Dk. Tulia Ackson akijinadi Novemba 17, 2015 katika kuwania nafasi ya Unaibu Spika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015
Dk Tulia Ackson huenda akawa mmoja wa Watanzania wachache wenye bahati ya kupata vyeo tofauti vya juu nchini ndani ya siku 67.

Katika kipindi hicho kifupi, Dk Tulia amepata fursa ya kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete Septemba 9, mwaka huu.

Cheo hicho amekitumikia kwa takriban miezi miwili akifanya kazi ya kuitetea na kushughulikia masuala ya kisheria yanayoihusu Serikali katika masuala mbalimbali, ikiwamo ya kuongoza jopo la mawakili wa Serikali katika kesi iliyovuta hisia za wengi ya kuomba tafsiri ya mahakama juu ya kifungu namba 104(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 iliyorejewa mwaka 2010.

Kesi hiyo ya kikatiba maarufu kwa jina la “kesi ya mita 200” ilifunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na mpigakura Amy Kibatala na baadaye Serikali ilishinda kutokana na Mahakama kuzuia watu kufanya mikusanyiko wala kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.

Wakati wengi wakitafakari ushindi wa Serikali kuhusu kesi hiyo iliyoendeshwa ndani ya wiki ya mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, Dk Tulia aliamua kusaka nafasi nyingine ya juu ya muhimili mwingine wa dola ya uspika wa Bunge kupitia CCM.

Novemba 13, alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na siku mbili baadaye aliteuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho akiingia kwenye ‘tatu bora’ akiwa na makada wenzake Job Ndugai na Abdullah Mwinyi.

Wakati akiwa na fursa ya uwezekano wa kuteuliwa na wabunge wa CCM kuwa mgombea wa uspika, jana asubuhi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge akiwa wa kwanza kati ya nafasi 10 alizonazo Rais kikatiba.

Uteuzi huo ulisababisha Rais atengue rasmi cheo cha Naibu Mwanasheria Mkuu alichokuwa akikishikilia.

Ndani ya saa chache za kuwa mbunge, Dk Tulia ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alijiengua kugombea uspika pamoja na Mwinyi na kumwachia Naibu Spika wa zamani, Ndugai.

Kujitoa kwa Dk Tulia hakukuwa mwisho wa safari ya kuwania cheo cha juu ndani ya Bunge na badala yake alikwenda kuchukua fomu ya kuwania unaibu spika kupitia chama hicho.

Kwa mantiki hiyo, kwa kuwa wabunge wa CCM wamempitisha kuwa mgombea wao wa nafasi ya naibu spika, hapana shaka kuwa ndiye mwenye nafasi kubwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la 11 kutokana na chama hicho kuwa na wabunge 252 kati ya 394 wa Bunge hilo.

Kitendo cha Dk Tulia kujitosa kugombea nafasi ya spika wa Bunge na hatimaye naibu spika kama kada wa CCM akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimezua maoni tofauti miongoni mwa wachambuzi wa siasa na sheria, wengi wakieleza kuwa ni mbinu za CCM kujijenga ndani ya mihimili ya dola ambayo ni Mahakama, Bunge na Serikali.

Wachambuzi hao walisema tafsiri ya taswira iliyoonyeshwa na mwanasheria huyo imeendelea kudhihirisha kwamba, kila unapofanyika uteuzi wa majaji au wanasheria wa Serikali lazima ulenge kulinda masilahi ya chama kilichopo madarakani.

Profesa Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kikatiba suala la kugombea uspika linatoa nafasi kwa kila Mtanzania mwenye sifa na siyo lazima awe kada wa chama cha siasa.

“Kwa hivyo inawezekana Mwanasheria Mkuu wa Serikali akagombea nafasi hiyo na asiwe anatokana na chama tawala,” alisema.

Hata hivyo, alifafanua kwamba watumishi wanaopewa nafasi za juu za mihimili hiyo ya dola hutazamwa kwa jicho la kulinda masilahi ya CCM.

Mtaalamu huyo wa masuala ya utawala alisema hali hiyo itaendelea kuwapo hadi chama hicho kitakapoondoka madarakani na kuingia chama kingine madarakani.

Kwa upande wake, mwanasheria wa kujitegemea kutoka Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff alisema asilimia kubwa ya uteuzi wa nafasi ya mwanasheria wa Serikali imejengewa msingi wa kulinda masilahi ya CCM.

Profesa Sheriff alisema CCM bado imeshika ‘hatamu’ licha ya kuwapo majaji waliowahi kuonyesha msimamo wa kutoyumbishwa na mfumo huo na badala yake wakasimama katikati wakati wa kutekeleza majukumu yao.

“Kuna Jaji Robert Kisanga na marehemu Jaji Fransic Nyalali walionyesha msimamo wao wazi. Mifano iko mingi ya utendaji wao, lakini wapo majaji ambao walitimiza wajibu wao wakati bado ni makada, mfano Jaji Agustino Ramadhan alipojitokeza kuwani urais ilijenga maswali kwa muhimili wa Mahakama,” alisema.

Alifafanua kwamba udhaifu huo ungeweza kuondolewa na Katiba Mpya iliyokuwa na mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Warioba. “Miiko ya utumishi wa umma ilibainishwa wazi kwenye rasimu hiyo na ingeweza kurejesha nidhamu na kuondoa udhaifu huo, lakini haikufanikiwa,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Profesa Abdallah Safari alisema pamoja na sheria kutoa nafasi kwa kila mmoja kuwania uspika, lakini imeonyesha udhaifu kwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwania nafasi hiyo.

Alisema udhaifu wa mfumo wa Serikali kujengwa na chama umesababisha kuwapo na ukandamizaji wa haki kwa vyama vingine vya siasa.

“Kwa mfumo ulivyo ni wazi hakuna mchakato bora wa kidemokrasia na tumepigania sana suala la udhaifu wa mfumo huo,” alisisitiza.

Profesa Safari alisema juhudi za kupambana na udhaifu huo ni kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na siyo suala la Katiba kutokana na mazingira magumu yaliyojitokeza katika upatikanaji wake.

Alisema mihimili yote imetekwa na CCM kwa sasa, hivyo hakuna mahali pa kukimbilia.

Profesa Safari alisema hakuna mfano wa kesi ya kisiasa kubwa iliyowahi kushinda upinzani mahakamani na badala yake kesi ndogondogo ndizo umekuwa ukishinda. “Kesi ya mgombea binafsi iliishia wapi? Baadaye majaji hao tunawaona kwenye urais CCM.

Binafsi mtanisamehe, sitaamini chombo cha Mahakama kwa kesi kubwa ya kisiasa ambayo itakuwa na masilahi kwa CCM, mfano imeonekana kwenye kesi ya mita 200 na nilitaka kuwazuia kwani nilijua wangepoteza muda tu,” alisema.
MWANANCHI
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.