Zahanati mpya yazinduliwa katika kijiji cha Mangucha..

Na Mwandishi Wetu, Tarime 

Katika hafla ya kukabidhiwa zahanati ya wananchi wa mangucha moja ya kijiji kilichopo Jirani na mgodi wa dhahabu wa North Mara Wilayani , Tarime walionekana kkuwa na nyuso za furaha na matumaini ya kuondokana na changamoto ya kutembelea mwendo mrefu kufuata huduma za afya.

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilikabidhiwa zahanati ya Kijiji ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 164 zilizotokana na fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Barrick North Mara unaoendeshwa na kampuni Barrick kwa ubia na serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Ufanikisha wa mradi huu ni moja ya utekelezaji wa mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick unaojumuisha ushirikiano na wadau na vipaumbele ambavyo vimelenga kufanikisha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyopo Jirani na migodi yake sambamba na kufanikisha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).

Akiongea wakati  wa hafla ya makabidhiano ya zahanati hiyo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime,Albinus Kirina,alisema kukamilika kwa ujenzi wa zahanati ya Mangucha kutawaondolea wakazi 4,460 wa kijiji hicho adha waliyokuwa nayo ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya nje ya kijiji hicho.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime (DAS) Saul Mwaisenye, alisema ujenzi wa zahanati hiyo umezingatia viwango vya ubora na thamani ya fedha iliyotumika (value for money).”Nimeridhika na ujenzi wa zahanati hii ndio maana nimekata utepe  na kuruhusu Mgodi na Halmashauri kutiliana saini za makabidhiano haya”alisema Mwaisenye akiyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Tarime,Meja Edward Gowele kama Mgeni Rasmi.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime (DAS) Saul Mwaisenye (wa pili kutoka kushoto) akikata utepe katika hafla ya uzinduzi wa zanati ya Mangucha iliyojengwa na mgodi wa Barrick North Mara,wengine pichani wa kwanza ksuhoto ni Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara , Francis Uhadi na wa tatu kulia ni Mbunge wa Tarime Vijijini , Mwita Waitara na viongozi wengine wa wilaya ya Tarime na Mgodi katika hafla ya makabidhiano ilifanyika mwanzoni mwa wiki kijijini Mangucha.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliitaka idara ya afya kutumia baadhi ya vyumba vya zahanati hiyo kwa ajili ya huduma za wanawake wanaojifungua wakati ujenzi wa majengo ya mama na mtoto na miundombinu ya kichoma taka yakisubiriwa.“Haitakuwa na maana kama akina mama hawatapata huduma za kujifungulia hapa,” alisema Mbunge Waitara.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, naye aliushukuru Mgodi wa Barrick North Mara na kuahidi kuendelea kuupatia ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mingine ya CSR ndani ya halmashauri hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard, aliishukuru Barrick North Mara kwa kuwezesha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imesogeza huduma za afya jirani na wananchi wa Mangucha.“Tunawashukuru sana watu wa Mgodi wa Barrick North Mara na tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa mgodi,” alisema Diwani Tiboche.

Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (kushoto) akiongoza ujumbe wa viongozi wa Serikali wilaya  ya Tarime kutembelea maeneo ya zahanati ya Mangucha iliyojengwa na Fedha za CSR zilizotolewa na mgodi huo wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika mwanzoni mwa wiki.

Awali, Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, alisema afya ni moja ya sekta ambazo wanazipa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi inayogharimiwa na fedha za mpango wao wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

"Sekta ya afya ni ya pili kwa ukubwa wa uwekezaji wa CSR, ikiwa na asilimia 20 ya fedha zote tulizowekeza hadi sasa. Tangu mwaka 2020 hadi sasa, mgodi umewekeza shilingi bilioni 5.4 katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi na vifaa tiba.

"Kwa mwaka 2025, tunatekeleza miradi 21 ya afya yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Miradi mingi ipo kwenye hatua za mwisho, ikiwemo huu wa Zahanati ya Mangucha uliokamilika kwa asilimia 100, na mingine itaendelea kukabidhiwa kwa halmashauri kadiri inavyokamilika.

“Makabidhiano ya zahanati hii ni ushahidi wa mafanikio tunayoyapata kupitia utekelezaji wa miradi ya CSR kwa ushirikiano wa karibu kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema Uhadi.

Akizungumza kwa niaba ya wana-Mangucha, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Kemahi Irumbe Mgesi,alitoa shukrani kwa kujengewa zahanati hiyo na aliahidi kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu yake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Ripoti ya utekelezaji Mkakati Endelevu ya mwaka 2024 ya kampuni ya Barrick Mining Corporation iliyotolewa karibuni imebainisha mafanikio muhimu yaliyopatikana katika uendeshaji wa shughuli zake katika mataifa mbalimbali duniani.

Mafanikio muhimu endelevu yaliyopatikana yaliyobainishwa katika ripoti hiyo ni kampuni kuwekeza katika matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala,Uwezeshaji biashara katika maeneo yake ya kazi,miradi ya jamii na Serikali, na kuunda ushirikiano na jamii zinazoishi Jirani na maeneo yake ya kazi kwa kutekeleza miradi ya kujenga shule,vituo vya afya,upatikanaji wa maji safi ya kunywa na miundombinu mingine muhimu-pamoja na uwekezaji katika kuwezesha upatikanaji wa walimu bora,wauguzi na vifaa vinavyohitajika kuboresha upatikanaji wa huduma hizo.

Mwisho