Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema pamoja na kutoa
maazimio manane kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya
Tegeta Escrow, Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha
na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo
zinahusika.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.PICHA|MAKTABA |
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake
Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alitaja mambo manne aliyoyatilia shaka
katika uamuzi huo wa Bunge, akisema yalilenga kulindana.
Mambo hayo ni msingi wa hukumu kwa watuhumiwa,
wahusika wengine kutotajwa, mwingiliano wa mamlaka ya mihimili ya dola
na wizara hizo kuachwa.
“Naona kama kulikuwa na namna fulani hivi ya
kulindana. Uamuzi wa Bunge ulifikiwa kutokana na msukumo wa wananchi wa
kutaka kujua hatima ya suala la escrow na IPTL, wahisani kusitisha
msaada kwa sababu ya uchotwaji huo wa fedha pamoja na siasa, hasa
zinazolenga urais mwaka 2015.”
Jaji Warioba alisema katika ripoti ya CAG na PAC,
wametaja ukiukwaji wa malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gain)
na ushuru wa stempu (stamp duty) na kuwa wanaohusika katika hilo ni
Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na upande mwingine
ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ambao uko chini ya
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Alisema wanaotakiwa kuidhinisha ulipwaji wa kodi
ni TRA, huku akihoji kitendo cha ripoti hizo mbili kuonyesha hisa
zimeuzwa kwa Sh6 milioni wakati ilikuwa ni Dola 6 milioni, nyingine
kuuzwa kwa Dola 300,000 za Marekani wakati ilikuwa Sh20 milioni.
“Hapa kuna ufisadi, maana hata kampuni iliyotajwa
kuwa imesajiliwa Brela inaonyesha katika ripoti kuwa wahusika
walioisajili hawakuweka majina yao, waliweka saini tu,” alisema.
Alisema uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya
Nishati na Madini lakini hasara iliyotajwa kuonekana inazihusu zaidi
Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda.
“Kulikuwa na mchezo wa siasa, kwamba baadhi
walindwe na wengine waachwe. Taarifa ya kamati imesema Kampuni ya PAP
kwa kushirikiana na ofisa wa ngazi za chini wa TRA walidanganya. Hivi
suala la kudanganya linafanywa na maofisa wa chini tu, kwani wa juu
hawahusiki?”
Alisema kama ilivyokuwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kutakiwa kujiuzulu kwa maelezo kuwa alikuwa akifahamu mlolongo wa
wizi huo, hata Hazina ilitakiwa kubanwa kwa sababu nayo ilikuwa
ikifahamu suala hilo... “Tumeambiwa kuna uchunguzi unafanyika. Jambo
hili bado halijafikia mwisho, iweje wengine waachwe wakati imeonekana
wazi kuwa Serikali imepata hasara?”
Waliopata mgawo
Jaji Warioba alisema suala jingine lililokosa
majibu ni kitendo cha watu wanaodaiwa kupewa fedha na James Rugemalira
kutajwa majina yao sambamba na akaunti ya aliyewapa, lakini wale
waliodaiwa kuchota fedha hizo katika magunia hawakutajwa.
“Taarifa inasema waliolipwa fedha kupitia Benki ya Stanbic
walichukua fedha kwenye magunia na mfuko, sasa mbona hawajatajwa? Hata
ukichukua fedha katika gunia lazima benki itabaki na kumbukumbu ya jina
la aliyechukua. Tusubiri uchunguzi zaidi, ila naona kama ni dalili za
kulindana.
Msingi wa uamuzi
“Ili Bunge lipate msingi wa kufanya uamuzi huo
walisema fedha za escrow ni za umma na wananchi wanaelewa fedha hizo ni
za umma. Binafsi nadhani katika hili Bunge halikutenda haki,” alisema.
Alisema Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa kwa
sababu ya mvutano kati ya Tanesco na IPTL ili kuweka fedha mpaka hapo
mzozo huo utakapomalizika... “IPTL imeendelea kutoa huduma na umma
umepata umeme kutoka katika kampuni hiyo na kulikuwa na malipo. Sasa
kuja kumaliza tatizo lazima fedha za escrow ndiyo zingetumika kulipia
gharama zote katika kipindi kile ambacho walikuwa hawajakubaliana.
“Kwa maana hiyo huwezi kusema fedha hizo ni za
umma. Zilikuwa ni za kumlipa anayetoa huduma ambaye ni IPTL, sasa kwa
kuwa hawakukubaliana juu ya gharama, waliamua fedha zibaki mpaka
tutakapokubaliana.
“Kama fedha hizo zingekuwa za umma zingewekwa
katika akaunti ya escrow kwa misingi ipi? Tusubiri uchunguzi zaidi ili
tujue za umma zilikuwa kiasi gani na za watu binafsi zilikuwa kiasi
gani.”
Alisema kama kulikuwa na fedha za Serikali ni kodi ambayo haikuwekwa wazi.
“Hii ambayo wameeleza kwamba Serikali imepoteza
Sh8 bilioni, ni kodi inayotokana na mauzo ya hisa, siyo gharama za
uwekezaji. Ukiuza hisa lazima ulipe kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru
wa stempu.
Hiyo ndiyo hasara wanayoisema na haihusiani na escrow kwa sababu hata kama escrow isingekuwa na matatizo, ilikuwa lazima walipe na ni utaratibu wa kawaida,” alisema.
Hiyo ndiyo hasara wanayoisema na haihusiani na escrow kwa sababu hata kama escrow isingekuwa na matatizo, ilikuwa lazima walipe na ni utaratibu wa kawaida,” alisema.
Post a Comment