Utagharimu takribani  shilingi Bilioni 4.8 za kitanzania

Na Mwandishi Wetu, Kahama Shinyanga

Mgodi wa  Barrick Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa  umefadhili mradi wa ujenzi wa chujio la maji ya mvua eneo la mwendakulima  wilayani Kahama mkoani Shinyanga unaoghalimu takribani shilingi Bilioni 4.8  kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa mji wa kahama maji safi na salama.

Akiongea wakati wa hafla ya kupokea mwenge ulioambatana na kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo wa mradi wa maji, Meneja wa Ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi ,Zonnastraal Mumbi alisema  mgodi katika hatua zake za mwisho za ufungaji umeamua kufadhili mradi huo ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji kwenye Wilaya ya Kahama.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa , Ismail Ali Ussi (Mbele mwanzo kushoto) akikata utepe na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chujio wa maji ya mvua , mradi unaofadhiliwa na Barrick Buzwagi na serikali ya Tanzania eneo la mwendakulima Wilaya ya Kahama katika upokeaji wa mbio za mwenge leo mchana mjini Kahama , mwanzo kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda.

“haya ni matokeo ya ufungaji wa mgodi wa Buzwagi kwa kuamua kufadhili mradi mkubwa kabisa wa maji ya mvua kwa kutengeneza miundombinu ya uvunaji , ukusanyaji na usambazaji wa maji ya mvua kwa ajili ya matumizi wa wananchi wa mji ya Kahama,” alisema Mumbi.

Kiongozi wa Mbio wa Mwenge , Ismail Ali Ussi akihutubia hadhara na wageni waalikwa kwenye uzinduzi wa uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji ya mvua eneo la mwendakulima.

Aliongeza kwamba moja ya dhamira ya kampuni ya Barrick inayoendeha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals ni kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

Sehemu ya jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa chujio wa maji ya mvua mjini kahama , shinyanga.

“Mgodi wa Buzwagi umefadhili mradi huu wa maji ya mvua kwa 62% kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu ya kisasa na bora inajengwa kwenye mradi huu kama sehemu za kuleta matokeo Chanya kwa wananchi wa mji wa kahama,” alisisitiza

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na  Usimamizi wa Mazingira, , Mamlaka ya Maji Safi  wa Mazingira Kahama (KUWASA)Mhandisi , Magige Marwa , alitoa pongezi kwa kampuni ya Barrick nchini  kwa kufadhili mradi huo mkubwa ambao ukikamilika utaondoa changamoto ya upatikanaji maji safi na salama wilayani Kahama,


Aliongeza kwamba mradi wa ujenzi wa chujio la maji mwendakulima unatazamiwa kuhudumia zaidi ya 66% ya wakazi waishio manispaa ya Kahama na una uwezo wa kuzalisha lita milioni 10 kwa siku.

“Mradi huu unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu na mpaka sasa 78% ya mradi mzima umeshakamilika kutokana na kasi ya ujenzi wa mradi huu mkubwa kwenye mji huu wa kahama,” alisisitiza

Mhandisi Marwa alifafanua kwamba mradi huo wa chujio la maji ya mvua 62% imefadhiliwa na mgodi wa Barrick- Buzwagi na 38% ni KUWASA kupitia Wizara ya Maji na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Meneja wa Ufungaji wa Mgodi wa Buzwagi , Zonnastraal Mumbi wa pili kulia kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.

Kwa upande wake , kiongozi wa mbio za mwenge , Ismail Ali Ussi alisema wizara ya maji inaendelea kufanya vizuri na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kupeleka huduma ya maji mijini na vijijini.

 

Kiongozi wa mbio za mwenge, Ismail Ali Ussi (Katikati) akisikiliza maelezo ya mradi kutoka kwa msimamizi wa mradi huo ,  Mhandisi , Magige Marwa (wa kwanza kulia) ambaye ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na  Usimamizi wa Mazingira, , Mamlaka ya Maji Safi  wa Mazingira Kahama (KUWASA) wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama , Frank Nkinda. 

“Nachukua fursa hii kuwapongeza wataalamu wote wa wizara na mamlaka za maji hapa kahama kwa kufanya kazi usiku na mchana katika kuhakikisha watanzania wanapata maji safi na salama,” amesema.

Sehemu ya ujenzi wa mradi wa maji ya mvua mwendakulima , Kahama shinyanga ndani ya mgodi wa Buzwagi Barrick.

Kwa upande wake , Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda alisisitiza kwamba umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea na ari hiyo ya kutekeleza miradi ya huduma za wananchi kwa viwango vya juu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Mwisho