ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amestaafu rasmi na kuagwa jana huku akikiri kuwa hatasahau joto la uchaguzi mkuu 2015 lililosababishwa zaidi na mchuano wa wafuasi wa wagombea urais John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akizungumza wakati wa kuagwa kwake na kisha kukabidhi majukumu kwa kamanda mpya wa kanda hiyo, Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, Kova alisema uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015 ni miongoni mwa vipindi vitatu asivyotarajia kuvisahau katika maisha yake yote ya kulitumikia jeshi la polisi.

Alivitaja vipindi vingine asivyovisahau wakati akilitumikia jeshi la polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa ni tukio la kuvamiwa kwa kituo cha polisi Stakishari lililoacha vifo kwa baadhi ya askari wake na pia ajali ya helikopta.

Akieleza zaidi kuhusiana na uchaguzi mkuu, Kova alisema uchaguzi huo ulimpa changamoto kubwa kutokana na wagombea hao kuungwa mkono na watu wengi kiasi cha kuhofia kutokea machafuko, hasa kutokana na kuwapo kwa mwamko mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wafuasi wa wagombea.
Hata hivyo, Kova alisema anashukuru kuwa serikali iliwaunga mkono vya kutosha katika kulinda usalama na hivyo kufanikisha uchaguzi huo kwa ufanisi.

“Napenda kuishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia jeshi la polisi wakati wa uchaguzi kwa kutuongezea vifaa vya kazi kama magari ya kufanyia doria, silaha pamoja, kwani vilituwezesha kufanikiwa kulinda amani na utulivu wa hali ya juu,” alisema Kova.

Akisimulia safari yake ndani ya jeshi la polisi kwa ufupi, Kamanda Kova alisema kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Kandaa Maalumu ya Dar es Salaam, aliwahi kuwa katika idara ya upelelezi kwenye mikoa ya Arusha, Kigoma, Mwanza, Kinondoni (Magomeni) na baadaye kuwa Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Mbeya. 

“Nina utumishi wa miaka 40 ndani ya jeshi la polisi na nilikuja kuwa Mkuu wa Polisi wa Jiji la Dar es Salaam (RPC) nikitokea Mbeya mwaka 2008,” alisema.

MATUKIO 

Akielezea matukio ya ajali ya helikopta na uvamizi Stakishari, Kova alisema hayo hatayasahau kama ilivyokuwa kwa mikikimikiki ya uchaguzi mkuu 2015.

Alisema tukio la Stakishariu lililowapoteza askari wanne hatalisahahu kwani hapo kabla alizoea kukabiliana na vitendo vya ujambazi vinavyohusisha uporaji wa fedha na mali na siyo ugaidi wa kuiba silaha kwenye vituo vya polisi.

Hata hivyo, alisema anafarijika kuona kuwa kwa kushirikiana vya kutosha ndani ya jeshi lao Kanda maaalum ya Dar es Salaam aliyokuwa akiiongoza, walifanikiwa kuwakamata wahusika wote waliofanya tukio hilo. 

Alisema tukio jingine ni kuanguka kwa helikopta wakati wa kutembelea wananchi waliokumbwa na mafuriko mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, akiwa pamoja na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, John Magufuli na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.
Simon Sirro
Simon Sirro
AMTAMBULISHA KAMANDA SIRRO 

Kamanda Kova alimtambulisha rasmi Naibu Kamishna wa Polisi Sirro, kuwa mrithi wa wadhifa wake.

Akiongea na waandishi wa habari juu ya hatua hiyo, Kova alisema kwake yeye, kukabidhi madaraka kwa Kamanda Sirro ni kitendo cha kihistoria kwani ilikuwa ni ishara ya kuhitimisha salama utumishi wake ndani ya jeshi hilo. 

“Ni siku ya kihistoria katika maisha yangu kutokana na tendo hili. Lakini naahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kila namna kwa Kamishna Sirro,” alisema

AKABIDHI VYETI

Katika hatua nyingine, Kova alikabidhi vyeti kwa maofisa 110 wa jeshi la polisi kutokana na utendaji wao katika hafla ya kumuaga.

Alitumia fursa hiyo kufanya ukaguzi wa baadhi ya vitu vilivyokamatwa na jeshi la polisi yakiwamo meno ya tembo, gari mbili, moja likiwa aina ya Toyota Ford liliibwa nchini Afrika Kusini na Toyota Toyota GX210 ambayo yote yalikamatwa eneo la Buguruni Jijini Dar es Salaam.

Kova alimtaka mrithi wake, Kamanda Sirro kufuata nyayo za uongozi wake kwa kuendeleza amani na utulivu katika jiji la dare s Salaam kwa kuhakikisha idadi ya matukio inaendelea kuwa ndogo zaidi.

Kwa upande wake Kamanda Sirro alimsifu Kamanda Kova kwa kazi yake nzuri aliyofanya kwa muda wote alipokuwa wakifanya kazi pamoja na kusema kuwa alikuwa kama mwalimu kwa kila afisa wa jeshi hilo kwa muda mrefu wa utumishi wake.

Alisema kuwa amefanya kazi kama kaimu wake wa kanda hiyo kwa miaka miwili, na kwa muda wote huo kanda hiyo ilikuwa shwari bila kuwepo na wimbi la machafuko.

“Nimefanya naye kazi vizuri kwa miaka isiyozidi miwili na amekuwa mwalimu kwangu na siyo kiongozi tu… ninachoweza kumuahidi ni kuwa nitaendeleza jitihada za kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.