Vyombo vya habari nchini hususani redio za kijamii zimetakiwa kuandika habari ambazo zinaelezea changamoto ambazo zinawakabili wananchi katika maisha yao ya kila siku na jinsi ambavyo wanaweza kuzitatua.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu wajibu wa redio za kijamii kwa maendeleo vijinini ambayo yamehusisha wasimamizi wa redio za kijamii na wawakilishi wa Halmashauri wa wilaya hizo ambao wanawakilisha halmashauri zao katika shughuli za uendeshaji wa redio hizo za jamii.
Alisema wanahabari na vyombo vya habari ni muhimu nchini kwa maendeleo ya Taifa lakini kama wasipokuwa makini katika utendaji wao wa kazi kunaweza kuwa na madhara makubwa hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanazingatia maadili ya uandishi wa habari.

Alisema sehemu kubwa ya wananchi ambao wanaishi vijijini hawapati taarifa muhimu zinazohusu maendeleo yao zikiwepo taarifa za kilimo, afya, mazingira na haki za kibadamu hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanaandika habari ambazo wananchi wamekuwa hawazipati kwa muda mrefu.
“Ni jukumu lenu sasa kuhakikisha redio hizo zinatimiza malengo yake hususani katika kumuelimisha wanajamii, kuwajengea uwezo wa kutambua na kupambana na mazingira ili kuinua hali zao za kimaisha,” Mhe. alisema Wambura.
Alisema mafunzo hiyo ni muhimu kwao kama wawakilishi wa redio za kijamii sababu itawapa mbinu ambazo wanaweza kuzitumia ili waweze kujisimamia wao wenyewe bila kuwa tegemezi kwa kuomba fedha kutoka sehemu zingine.

“Natambua changamoto zilizopo katika uendeshaji wa redio za kijamii ambazo ni kama upatikanji wa habari endelevu na zinazolingana na mahitaji ya jamii husika, uhaba wa rasilimali fedha za kuendeshea redio husika, na udhaifu katika usimamizi stahiki wa taasisi hizo lakini kwa hakika mafunzo haya ni muhimu kwa vile yanalenga kutatua changamoto hizo,” alisema Wambura.
Aidha Naibu Waziri Wambura amewashukuru Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kutoa mafunzo hayo ambayo yatasaidia kujenga Taifa lenye waandishi na wasimamizi wa habari wenye weledi na kazi zao pia mafunzo hayo yanakwenda sambamba na dira ya wizara ya kuwa na Taifa lililohabarishwa vizuri ifikapo 2025.


“ESRF kwa ufadhili wa UNDP ilisimamia uanzishwaji wa redio jamii nne ambazo ni Redio Unyanja (Nyasa), Redio Bunda (Bunda), Redio Kagera (Bukoba Vijijini) na Redio Ileje (Ileje) na redio zingine mbili Redio Sengerema (Sengerema) na Redio Mazingira (Bunda) zilipata misaada mbalimbali kwa ajili ya kujiendesha,” alisema Dk. Kida.
Mafunzo hayo yamehusisha wasimamizi wa redio za kijamii kutoka wilaya tano nchini ambazo ni Ileje, Bukoba Vijijini, Bunda, Nyasa na Sengerema pamoja na wawakilishi wa halmashauri wa wilaya hizo ambao wanawakilisha halmashauri zao katika shughuli za uendeshaji wa redio hizo za jamii.









Post a Comment