Mpaka sasa Tsh 8 billioni zimetolewa kwa malipo ya mrahaba  

‎Na Mwandishi Wetu, Tarime 

‎Miradi mipya ya kijamii imeanza kutekelezwa kwa kasi katika vijiji vitano kutokana na fedha za gawio wa mrabaha wa asilimia moja zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika miaka ya hivi karibuni  ambazo zimekuwa zinawekwa kwenye akaunti za benki kwa muda mrefu bila matumizi ya yoyote ili kuleta matokeo Chanya kwa wananchi.


‎Kila robo ya mwaka  vijiji vya Genkuru, Nyangoto, Kerende, Nyamwaga na Kewanja ambavyo vipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara vimekuwa vikipokea gawio la mrabaha kutokana na  haki ya kuchimba dhahabu katika shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya Mgodi wa Barrick North Mara) kabla ya kampuni ya Barrick kukabidhiwa kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.

‎‎Wakizungumza na waandishi wa habari jana, viongozi wa vijiji hivyo walisema fedha hizo za mrabaha zimeelekezwa kwenye miradi ya kijamii inayogusa mahitaji ya wananchi wengi.

‎‎Katika kijiji cha Genkuru pekee, zaidi ya Tsh 2 bilioni zilizotokana na mrabaha zimeelekezwa kwenye ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya elimu, afya, barabara na ununuzi wa eneo la kujenga soko. “Tulianza na ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 7.8  na nyingine yenye urefu wa kilomita zaidi ya tatu inayounganisha kijiji chetu cha Genkuru na kijiji jirani cha Msege, na utekelezaji wa miradi hii umefikia asilimia 90.

‎“Kwa upande mwingine, tumetumia sehemu ya fedha yetu ya mrabaha kununua mashine ya usingizi ya Kituo cha Afya Genkuru,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye. ‎Kegoye anaongeza kuwa wametumia sehemu ya fedha hiyo pia kununua (microscope) ya kupima wagonjwa na kwenye ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi katika kituo hicho cha afya.

‎‎Lakini pia, alisema wanakarabati nyumba ya mwalimu katika Shule ya Sekondari Bwirege, nyumba saba za walimu katika Shule ya Msingi Genkuru na ujenzi wa jengo la utawala wa shule ya msingi mpya ya Kerondo. “Miradi mingine inayotekelezwa ni ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya msingi mpya ya Kuruya na ununuzi wa viti 350 na meza zake kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Bwirege,” aliongeza Kegoye


Alitaja mradi mwingine uliyo kwenye mpango wa kutekelezwa kutokana na fedha za mrabaha kuwa ni ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Rewandwi. “Tunajenga pia vyumba vinne vya madarasa na kuchimba matundu sita ya vyoo katika shule hiyo ya Rewandwi,” aliongeza Mwenyekiti Kegoye.

‎Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kewanja, Joshua Chacha - maarufu kwa jina la Chia, alisema: “Sisi tumeelekeza fedha za mrabaha kwenye ujenzi wa nyumba pacha (two in one) ya walimu katika Shule ya Msingi Kewanja.”

‎“Vilevile, tunajenga nyumba pacha ya watumishi katika zahanati ya kijiji chetu,” aliongeza Chia na kubainisha kuwa miradi yote hiyo ilitengewa  Tsh  milioni 280 zilizotokana na gawio la mrabaha.

‎Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga, Emmanuel Wankaba, alitaja miradi inayotekelezwa katika kijiji hicho kutokana na fedha za mrabaha kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba saba vya madarasa ya shule ya msingi mpya ya Maika. “Sambamba na vyumba hivyo vya madarasa, tunajenga jengo la utawala na nyumba ya kuishi familia mbili za  walimu na tunakarabati nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamwaga,” aliongeza Wankaba.

‎Alitaja miradi mingine iliyo kwenye mpango wa kutekelezwa kijijini hapo kuwa ni ukarabati na uzibuaji wa barabara mbili zenye urefu wa kilomita zaidi ya 10 na uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Nyamwaga. Viongozi hao wa vijiji walisema utekelezaji wa miradi mingi uko katika hatua za mwisho kukamilika na kwamba wananchi wameipokea kwa furaha - wakitarajia kuona maboresho ya huduma za kijamii na kuchochea maendeleo katika maeneo yao.

This is the most recent post.
Older Post

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.