Na Damas Makangale, Makangale Satellite Blog
“Kila mwaka idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini hasa kwa vijana wenye umri mdogo kabisa kati ya miaka 15 mpaka 25 inakadiliwa kufika 10,000 hadi 11,000 kila mwaka nchini ni idadi kubwa na hali inatisha,’ anasema Afisa kutoka Kitengo cha Kudhibiti dawa za kulevya nchini, Moza Makumbuli
Wiki
iliyopita Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini ( Drug Control Commission)
kiliandaa semina ya siku moja kwa wadau mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya
habari, magereza, Polisi, Mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali, Madaktari na
wizara ya afya na lengo la semina hiyo ilikuwa kuwapa wadau matokeo ya utafiti ya
watumiaji wa dawa za kulevya cocaine na heroin nchini.
Akizungumza
na wanasemina hiyo, Bi Makumbuli amesema kwamba utafiti huo ulifanyika katika
mikoa 12 ya Tanzania bara kwa kufanya mahojiano na watumiaji, waathirika,
wananchi wa kawaida, polisi na watu mbalimbali pamoja na watoa taarifa ikiwemo
na utafiti wa mahali husika.
Amesema
kwamba utafiti huo ulifanyika katika mikoa ya Mtwara, Dodoma, Morogoro, Pwani,
Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Shinyanga, Geita na kigoma.
Lengo
linguine la utafiti huo wa kisayansi ni kuongeza uelewa wa athari za matumizi
ya dawa za kulevya, hatari ya watumiaji kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi
na tatizo la wagonjwa wa akili nchini inayochangiwa na matumizi ya dawa za
kulevya nchini.
Bi
Makumbuli aliongeza kwamba matumizi ya dawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga
kwa sindano imeongezeka maradufu Duniani na Kusini Mwa Jangwa La Sahara ambapo
takribani watu milioni 13 wanatumia dawa hizo za kulevya kati ya heroin na
cocaine duniani na kusini mwa jangwa la sahara takribani watu milioni 1.5 wapo
kwenye matumizi ya dawa hizo.
Alifafanua
kwamba tatizo la madawa ya kulevya nchini halikupata nafasi ya kuhifadhi
kitakwimu au taarifa zake nyingi hazijapata nafasi ya kuwekwa vizuri kwenye
kumbukumbu (Well documented) kwa muda mrefu na ndiyo kikwazo kwa serikali
kuamua, kupanga na kuchangua mikakati madhubuti ya kupambana na ongezeko hilo
la uuzwaji na utumiaji wa madawa hayo ya kulevya nchini.
“kwenye
utafiti wetu tumegundua kwamba sehemu nyingi za pwani (Coast Region) na
pembezoni mwa barabara (Along the road corridor) zimeathirika sana kwa vijana
wengi kujihusisha na uuzwaji na utumiaji wa madawa hayo ya kulevya na wengi
kazi zao ni makodakta wa daladala, wapiga debe, wavuvi sehemu za pwani na
wengine ni vibaka na wanawake wanajihusisha na biashara ya ukahaba,” aliongeza.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Programu ya kudhibiti dawa za kulevya kutoka kitengo
hicho cha serikali, Bw Joel Ndayongeje amesema kwamba mapambano dhidi ya dawa
za kulevya bado yana safari ndefu hapa Tanzania kutokana na kusongwa na vikwazo
lukuki vikiwamo vya sheria dhaifu, ukosefu wa sera ya Taifa ya udhibiti na
kuendekezwa kwa vitendo vya rushwa katika vyombo vya dola.
Bw
Ndayongeje aliongeza kwamba kwenye utafiti wao waligundua pia mikoa inayoongoza
kwa matumizi makubwa ya dawa za kulevya nchini ni 5,190, Tanga, 3,300 Mwanza, 2,700 Arusha, 1,539
Morogoro, 1,096 Dodoma, 820 Mbeya, 563 Kilimanjaro, 319 Shinyanga, 108 Geita,
100 Kigoma na watu 65 mtwara.
Amesema
kwamba katika miaka ya hivi karibuni matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake
yameongezeka mara ya mwisho ulifanyika na kupata matokeo ya asilimia 6% lakini
utafiti wa hivi karibuni kwa kushirikiana na Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na
magonjwa cha wa marekani (US Centres for Disease and Prevention (CDC) nchini
idadi ya wanawake kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sasa ni asilimia 20%
Pamoja
na mambo mengine Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwahi kukiri kuwa
tatizo la dawa za kulevya hapa nchini ni kubwa, linalohitaji nguvu kubwa ya
mataifa yote duniani.
“Mapambano
dhidi ya dawa za kulevya hayatafanikishwa na nchi moja bali nchi zote duniani,”
amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akiliahirisha Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Septemba 6, mwaka jana.
Kutokana
na ukubwa wa tatizo hilo, Pinda anasema Serikali inafikiria kuanzisha mahakama
maalumu ili kuharakisha mashauri ya dawa za kulevya.
“Nina
imani tukijipanga vizuri inawezekana… tutafika mahala tufikirie mahakama
maalumu ya dawa za kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu ya kusimamia mashauri
yanayohusu dawa za kulevya,” anasema.
Kadhalika,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi, anasema Serikali inaandaa mapendekezo ya kufuta Sheria ya Dawa
za Kulevya na kutungwa mpya itakayokidhi mahitaji ya kushughulikia ipasavyo
makosa ya dawa za kulevya.
Wakati
Serikali ikitangaza msimamo wake huo, meli iliyosajiliwa Tanzania (upande wa
Zanzibar) iliripotiwa kukamatwa nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa
za kulevya zenye thamani ya paundi milioni 50, sawa na Sh bilioni 123 za
Tanzania.
Kutokana
na mazingira hayo, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini (DCC)
kwa upande wake, inaona pia kuna haja ya Serikali kutangaza dawa za kulevya
kuwa adui namba moja kama hatua mojawapo ya kuonesha ukubwa wa tatizo hilo hapa
nchini lakini watafanya hivyo endapo tu kutakuwa na ushahidi wa kitafiti na
kitakwimu ili kuweza kujenga hoja hiyo.
Heroin
na madhara yake
Heroin
ni aina ya dawa ya kulevya ya unga inayopumbaza mfumo wa fahamu. Dawa hiyo
inatokana na mmea uitwao ‘opium poppy’. Imekuwa ikiingizwa hapa Tanzania
ikitokea nchi za Mashariki ya mbali.
Mitaani
heroin huitwa majina mengi kama vile unga, brown shugar, ngoma, ubuyu, mondo,
ponda, dume, farasi, n.k.
Cocaine
na madhara yake
cocaine
ni dawa ya kulevya inayotengenezwa kutokana na mmea wa coca ambao hustawi zaidi
katika nchi za Amerika ya Kusini. Kitaalamu mmea huo hujulikana kwa jina la
erythroxylon coca.
Cocaine,
kwa mujibu wa watafiti , huwa katika unga mweupe au katika hali ya mawe madogo
madogo. Inajulikana kwa majina mengi kama vile snow, star dust, keki, unga, big
c, bazooka, white sugar na unga mweupe.
Hapa
Tanzania cocaine hupatikana kwa shida kwa sababu ya bei yake ni nadra sana
kupatikana nchini.
Anataja
madhara ya cocaine kuwa ni kuathiri mfumo wa fahamu wa binadamu, kutokwa na
damu puani, kuwa na mafua makali yasiyopona, kukosa hamu ya chakula, kupanuka
kwa mboni za macho, mchafuko wa damu na kupata majipu, kuongezeka kwa mapigo ya
moyo na shinikizo la damu.
Madhara
mengine ya cocaine ni mtu kuchanganyikiwa, kukosa ufanisi kazini, kuwa na hisia
za kuwapo kwa vijidudu mwilini, magonjwa ya ini, kuharibika kwa mishipa ya
fahamu, kuharibika kwa moyo, figo na mapafu, kikohozi cha muda mrefu, kupasuka
kwa mishipa ya damu kichwani kunakoweza kusababisha kiharusi au kifo na kumweka
mtu katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi.
Mwisho.
Post a Comment