MUUNGANO wa makampuni kadhaa kutoka nchini Oman, umetangaza uwekezaji wa kihistoria kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Muungano
huo, umekusudia kutoa Sh bilioni 160 kwa ajili ya mambo mbalimbali,
yakiwamo ya kununua ndege mpya na za kisasa na ujenzi wa kituo cha
mafunzo.
Hatua hiyo,
imekuja baada ya ziara iliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, nchini Oman
Oktoba mwaka jana, ambapo alitoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza
katika sekta za maendeleo nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana Mwenyekiti wa Kampuni
ya Al Hayat Development, Sheikh Salim Al Harthy, alisema hatua ya
uwekezaji huo, utasaidia kufungua milango kwa nchi na Watanzania kwa
ujumla.
Alisema
makubaliano hayo, yamefikiwa na Mtukufu Sultan Qaboos Bin Said Sultan wa
Oman. Alisema katika sehemu ya kwanza ya kujitolea kwa nchi hiyo,
itaingia makubaliano ya kusaini mkataba maalum kuisaidia ATCL, kwa
kuwekeza Dola za Marekani milioni 100 na kuongeza ndege za makampuni
mengine. Alisema uwekezaji huo, utakwenda sambamba na ununuzi wa ndege
ambazo zitatumika katika safari za ndani na nje ya Afrika.
“Kutokana
na ziara ya Rais Jakaya Kikwete katika nchi ya Oman, Oktoba mwaka
jana, alifanikiwa kufanya mazungumzo kwa kirefu na Mtukufu Sultan
Qaboos Bin Said Sultan, na kukubaliana uamuzi wa kuwekeza nchini.
“Kabla
ya makubaliano haya, yalifanyika makongamano mengi nchini Oman, ambayo
yalishirikisha makampuni mbalimbali, sasa yameamua kuutumia muungano
wao na kufanya uwekezaji mkubwa kwa nchi yetu.
“Uwekezaji
huu mkubwa kwa ATCL, utafungua njia za kibiashara kwa kuwa na ndege za
kisasa, ambazo zitafanya biashara ya kubeba abiria ndani ya nje ya
nchi.
“Tunamshukuru
Mtukufu Sultan Qaboos Bin Said wa Oman na Rais Kikwete, kutupatia
nafasi hii, hasa ukizingatia kipindi hiki tuna mpango wa kujenga kituo
cha mafunzo ya masuala ya ndege kwa ATCL.
“Mbali
na hili, tutajenga ofisi ya kisasa ambayo itakuwa kwa ajili ya
matumuzi ya shirika hili la ndege ya Tanzania, pamoja na kufanya
shughuli nyingine za maendeleo tunazotarajia kuanza ndani ya miezi sita
hadi kumi kutoka sasa,” alisema.
Sheikh Salim Al Harthy, alisema uwekezaji huo, ni matokeo mazuri ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Serikali ya Oman.
Mwaka
jana, Rais Kikwete alipotembelea Oman, baada ya kualikwa na Mtukufu
Sultan Qaboos Bin Said, ambapo aliambatana na ujumbe wa mawaziri na
viongozi waandamizi wa biashara. Katika ziara hiyo, Rais Kikwete
alibadilishana uzoefu wa uhusiano na kuangalia namna ya kudumisha
ushirikiano wa nchi hizo, kuhusiana na biashara, elimu na utamaduni.
Ziara ya Rais Kikwete katika nchi ya Oman ni ya pili kufanyika, baada
ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutembelea nchi hiyo,
mwaka 1985.
Post a Comment