka chama chochote wenye malengo safi na
kuwa kwa miaka 25, kimepigana kuingia Ikulu huku viongozi wake
wakijitolea.
“Kwenye safari hiyo ya miaka 25 wapo
waliokufa, waliopata vilema, waliofukuzwa kazi kwa kusimamia
walichokiamini, waliofungwa magerezani na wapo waliohama nchi. Safari
hii haikuongozwa na Chadema pekee, iliongozwa na vyama vyote vinavyounda
Ukawa.
“Wapo tunaowaita magamba nao wakaamua kimagamba
magamba wafunge safari ya matumaini. Wakafunga safari yao wakiitafuta
haki na kweli katika nchi hii,” alisema Mbowe.
Alisema
walioanza safari ya matumaini waliongozwa na dhamira kwa lengo la
kujitoa unyonge na kujifungua minyororo ya chama chao, ili kuitafuta
haki na dhamira yao nje ya chama chao.
“Chadema na
Ukawa nchi nzima, watu hawa (walioanza safari ya matumaini) hatuna haki
na sababu ya kuwahukumu, tuna kila sababu ya kuwatia moyo na kuwaunga
mkono na kuwakaribisha miongoni mwetu ili ndoto ya Taifa hili ikatimie,”
alisema.
Alisema wanaojiunga Chadema na waliopo ndani
ya chama hicho wote ni binadamu na kwamba watakaojiunga na chama hicho
na Ukawa wataishi kama wanavyoishi wanachama wa vyama vinavyounda umoja
huo.
“Sisemi wanaokuja Chadema hawana dhambi wote, hata
sisi wana–Chadema tuna dhambi zetu, uongo?” aliuliza Mbowe na kujibiwa
na wanachama, ‘ndiyooo.’
“Sisi ni nani, hiki ni chama cha siasa na siasa ni watu. Chama cha siasa si mahakama.”
Alisema
kuna kila sababu ya chama hicho kujenga utamaduni uliozoeleka wa
kuwakaribisha Watanzania wengine katika chama hicho ambao wanaamini
kupitia Chadema na Ukawa kuwa ndoto ya Taifa inakwenda kutimia.
Alisema
Chadema imejengwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na kifamilia na
ndani ya chama hicho, hakuna aliye mkubwa kuliko mwingine.
“Tukikubaliana
kusonga mbele tunasonga mbele. Mnaokuja Chadema tusaidieni kulinda
umoja wetu na yale mabaya mliyokuwa nayo katika chama chetu cha zamani
tumewasamehe na huku mtuletee mazuri yote mliyopata katika chama chenu
cha zamani...”
“Vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi ni magari na madaraja ya kutuvusha kwenda katika ndoto ya Taifa.
“Watu
wanashangaa leo kuambiwa kuwa Duni ndiyo mgombea mwenza wa Ukawa. Huyu
(Duni) mpaka jana (juzi), alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar ila kwa sababu ya uzito wa ndoto ya Taifa, ameona ajiuzulu
uwaziri ili kusaidia kufanikisha ndoto,” alisema.
Akizungumzia
katiba ya chama hicho kuhusu kupitisha mgombea urais alisema, “Katiba
ya Chadema imetoa maelekeo jinsi ya kumpata mgombea urais na mgombea
mwenza. Kifungu cha 7.16, kinazungumzia kazi za Kamati Kuu, ikiwamo ya
kufanya utafiti wa wagombea wa urais na mwenza na kuwasilisha ripoti kwa
Baraza Kuu kwa ajili ya mapendekezo kwa Mkutano Mkuu. Kamati Kuu
ilifanya utafiti.”
Alisema katika utafiti huo, Kamati
Kuu kwa kauli moja, ilipendekeza kwa Baraza Kuu la chama hicho Lowassa
kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na ikapendekeza vyama
vinavyounda Ukawa kutoa mapendekezo yao kuhusu uamuzi huo.
“Halikuwa
jambo jepesi na tulipishana kauli hadi usiku wa manane. Utafiti wetu
mbalimbali ulituambia kwamba Lowassa akipeperusha bendera kupitia Ukawa
na kundi lake kubwa ndani ya CCM ndoto za Taifa hili zinakwenda
kutimia.”
“Wote, akiwamo Dk Slaa walikubali.
Tulimwalika Lowassa katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema na kumhoji,
pengine watu wa pembeni walishauri tofauti lakini vikao vya chama
viliamua kuwa Lowassa ndiyo mgombea,” alisema.
Akizungumza
wakati akifunga mkutano huo alisema, “Tumekubaliana kuunganisha nguvu
kwa utaratibu huu, wapo wabunge ambao watakosa nafasi, watakaokosa
nafasi naomba tuvumiliane na hii ni kwa wanaogombea udiwani, ubunge na
urais. Watu ni wengi na utaratibu huu lazima utawaacha wengine kando.
Watakaoachwa waendeleze moto wa kukiimarisha chama.”
Mkutano wenyewe
Mkutano
huo ulianza kwa wajumbe wengi kutiririka katika eneo la ukumbi huo
kuanzia saa tatu asubuhi wakisubiri kugawiwa sare za mkutano huku
asilimia kubwa wakiwa wamevaa vitambulisho vyenye picha na maandishi...
‘Lowassa 2015.’
Viongozi wakuu na wageni maalumu
walianza kuwasili saa 4:10 asubuhi wakiongozana na Kaimu Katibu Mkuu,
Salum Mwalimu na kufuatiwa na wenyeviti wenza wa Ukawa, Maalim Seif na
Mbowe.
Wafanyabiashara nao hawakusita kutafuta riziki
pale walipojitokeza kuuza nguo na mapambo mbalimbali kama skafu, kofia,
beji na mabango yenye picha ya Lowassa.
Tofauti na
ilivyozoeleka, idadi ya wafuasi nje ya ukumbi haikuwa kubwa kumsindikiza
Lowassa na hata alipoingia saa 5.25 asubuhi hawakuwa wameugundua
msafara na baada ya kung’amua walianza kuimba “rais, rais, rais.”
Asilimia
kubwa ya wafuasi waliojitokeza, walivalia fulana za chama hicho zenye
mistari ya rangi nyekundu, nyeupe, bluu na nyeusi huku wengine wakiwa
wamevalia fulana zenye maandishi ya 4u Movement na “Zuia goli la mkono
2015”.
Barabara ya Sam Nujoma, hadi eneo lote la
Mlimani City ulipokuwa ukifanyika mkutano huo lilipambwa kwa bendera za
Chadema na kuchagizwa na sare na wajumbe hao kiasi cha kufanya rangi
zinazotumiwa na chama hicho kutawala.
Ulinzi
uliimarishwa kila kona ukihusisha askari polisi na walinzi wa chama
hicho, “Red Brigade” ambao walikuwa na kazi ya kuwarudisha nyuma wafuasi
waliokuwa wakiwakimbilia viongozi mbalimbali kwenda kuwasalimia.
Eneo lote la Mlimani City lilijaa magari kiasi cha baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kukosa maegesho na kulazimika kuegesha nje.
Kabla
ya kumkaribisha Mbowe, Mwalimu alielezea shughuli na mikakati
mbalimbali iliyofanywa na chama hicho katika kujiimarisha na kuongeza
uimara na Ukawa.
Alisema Ofisi ya Katibu Mkuu ilifanya
mambo makuu matatu ambayo ni kutoa hamasa kwa makada wote, kufanya
oganaizesheni mbalimbali za chama na kutekeleza agizo la kufanya usajili
wa makada wapya kutoka vyama vingine, hususan CCM.
Katika oganaizesheni, alisema walifanya mafunzo kwa viongozi wote wa chama na watiania na kuimarisha kanda 10 za chama hicho.
Huku
akifananisha usajili wa wafuasi kutoka vyama vingine kuingia Chadema na
usajili wa mpira wa miguu barani Ulaya, Mwalimu alisema:
“Mheshimiwa
mwenyekiti usajili uliotufanyia katika dakika za majeruhi siyo ushindi
wa ligi kuu pekee, bali wa ligi ya mabingwa Ulaya.”
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Bakari, Nuzulak Dausen na Peter Elias
Chanzo cha habari na gazeti makini la kila siku la mwananchi
Chanzo cha habari na gazeti makini la kila siku la mwananchi
Post a Comment