HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P.  PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 19 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 01 APRILI, 2015

I: UTANGULIZI  

Masuala ya jumla
Mheshimiwa Spika,
  1. Leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa za Mkutano wa 19 wa Bunge lako Tukufu.  Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.

Mheshimiwa Spika,
  1. Tarehe 17 Machi, 2015 wakati tunaanza Mkutano huu, ulitoa taarifa ya kusikitisha ya kumpoteza Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Hayati Kapteni John Damian Komba, Mbunge wa Mbinga Mashariki aliyefariki tarehe 28 Februari, 2015 na kuzikwa nyumbani kwake Lituhi tarehe 03 Machi, 2015.  Napenda nitumie fursa hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wote kutoa pole kwako, Wananchi wa Mbinga Mashariki na kwa Watanzania wote kwa kuondokewa na ndugu yetu mpendwa Hayati John Damian Komba.  Kwetu sisi tulioko ndani ya Bunge lako Tukufu hakuna asiyejua sifa za Mheshimiwa Hayati Kapteni John Komba.  Sote tutaendelea kumkumbuka kwa yale yote aliyoyafanya kwa faida na maendeleo ya Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
  1. Vilevile katika kipindi hiki tangu Mkutano wa mwisho kulitokea majanga na ajali mbaya za Barabarani ambazo watu wengi wamepoteza maisha.  Nitumie nafasi hii ya awali kabisa kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki ambao wote wameguswa na misiba hiyo.  Tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu roho za Marehemu zilale mahala pema peponi. Kwa wale waliopata majeraha, tunawaombea wapone haraka.

Mheshimiwa Spika,
  1. Nitumie pia fursa hii ya mwanzo kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Grace Khwaya Puja na Mheshimiwa Innocent Rwabushaija Sebba kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Uteuzi wao unaonesha imani kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais katika utendaji wao.  Pamoja na kuwakaribisha Bungeni, tunawaahidi ushirikiano wetu katika kutekeleza majukumu yao.

b) Maswali

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na jumla 156 ya msingi na 425 ya nyongeza na kujibiwa na Serikali.  

(c) Miswada
Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Mkutano huu, jumla ya Miswada 21 ilipangwa kujadiliwa katika Mkutano wa 19.  Miswada iliyowasilishwa na kupitishwa katika hatua zote ni 14 ambayo ni kama ifuatavyo:

  1. Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Ajira za Wageni wa mwaka 2014 (The Non-Citizens Employement Regulation Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Silaha wa Mwaka 2014 (The Firearms and Ammunition Control Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji wa Mwaka 2014 [The Immigration (Amendment) Bill, 2014];

  1. Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 (The Tax Aministration Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Takwimu wa Mwaka 2014 (The Statistics Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa wa Mwaka 2014 [The Disaster Management Bill, 2014];

  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Stakabadhi Ghalani wa Mwaka 2014 [The Wharehouse Receipts (Amendment) Bill, 2014];

  1. Muswada wa Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Mwaka 2015 (The National Payment Systems Bill, 2015);

  1. Muswada wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya wa Mwaka 2014 [The Drug Control and Enforcement Bill, 2014];

  1. Muswada wa Sheria ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI wa Mwaka 2014 [The Tanzania Commision for AIDS (Amendment) Bill, 2014];

  1. Muswada wa Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2014 (The Budget Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania wa Mwaka 2015 [The Youth Council of Tanzania Bill, 2015];

  1. Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa Mwaka 2014 (The Electronic Transaction Bill, 2015); na

  1. Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa Mwaka 2015 (The Computer and Cyber Crimes Bill, 2015).

Mheshimiwa Spika,
  1. Miswada iliyoachwa kwa sababu mbalimbali ni:

  1. Muswada wa Sheria ya Wataalam wa Kemia wa Mwaka 2014 (The Chemist Professionals Bill, 2014);

  1. Muswada wa Sheria ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2014 (The Government Chemistry Laboratory Bill, 2014); na

  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2014 [The Written Laws (Miscellaneous Amendements) (No. 2) Bill 2014].

Mheshimiwa Spika,
  1. Miswada ifuatavyo ilisomwa kwa mara ya Kwanza.

  1. Muswada wa Sheria ya kupata Habari wa Mwaka 2015 (The Access to Information Bill, 2015);

  1. Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015 (The Media Services Bill, 2015);

  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani wa Mwaka 2015 [The Fair Competition (Amendment) Bill, 2015]; na

  1. Muswada wa Sheria ya Tume ya Walimu wa Mwaka 2015 [The Teachers Servce Commission Bill, 2015].

d) Maazimio

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili na kuridhia Maazimio mawili yafuatavyo:

  1. Azimio la kuridhia Mkataba wa Msingi na Kanuni za Utumishi wa Umma na Utawala Barani Afrika Mwaka 2011 (The African Charter and Principal of Public Service and Administration, 2011); na

  1. Azimio la Kuridhia Makubaliano ya Msingi ya Ushirikiano katika Bonde la Mto Nile (Agreement on the Nile River Basin Co-operative Framework – CFA);

  1. Napenda kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kujadili miswada mingi kiasi hiki na kuipitisha pamoja na kuridhia maazimio yote yaliyowasilishwa.

II: MAAFA YALIYOJITOKEZA

  1. Dhoruba ya Mtwara
Mheshimiwa Spika,
  1. Usiku wa kuamkia tarehe 14 Januari 2015 kulitokea mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika eneo la Mnazi Bay, Mtwara; hali ambayo ilisababisha eneo la Nchi kavu takribani mita 105 upana na mita 1,100 urefu kumeguka na kuwa sehemu ya maji ya bahari. Eneo hili limejengwa miundombinu ya gesi asilia kama ifuatavyo:-
  1. Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom Tanzania (M&P) kinachozalisha gesi ambayo inatumika kuzalishia umeme kwenye mitambo ya TANESCO iliyopo Mtwara Mjini. Umeme unaozalishwa unatumika kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi; na
  1. Bomba la gesi la inchi 16 litakalopeleka gesi asilia isiyosafishwa (raw gas) kutoka visima vilivyopo Mnazi Bay kwenda kiwanda kipya cha Serikali cha kuchakata gesi asilia kinachojengwa Kijiji cha Madimba.
Mheshimiwa Spika,

  1. Hali hii ilihatarisha zaidi kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Maurel & Prom Tanzania (M&P) na kwa kiasi kikubwa bomba la gesi asilia kama ilivyoelezwa hapo awali. Kiasi kikubwa cha eneo la Nchi kavu kilimezwa na bahari na kuacha mita 6 tu kulifikia bomba la gesi asilia linalopeleka gesi kiwanda cha Madimba na mita 29 kukifikia kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha M&P.

  1. Kufuatia hali hii, kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa (KUU) ambacho pia kiliwashirikisha Wataalam wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, JWTZ, TPDC, TANESCO na Kamishna wa Madini wa Kanda kilifanyika tarehe 16 Januari, 2015 kujadili namna ya kukabiliana na tatizo lililojitokeza la mmomonyoko mkubwa wa udongo uliotokea katika eneo la Mnazibay.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kikao cha Kamati ya Ulinzi kiliazimia kazi ya kuzuia mmomonyoko ianze kufanyika mara moja alfajiri ya tarehe 17 Januari 2015 kwa kutumia Majeshi yote yaliyopo Mkoani kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa. Aidha, Kampuni ya Dangote, TPDC, walishirikiana na majeshi yetu ya JWTZ, Magereza, Jeshi la Polisi walianza kuimarisha kingo kwa kutumia viroba vilivyojazwa mchanga, mawe na vifusi vya zege.

Mheshimiwa Spika,
  1. Nachukua fursa hii kuwapongeza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa jitihada mlizofanya za kusimamia zoezi zima la kuzuia mmonyoko wa ardhi katika kingo za bahari, eneo la Mnazi Bay. Nitakuwa sijatenda haki kama nisipowataja wote walioshiriki katika shughuli hii ya dharura. Makundi ambayo yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana kukabiliana na janga hilo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Wengine ni Kampuni ya Dangote, Kampuni ya Maurel & Prom Tanzania, Kampuni ya Shideshi Co. Ltd, Shirika la Petroli Tanzania (TPDC), Wizara ya Nishati na Madini na Wataalam kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Aidha, Wakala wa barabara (TANROAD) Mtwara kwa kushirikiana na Mkandarasi “BQ Contractors” walitoa vifaa vya uchimbaji wa mawe na kupakia kwenye magari.

Mheshimiwa Spika,
  1.    Tayari Wizara ya Nishati imepeleka Wataalam kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizopatikana na jinsi ya kutunza eneo hilo.  Jeshi letu kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wanaendelea kuimarisha kingo za bahari ili zisilete athari kwa Kiwanda na Bomba la Gesi Asilia.

  1. Kazi nzuri iliyofanyika imewezesha kudhibiti kasi ya maji kuendelea kumega sehemu ya ardhi iliyobaki. Hali halisi iliyopo sasa baada ya jitihada zilizofanywa kukabiliana na janga hilo, ni kwamba Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay kinachoendeshwa na Kampuni ya Maurel & Prom, kinaendelea kuzalisha gesi na Mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kupata umeme.

  1. Mafuriko
  1. Wilaya ya Kahama – Mkoa wa Shinyanga

Mheshimiwa Spika,
  1. Usiku wa kuamkia tarehe 4 Machi, 2015 mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha katika Vijiji vitatu vya Mwakata, Nhumbi na Maguhung’hwa vya Kata ya Mwakata, Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.  Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zinaonesha kuwa mvua hiyo ilisababisha vifo 47, majeruhi 112 na nyumba 657 ziliathirika.  Ekari 2,393 za mazao ya chakula ziliharibika. Aidha, mifugo mingi ilikufa wakiwemo ng’ombe 35, mbuzi 240, kondoo 50, kuku 1,034 na bata 240.  Mifugo hii ilikufa kwa kupigwa na mawe makubwa ya barafu na kisha kuangukia kwenye maji ya baridi kali. Vifo hivyo, vya mifugo vimeleta athari kubwa hasa kwa kaya duni ambazo mifugo ilikuwa ni tegemeo kwa mahitaji muhimu ikiwemo ada za Shule na shughuli nyingi za kijamii.  Vilevile, kulitokea uharibifu mkubwa wa miundombinu na huduma muhimu za kijamii, kama vile Shule kufungwa na kukosekana kwa maji safi na salama.  

Mheshimiwa Spika,
  1. Tarehe 5 Machi, 2015 niliweza kutembela baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mvua hizo ikiwa ni pamoja na kuwapa pole waliopoteza ndugu na vifaa mbalimbali kama nyumba na mifugo. Aidha, tarehe 12 Machi, 2015 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye alifanya ziara maalum ya kutembelea Vijiji vitatu katika Kata ya Mwakata, Wilayani Kahama, Shinyanga ili kuwapa pole na kuwafariji Wananchi walioathirika na mvua kubwa iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali na mawe.  Tayari Serikali imechukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba waathirika wote wanapatiwa msaada wa haraka ikiwemo vyakula, mahema, mablanketi na dawa za kuwasaidia. Aidha, wakati nikiwa Shinyanga niliwaomba Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa hali ya kawaida inarejeshwa katika maeneo yote yaliyoathirika.

  1. Wilaya ya Ilala – Mkoa wa Dar es Salaam

Mheshimiwa Spika,

  1. Wakati huo huo mvua kubwa zilizonyesha katika Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia tarehe 20 Machi, 2015 nazo zimesababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu katika sehemu za Jiji la Dar es Salaam.  Kutokana na mvua hizo Watu 7 walipoteza maisha na wengi kukosa makazi baada ya nyumba zaidi ya 200 eneo la Buguruni kwa Mnyamani kuzingirwa na maji. Serikali itahakikisha inachukua hatua za kujenga mtaro wa kutoa maji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika,

  1. Jitihada za kukabiliana na maafa hayo zimekuwa na mafanikio makubwa.  Kwa vile majanga haya ni makubwa, ni dhahiri kwamba Serikali peke yake isingeweza kubeba jukumu la kuwasaidia wote walioathirika na mvua hiyo Watu binafsi, Wafanyabiashara, Mashirika ya Umma na Yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Dini na Viongozi mbalimbali wameitikia wito wa kushirikiana na Serikali kusaidia ndugu na jamaa walioathirika na maafa hayo.  Napenda nitumie fursa hii kuwashukuru wote waliojitolea kwa hali na mali na moyo msaada ambao ulihitajika sana katika kipindi hiki kigumu. Wito wangu kwa Wananchi wote ni kuwaomba tena kuendelea kushirikiana kama ishara ya mshikamano kila wakati maafa yanapotokea.

  1. Ajali za Barabarani

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia ajali za barabarani zikiendelea kupoteza maisha ya wananchi sambamba na kuwafanya wengi kujeruhiwa na wengine kupata ulemavu wa kudumu.  Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014 kulikuwa na jumla ya matukio 15,420 ya ajali za barabarani ambayo kati ya matukio hayo, ajali 3,106 zilisababisha vifo 3,857. Aidha, ajali hizo zilisababisha majeruhi 15,230.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Februari, 2015 kulikuwa na jumla ya ajali 1,464 zilizosababisha vifo 509 na majeruhi 1,602. Moja ya ajali za kutisha za hivi karibuni ni ile iliyotokea tarehe 11 Machi, 2015 katika mlima wa Changalawe, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa ambapo Basi la Kampuni ya Majinja Special toka Mbeya kuelekea Dar es Salaam liligongana uso kwa uso na gari kubwa na kusababisha vifo vya watu 50 kati yao Wanawake 13 na Wanaume 37. Katika ajali hiyo, watu 21 walijeruhiwa.

Mheshimiwa Spika,
  1. Mnamo tarehe 17 Machi, 2015 ajali nyingine ilitokea katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo magari matatu yaligongana na kusababisha vifo vya watu wawili (2) na majeruhi wanne (4). Siku mbili baadaye tarehe 19 Machi, 2015 katika eneo hilohilo la Hifadhi Mikumi Morogoro Mini Bus ya Kampuni ya Msanga, iligongana uso kwa uso na Basi la Kampuni ya Luwinzo na kusababisha vifo vya watu 7 na majeruhi 17.

Mheshimiwa Spika,
  1. Wakati huo huo, tarehe 23 Machi 2015 ajali nyingine ilitokea eneo la Majimazuri  Mbeya ambapo Watu 8 walipoteza maisha na wengine  6 kujeruhiwa.  Aidha, ajali nyingine ni ile iliyotokea tarehe 25 Machi 2015, iliyohusisha Basi la Kampuni ya Super Shem liligongana uso kwa uso na gari la Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na kusababisha vifo vya Watu 6 na wengine 9 kujeruhiwa.  Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Mwanza – Dar es Salaam eneo la Kijiji cha Undomo, Kata ya Uchama, Wilayani Nzega Mkoani Tabora.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa maana hiyo, kati ya Januari na Machi, 2015 jumla ya Watu 73 walipoteza maisha na wengine 57 Walijeruhiwa.  Sababu kuu ya kutokea kwa ajali hizo inatajwa kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa madereva. Ni dhahiri kwamba, Matukio haya ya ajali hayavumiliki na hayazoeleki. Aidha, hii ni idadi kubwa ya ajali na vifo vilivyotokea katika kipindi cha muda mfupi.

  1. Nitumie fursa kuziagiza Wizara ya Mambo Ndani ya Nchi, Wizara ya Uchukuzi Wizara ya Fedha Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi za Usafiri kama SUMATRA katika kipindi cha Mwezi mmoja  kutoa  mapendekezo  kuhusu  hatua  za dharura za namna ya kukabiliana na ajali hizi.  Vilevile, pale itakapobidi, Wataalam waangalie uzoefu wa Nchi nyingine kujua hatua walizotumia katika kukabiliana na ajali.  

  1. Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka zinazohusika na Uchukuzi na Usafirishaji zitaendelea kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na ajali hizo ikiwemo kuyafungia Makampuni ya Usafirishaji yaliyokithiri katika matukio ya ajali. Pia, Madereva Wazembe wataendelea kuadhibiwa kwa Mujibu wa Sheria na ikibidi kufutiwa Leseni zao za Udereva. Nirudie kuagiza Jeshi letu la Polisi kuongeza juhudi katika kuzuia ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya Watu wengi na kusababisha ulemavu na upotevu wa mali.

III. KILIMO

Hali ya Chakula
Mheshimiwa Spika,
  1. Hali ya chakula hapa Nchini kwa mwaka 2014/15 imeendelea kuwa imara kutokana na mavuno mazuri na ya ziada yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2013/14. Tathmini ya uzalishaji iliyofanyika mwaka jana, ilibainisha Nchi kuwa na ziada ya chakula kwa viwango vya utoshelevu vya Asilimia 125. Mikoa 23 kati ya 25 ya Tanzania Bara ilibainika kuwa na viwango vya ama ziada au utoshelevu.  Katika kipindi hicho ni mikoa miwili tu iliyodhihirika kuwa na uhaba wa chakula na maeneo tete katika Halmashauri 41.

  1.  Mwenendo wa Bei

Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa ujumla hali ya chakula na upatikanaji wa vyakula sokoni unaridhisha katika Mikoa yote kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo 2013/2014. Bei ya mazao ya chakula imekuwa ikishuka au kupanda katika eneo moja na jingine. Kwa mfano, bei ya wastani ya mahindi Kitaifa imeshuka kutoka Shilingi 41,313 mwezi Agosti, 2014 hadi Shilingi 37,355 mwishoni mwa mwezi Februari, 2015 kwa gunia la kilo 100.  

  1. Aidha, katika kipindi hicho, bei ya mchele imepanda kutoka Shilingi 116,960 hadi Shilingi 150,563; na maharage kutoka Shilingi  139,452  hadi  Shilingi 149,777 kwa gunia la kilo 100. Bei hizo ziko chini kuliko ilivyokuwa kwa kipindi kama hicho mwaka jana na kwa wastani wa miaka mitano iliyopita. Hata hivyo, hadi mwishoni mwa mwezi Februari 2015, bei ya mahindi katika baadhi ya masoko ya Miji Mikuu hapa Nchini ilikuwa juu ikilinganishwa na wastani ya Shilingi 37,355 kwa gunia la kilo 100. Masoko hayo ni pamoja na Lindi (Shilingi 57,917), Musoma (Shilingi 49,375), Kigoma (Shilingi 41,625) na Tanga (Shilingi 37,375).

  1. Mwenendo wa mvua za vuli na upatikanaji wa chakula

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika msimu wa 2014/2015, maeneo yanayopata mvua za vuli hasa maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Tanga) yalipata mvua za wastani zilizoanza Mwezi Septemba, 2014; na maeneo machache ya Kanda ya Ziwa (Kagera na Mwanza) zilipata pia mvua za wastani. Hali hiyo, imefanya uzalishaji katika maeneo hayo kutoridhisha hali inayoashiria kupungua kwa mchango wa mvua za vuli (ambao ni takriban asilimia 27) ya chakula msimu huu.

  1. Hali ya mazao mashambani

Mheshimiwa Spika,

  1. Tathmini iliyofanyika tarehe 3 Machi, 2015, inaonesha kuwa mvua za msimu zilianza vibaya katika Mikoa 11 ya Dar es Salaam, Mara, Morogoro, Pwani, Shinyanga, Tanga, Lindi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Tabora; na kwamba mtawanyiko wa mvua hizi uliendelea vibaya katika Mikoa tisa (9) ya Arusha, Dar es Salaam, Pwani, Shinyanga, Simiyu, Tanga, Manyara, Singida; na Tabora. Kutokana na hali hii, inatarajiwa kuwa mavuno ya msimu wa 2014/2015 yatakuwa chini ya kiwango hivyo kusababisha kuwepo kwa uhaba wa chakula katika Mikoa sita (6) ya Arusha, Kilimanjaro, Mara, Pwani, Shinyanga na Tabora.

Mheshimiwa Spika,
  1. Tathmini hii imeonesha pia kuwa utekelezaji wa malengo ya uzalishaji katika msimu wa 2014/2015 haujafikiwa katika Mikoa 18. Kwa Mikoa inayopata mvua mbili za vuli na masika (Bimodal rain), nimeeleza kuwa kilimo cha vuli kilishapita bila mchango mkubwa wa chakula; na kwa vile mvua za masika zitategemewa kunyesha kwa mtawanyiko wa wastani na kwa kipindi kifupi, ni wazi kuwa uzalishaji utakuwa pungufu ikilinganishwa na uzalishaji wa mwaka 2013/2014 na hivyo kufanya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa chini ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa chakula katika msimu wa 2015/2016 katika Nchi yetu, napenda kuchukua fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa iliyopata mvua hafifu; na ile yenye akiba kubwa ya chakula wasimamie kwa karibu shughuli za hifadhi ya mavuno yaliyopatikana katika msimu wa 2013/2014 kwa kuzishirikisha Halmashauri zote na wananchi. Vile vile, kwa Mikoa yenye mvua chache wachukue hatua madhubuti na za haraka kwa kushirikiana na Halmashauri zote kuhakikisha kuwa wananchi wanapata mbegu bora za muda mfupi zinazostahimili ukame kama vile mtama, uwele, n.k. ili wapande mapema kwa kutumia mvua zinazonyesha sasa.

  1. Hifadhi ya Taifa ya Chakula

Mheshimiwa Spika,
  1. Hadi tarehe 11 Machi 2015 Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulikuwa umenunua Tani 304,514 za nafaka ziwemo Tani 295,900 za mahindi, Tani 4,674 za mtama; na Tani 3,940 za mpunga. Kutokana na NFRA kuwa na akiba ya Tani 188,987 za mahindi na Tani 506 za mtama wakati wa kuanza msimu wa ununuzi tarehe 01 Julai, 2014 hadi sasa  akiba iliyohifadhiwa katika Kanda mbalimbali za NFRA ni jumla ya Tani 494,007 ambapo Tani  484,887 ni za mahindi, Tani 5,180 ni za mtama; na Tani 3,940 ni za mpunga. Tunafahamu kuwa kuna maeneo kadhaa hapa Nchini yaliyopata mavuno hafifu kutokana na maeneo yao kukosa mvua ya kutosha. Hivyo, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu na wananchi kuwa Serikali ina akiba ya kutosha ya chakula kwa Wananchi wote watakaokuwa na matatizo ya njaa. Nichukue fursa hii kuitaka Mikoa na Halmashauri zenye upungufu wa chakula kufanya tathmini ya haraka kupata takwimu za wananchi wenye njaa ili wapatiwe chakula mapema bila kuchelewa.

f) Mwenendo wa Malipo ya NFRA
Mheshimiwa Spika,
  1. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulipanga kununua Tani 200,000 za nafaka kwa gharama ya Shilingi Bilioni 109.6. Hata hivyo kutokana Wananchi kuzalisha kwa wingi na kuiwezesha Nchi kuwa na ziada ya chakula hasa mahindi, mpunga na mtama kwa takriban Tani Milioni 3.2, Serikali iliongeza lengo la ununuzi wa nafaka hadi Tani 298,122. kwa thamani ya Shilingi Bilioni 151.3.  Serikali ilichukua hatua hiyo ili kuepuka kuharibika kwa mazao yaliyokuwa yameletwa na wakulima kuuzwa katika vituo vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Aidha, kutokana na fedha za Tani za ziada kutokuwepo katika Bajeti ya awali, Serikali ilishindwa kuwalipa kwa wakati wakulima wote waliopeleka nafaka katika vituo hivyo na kusababisha Serikali kuwa na madeni kwa wakulima hao.

Mheshimiwa Spika,
  1. Hadi tulipofika Januari 2015, deni lilikuwa limefikia Shilingi Bilioni 89.2 kwa Tani 175,606 za nafaka.  Kwa msingi huo hadi tarehe 24 Februari 2015, Serikali ilikuwa imetoa Shilingi Bilioni 15 na kukopa Shilingi Bilioni 15 kutoka Benki ya CRDB zilizolipa na  kupunguza madeni ya wakulima. Takwimu za sasa zinaonesha kuwa hadi tarehe 27 Machi, 2015 deni lilikuwa limepungua hadi kufikia Shilingi Bilioni 45 kwa Tani 88,910 za nafaka.  

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika kuendelea kupunguza malipo ya deni lililobaki, tarehe 31 Machi, 2015 Serikali imetoa Shilingi Bilioni 20 na kubakiza deni la Shilingi Bilioni 25. Aidha, Serikali imepanga kuuza sehemu ya akiba ya nafaka iliyopo katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kwa Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme) na Jeshi la Magereza ili kupata fedha zakulipia deni lote lililobaki. Napenda kutoa msisitizo kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kufanya malipo haya kuzingatie maagizo ya Serikali ya kutoa kipaumbele cha kufanya malipo kwa wakulima wadogo wadogo, mmoja mmoja kabla ya makundi mengine.
IV: UNUNUZI WA MADAWATI SHULE ZA MSINGI KWA KUTUMIA FEDHA YA FIDIA YA RADA

Mheshimiwa Spika,
  1. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokea fedha zilizotokana na fidia ya Rada (BAE System Plc Funds) kiasi cha Paundi za Uingereza 29,542,266, sawa na Shilingi 72,324,609,162.  Kulingana na Mkataba wa Makubaliano (MOU) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo - DFID, ilikubaliwa kuwa Paundi 24,392,266 sawa na Shilingi 59,716,513,062 zitumike katika ununuzi wa vitabu vya kiada, mihutasari na miongozo ya mihutasari kwa shule za msingi Tanzania Bara; Paundi 5,000,000 sawa na Shilingi 12,240,870,000 zitumike kununulia madawati kwa shule za msingi Tanzania Bara. Aidha, Paundi za Uingereza 150,000.00 sawa na Shilingi 367,226,100.00 zilipangiwa kazi ya ukaguzi na ufuatiliaji na udhibiti wa mchakato wa ununuzi.  

Mheshimiwa Spika,
  1. Kutokana na Mkataba wa Makubaliano hayo ilipangwa kuwa madawati yanunuliwe kwa ajili ya Halmashauri tisa (9) zenye upungufu mkubwa wa madawati na matokeo dhaifu katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi. Lengo lilikuwa ni kumaliza uhaba wa madawati katika Halmashauri hizo. Hata hivyo, Bunge katika kikao chake cha mwaka 2012/2013 ilishauri kwamba Halmashauri zote zipate mgao wa madawati kwa usawa. Hivyo, Mikoa yote ishirini na tano ya Tanzania Bara imepata na itaendelea kupata madawati kwa usawa.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kikao cha Kamati Tendaji ya matumizi ya fedha za BAE kiliamua kuwa yatengenezwe madawati ya kukaa mwanafunzi mmoja mmoja ili kukidhi na kurahisisha ufundishaji kwa kutumia njia shirikishi ambazo huwezesha wanafunzi kujadiliana zaidi na kuchangiana mawazo ya uelewa wao kuliko kumsikiliza mwalimu zaidi. Hivyo madawati yatengenezwe na kugawiwa kwa kuzingatia aina za madawati na umri wa Wanafunzi. Wataalamu wa Ufundi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU) wakishirikiana na Wataalamu wa Ufundi kutoka DFID walitoa viwango vya ulinganisho (technical specifications) vya madawati hayo.

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika kugawa madawati, Mikoa sita ya ukanda wa Pwani ilipangwa kupata madawati ya Plastiki Ngumu (Hard Plastic Desks). Mikoa hiyo ni Dar es salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara na Morogoro. Mikoa kumi na tisa iliyobaki itapatiwa madawati ya mbao (Steel Framed Desk).

Mheshimiwa Spika,
  1. Awamu ya kwanza ya ununuzi wa madawati ilianza mwezi Oktoba 2013 na ilihusisha ununuzi wa aina mbili za madawati, madawati ya Plastiki Ngumu na madawati ya Mbao.

Mheshimiwa Spika,
  1. Jumla ya madawati 30,996 ya Plastiki Ngumu (Hard Plastic Desks) yamenunuliwa kwa ajili ya Mikoa sita ya Ukanda wa Pwani ambao una Halmashauri 41 ambapo kila Halmashauri imepata madawati 756 na usambazaji wake umekamilika na madawati yameanza kutumika. Aidha, jumla ya madawati 62,992 ya Mbao yamenunuliwa na usambazaji umekamilika ambapo kila Halmashauri kati ya 124 za Mikoa 19 isiyo ya Ukanda wa Pwani imepata madawati 508.

Mheshimiwa Spika,
  1. Awamu ya pili ya ununuzi wa madawati ilianza mwezi Juni 2014. Awamu hii imehusisha jumla ya madawati 74,897 ya Plastiki Ngumu na ya mbao. Kila Halmashauri ya Mikoa sita ya Ukanda wa Pwani imepata madawati 617 ya Plastiki Ngumu. Ilihali kila Halmashauri za Mikoa 19 isiyo ya Pwani itapata madawati 400 ya mbao. Inatarajiwa madawati haya ya mbao yatakamilika kusambazwa katika Halmashauri kati kati ya mwezi wa Nne 2015.

Mheshimiwa Spika,
  1. Madawati ambayo yameshasambazwa mpaka sasa ni 119,285 yakiwemo ya plastic ngumu 56,293. Madawati mengine ya mbao 49,600 yatakamilika kusambazwa kati kati ya mwezi April 2015. Mchakato huu wa ununuzi wa madawati ukikamilika bado tatizo la upungufu wa madawati litakuwa halijaisha. Kuna uhitaji wa madawati 3,302,678, na madawati yaliyopo shuleni ni 1,837,783 na kuna upungufu wa madawati 1,464,895. Baada ya kukamikisha usambazaji wa madawati 168,885 kwa kutumia fedha hizi za fidia ya rada kutakuwa na upungufu wa madawati 1,296,010. Hivyo, bado kuna ulazima wa kuendelea kutenga fedha zaidi katika kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia na kuendana na mahitaji ya Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN).
Mheshimiwa Spika,
  1. Nachukua fursa hii kuwashukuru sana wote walioshirikiana katika harakati hizi za kuondoa upungufu wa madawati Nchini.  Napenda kuwakumbusha Viongozi na Wananchi kuwa bado tunayo kazi kubwa.  Kila mmoja awe mbunifu katika eneo lake na kushirikiana  pamoja katika kuweka na kutekeleza mipango endelevu ya kuongeza idiadi ya madawati.  Halmashauri ziendelee kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya Madawati na nawaomba Wadau wa Maendeleo kuendelea kusaidia katika eneo hili. Ninaamini wote tukishirikiana kwa pamoja tutafanikiwa.

V: MAUAJI YA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI (ALBINO)

Mheshimiwa Spika,
  1. Hivi karibuni yameibuka tena mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino). Ninasema yameibuka tena kwa kuwa yalikuwa yamekoma hususani mwaka 2011 na tukaishi kwa amani kidogo. Hata hivyo, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia Taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari 2015 alilieleza Taifa kuwa mauaji hayo yameibuka tena. Mauaji haya kwa taarifa zilizopo yalianza mwaka 2006 ambao ulikuwa na tukio moja (1). Idadi ya matukio ya mauaji iliendelea kupanda hadi kufikia saba (7) mwaka 2007 na 18 mwaka 2008. Mwaka 2009 matukio yalianza kupungua kutokana na juhudi za Serikali na Wananchi. Mwaka huo ulikuwa na matukio Tisa (9), mwaka 2010 ulikuwa na tukio moja (1) na mwaka 2011 kama nilivyosema haukuwa na tukio. Hata hivyo, kwa miaka iliyofuata kulikuwa na tukio moja (1) mwaka 2012, tukio moja (1) mwaka 2013 na kufikia matukio manne (4) mwaka 2014. Mwaka huu wa 2015 limeshatokea tukio moja (1) na kufanya jumla ya matukio ya mauaji kuwa 43 hadi sasa (Mwaka 2006 – 2015). Matukio haya hayahusishi yale ya kujeruhi.

Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa upande wa Watuhumiwa takwimu za watuhumiwa kati ya mwaka 2006 -2015 zinaonesha kuwa:
  1. Jumla ya watuhumiwa 181 wakiwemo Wanaume 171 na Wanawake 10 walikamatwa na kuhojiwa. Kati yao watuhumiwa 133 walifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji  na 46 kwa makosa ya kujeruhi.

  1. Kesi 10 bado zinaendelea katika hatua mbalimbali za uchunguzi;

  1. Watuhumiwa 15 wamehukumiwa katika Mahakama, 13 kati yao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

  1. Watuhumiwa wawili waliuawa na Wananchi kabla ya kufikishwa Polisi.

  1. Mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kujeruhi;

Mheshimiwa Spika,
  1. Chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.  Aidha, Matukio 41 kati ya 43 yametokea katika Ukanda wa Ziwa na Magharibi, kwani hadi sasa yametokea matukio 13 ya Mauaji Mwanza, Kagera matukio sita (6), Tabora matukio matano (5), Mara matukio manne (4), Geita matukio manne (4), Kigoma matukio Manne (4) Simiyu matukio matatu (3) na Shinyanga matukio mawili (2).  Hali hii inayoonesha dalili kuwa imani hizi za kishirikina zimejikita zaidi katika eneo hili la Nchi. Wakati akihutubia Taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari 2015 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka wazi msimamo wa Serikali kwamba Serikali itafanya kila jitihada kukomesha mauaji haya. Aidha, Serikali haitaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Spika,
  1. Wito wangu ni kuomba ushirikiano wa Wananchi na Viongozi wa Dini zote, Mashirika ya Serikali na Yasiyo ya Serikali na Wadau wote wa Maendeleo katika vita hii. Aidha, niwaombe watu wote walio wazalendo na wenye kupenda amani katika Taifa letu la Tanzania kuendelea kulaani kwa nguvu zote vitendo hivi vya kikatili na visivyokubalika na kuendelea kutoa taarifa zozote zinazohusu vitendo hivi kwa vyombo vya Serikali ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo. Niwaombe tena Taasisi zote za Dini kusaidia katika kuondoa au kubadili imani hizi za kishirikina miongoni mwa jamii na Mahakama kusaidia katika kuharakisha kesi za mauaji ya Walemavu wa Ngozi na kutoa adhabu kali kwa watakaothibitika kushiriki katika vitendo hivyo. Vyombo vya Dola vitumie kila ujuzi na mbinu kutekeleza maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukomesha mauaji haya. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii tutashinda.

VI: KURA YA MAONI KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA UCHAGUZI MKUU

  1. Kuboresha Daftari la Wapiga Kura

Mheshimiwa Spika,
  1. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea katika Mkoa wa Njombe chini ya Usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.  Sambamba na Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura, Tume inaendelea pia na maandalizi ya utekelezaji wa Upigaji Kura ya Maoni na   Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Jukumu kuu la Tume kwa sasa ambalo limekwisha anza ni ukamilishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa haraka ili kuwezesha kufanyika kwa Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu. Uandikishaji unafanyika kwa kutumia vifaa maalum vinavyojulikana kama “Biometric Voters Registration (BVR)”. Vifaa hivi vina uwezo wa kumtambua mtu  na kumtofautisha na  mwingine  kama  vile  alama za  vidole,  sura, mpangilio  wa  mikono, saini ya  mtu  n.k. Hivyo vifaa hivi vinatumika katika Uandikishaji wa Daftari la kudumu ili kuwa na Daftari sahihi na linaloaminika zaidi.

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika kutekeleza uboreshaji wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imelenga kuandikisha Wapiga Kura milioni 21. Vituo vya Kuandikishwa vimesogezwa karibu na Wapiga Kura katika ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa; na inakadiriwa kutakuwa na Vituo 36,164. Kila Kituo kitaandikisha kwa siku 7 hadi 11 kufuatana na idadi ya watu na vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 hadi saa 12 jioni.

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika zoezi zima la kuboresha Daftari la Wapiga kura Tume inategemea kutumia BVR Kits 8,000 katika uboreshaji huu. Tayari BVR 250 zilitumika katika zoezi la majaribio kwa mafanikio makubwa. Uboreshaji wa awamu hii utahusisha Wapiga Kura wote, wapya na wa zamani na wale wote waliozaliwa kabla ya Septemba 1997. Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza Uandikishaji katika Mkoa wa Njombe tarehe 16 Machi, 2015 na unatarajiwa kukamilika tarehe 18 Aprili 2015 ambao ni takriban muda wa Mwezi mmoja.

  1. Tarehe 24 Februari, 2015 nilifanya uzinduzi Kitaifa wa Zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura katika Daftari la Wapiga Kura, hafla iliyofanyika Mjini Makambako katika Mkoa wa Njombe. Taarifa tulizopata ni kwamba uandikishaji huo umekuwa wa mafanikio makubwa; kwani watu wanajitokeza kwa wingi sana. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Tume ilipanga kuandikisha Wastani wa Wapiga Kura 1,850 kwa siku ya kwanza lakini walioandikishwa 3,014 ambao ni mara 2 ya waliotarajiwa.  

Mheshimiwa Spika,
  1. Serikali kwa upande wake imehakikisha fedha yote kwa ajili ya ununuzi wa BVR 8,000 zimelipwa kwenye Tume ya Uchaguzi ya Taifa.  Matarajio ni kwamba kazi ya kuandikisha katika Mikoa mingine itaanza na kuendelea kwa kasi.  Aidha, tunatarajia Tume itatoa taarifa ya Ratiba itakayotumika kutuwezesha kukamilisha zoezi la uandikishaji. Tume itatoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa Kura ya Maoni.  Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha Ratiba kamili.  Wakati Tume inajitahidi kufikia malengo hayo, Serikali inaendelea na mipango ya kuelimisha Wananchi kupitia Raido, Televisheni, Magazeti mbalimbali kuhusu umuhimu wa Katiba Inayopendekezwa ili kila Mwananchi aielewe vizuri na kuweza kuipigia kura kwa matakwa yake mwenyewe bila kurubuniwa muda utakapofika.

  1. Usambazaji wa Nakala za Katiba Inayopendekezwa na Hatua iliyofikiwa.

Mheshimiwa Spika,
  1. Wakati huo huo zoezi la kusambaza Nakala za Katiba Inayopendekezwa linaendelea.  Kama mtakumbuka Serikali ilipanga kuchapisha nakala 2,000,000 za Katiba Inayopendekezwa. Usambazaji wa nakala za Katiba hiyo kutoka Bohari kuu kwenda Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia  tarehe 3 Januari, 2015 hadi tarehe 18 Machi, 2015 ulifikia jumla ya nakala 1,716,010. Katika Tanzania Zanzibar (Unguja na Pemba) nakala 210,000 zilisambazwa na katika Mikoa 25 ya Tanzania Bara zilisambaziwa jumla ya nakala 1,141,300. Nakala hizo zilisambazwa katika Kata zote 3,802 za Tanzania Bara ambapo kila Kata ilipata nakala 300. Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri walisambaziwa nakala 40 kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika,

  1. Takwimu za ugawaji wa nakala za Vitabu vya Katiba Inayopendekezwa katika Taasisi zinaonesha kuwa jumla ya nakala 346,000 zilisambazwa kwa Wizara na Taasisi mbalimbali Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Wizara zimepangiwa kupata nakala 9,700, Taasisi za Serikali za Tanzania Bara nakala 79,100, Taasisi za Elimu ya Juu nakala 43,200 na Taasisi za Kidini zitapata nakala 24,000. Asasi za Kiraia nakala 6,400, Vyama vya Siasa nakala 170,100, na Taasisi nyingine kama Tanzania Private Sector Foundation, TUCTA Media Council of Tanzania na Chama cha Walimu nakala 3700.  Wizara na Taasisi za Zanzibar zimepangiwa nakala 10,000. Matumaini ni kwamba Nakala zote zitakuwa zimesambazwa kwa wahusika.  Wito wangu ni kuwaomba Wananchi kuhakikisha wanapta nakala ya Katiba Inayopendekezwa kuisoma vizuri na kuielewa na hatimaye kuipigia kura Katiba hiyo.

VIII: UFAFANUZI KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ilikusudia kuwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali [The Written Laws(Miscellaneous Amendments) Act] Na. 2/2014. Sehemu ya Tano ya Muswada huo ilikusudia kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislam [The Islamic Law (Restatement) Act], Sura ya 375. Hata hivyo, kama nilivyoeleza hapo awali Muswada huu ni miongoni mwa Miswada mine (4) ambayo haikupata nafasi ya kujadiliwa na Bunge. Serikali itatumia fursa kuendelea kushirikisha Wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua uelewa juu ya maudhui na madhumuni ya Muswada huu.

IX: CHANGAMOTO  ZA  WAFANYABIASHARA  KUHUSU UTOZAJI  KODI

Mheshimiwa Spika,
  1. Tarehe 27 Machi, 2015 Serikali ilikutana na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina (Mb.) ambaye aliongozana  na  Wafanyabiashara  hao  baada ya Kamati yake kuwasikiliza na Mheshimiwa Deo Kasanyenda Sanga (Mb.) ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo. Lengo la Kikao hicho lilikuwa ni kuzungumzia kuhusu kero na malalamiko mbalimbali ya Wafanyabiashara na kuyatafutia ufumbuzi wa pamoja.

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Kikao hicho, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Mchungaji Silver L. Kiondo alieleza kuwa, malalamiko yao ambayo wanaomba Serikali iyashughulikie ni yafuatayo:

  1. Changamoto ya Kimfumo ya Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD;

  1. Ongezeko la Makadirio ya Kodi ya Mapato kwa Asilimia 100 kwa Wafanyabiashara ambao hawana kumbukumbu za biashara zao; na

  1. Maombi ya kuachiliwa huru kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Bwana Johnson Estomihi Minja kutokana na kuondolewa kwa dhamana na Mahakama baada ya kesi inayomkabili kutajwa tarehe 26 Machi, 2015.

Mheshimiwa Spika,
  1. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, katika jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato Nchini; mwaka 2010 Serikali ilibuni Mfumo rahisi wa kulipa Kodi unaoendana na mazingira ya sasa ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia. Mfumo huo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki ulianzishwa kwa malengo ya kuboresha utunzaji wa kumbukumbu kwa Wafanyabiashara; kuongeza uwazi katika ukadiriaji wa Kodi;  kupunguza mianya ya rushwa na kukuza ulipaji Kodi kwa hiari na hivyo kupunguza malalamiko ya ulipaji Kodi yasiyo ya msingi.

  1. Aidha, Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD; unarahisisha usimamizi wa Kodi, kwani mauzo yote yanarekodiwa kwenye Mashine za Kielektroniki na hatimaye kutumwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa njia ya Mtandao wa moja kwa moja. Utumiaji ipasavyo wa Mashine za EFD huongeza ulipaji Kodi kwa hiari na hivyo kuongeza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika,
  1. Naomba nitumie fursa hii kurejea kwa muhtasari manufaa ya Matumizi ya Mashine za Kielektroniki (EFD) kwa Wafanyabiashara na Serikali. Kama mnavyofahamu kutokana na maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki za EDF zinafanya kazi zifuatazo:

Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;

Pili: Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;

Tatu: Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;

Nne: Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;

Tano: Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;

Sita: Mashine za Kielektroniki zinaweza kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu, n.k;

Nane: Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;

Tisa: Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi halali.

Mheshimiwa Spika,
  1. Utekelezaji wa Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki unatekelezwa kwa Awamu mbili. Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ulianza rasmi mwezi Julai, 2010 ukihusisha Wafanyabiashara waliosajiliwa kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Awamu ya Pili ilianza mwaka 2013 ikihusisha Wafanyabiashara waliosajiliwa kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika utekelezaji wa zoezi hili, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi wapatao 250,000 kati ya Walipa Kodi 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za Kielektroniki za EFD. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika Awamu hizi mbili, Wafanyabiashara wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile, Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika,
  1. Napenda kusisitiza kuwa, Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki ni mzuri na unawasaidia Wafanyabiashara kutunza kumbukumbu na kulipa Kodi stahiki. Nawasihi Wafanyabiashara wajenge tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zao ili waweze kulipa Kodi Stahiki badala ya kutumia Mfumo wa Makadirio ambao umepitwa na wakati. Serikali inaamini kuwa, Matumizi ya Mashine za Kielektroniki zitaongeza Makusanyo ya Kodi na kupunguza vishawishi vya Rushwa.

Mheshimiwa Spika,
  1. Baada ya maelezo hayo, napenda kueleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kushughulikia Malalamiko ya Wafanyabiashara  pamoja na  muhtasari wa makubaliano baina ya Serikali na Wafanyabiashara katika maeneo yanayolalamikiwa kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika,
  1. Serikali ilikwishaanza kushughulikia Malalamiko ya Jumuiya ya Wafanyabiashara tangu mwezi Januari, 2014, hususan kuhusu kushughulikia changamoto zinazotokana na Mfumo wa Mashine za Kielektroniki. Aidha, mwezi Septemba, 2014 iliundwa Kamati ya Taifa ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD na Kamati ya Ndogo ya Kiufundi ya kupitia mfumo wa uongoshaji wa Mizigo Bandarini. Vilevile, Wizara ya Fedha imeunda Kamati za Mikoa za kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili Wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuelimisha Umma kuhusu Matumizi ya Mashine za EFD. Kutokana na hatua hizo kwa sasa mshine za kielektroniki za EFD zimeboreshwa zaidi na kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania uwezo mkubwa wa kusimamia mauzo ya Wafanyabiashara. Aidha, zoezi la elimu kwa walipa kodi  linaendelea katika Mikoa yote Nchini.

Mheshimiwa Spika,
  1. Katika Kikao cha tarehe 27 Machi, 2015 Serikali pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara tuliafikiana kwamba:
  1. Kamati ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki (EFD) au Kamati ya pamoja ya maridhiano baina ya Wafanyabiashara na Serikail kuhusu matatizo ya kimfumo ya utozaji kodi na yale yanayotokana na mfumo wa Mashine za Kielektroniki za EFD; ikutane mapema iwezekanavyo kuanza majadiliano ili kuyapatia ufumbuzi malalamiko, changamoto na kero zinazowakabili Wafanyabiashara na kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 28 Machi 2015. Kamati husika ikamilishe kazi yake kabla ya mwisho wa mwezi Aprili, 2015;

  1. Ili kuwepo na uwakilishi mpana kwenye Kamati ya Taifa ya pamoja ya Wafabiashara na TRA, Serikali itateua  Wajumbe wawili kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) wawe sehemu ya Kamati iliyoundwa inayojumuisha Wajumbe Watatu (3) kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na Wajumbe Watatu (3) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mjumbe mmoja (1) kutoka Wizara ya Fedha;

  1. Kwa kuwa suala la Ongezeko la Kodi ya Mapato la Asilimia 100 linatokana na Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2014/2015 ambayo imepitishwa na Bunge, na linawahusu wale tu ambao hawatunzi kumbukumbu zozote za mauzo ya bidhaa zao.  Hivyo, ufumbuzi wa suala hili unapaswa ufuate utaratibu wa mchakato wa marekebisho ya Sheria husika kupitia Bunge. Tuliafikiana kuwa, Jumuiya ya Wafanyabiashara baada ya kujadiliana ndani ya Kamati ya pamoja iwasilishe mapema mapendekezo ya kurekebisha Mfumo wa Kodi unaolalamikiwa ili maoni yao yajadiliwe kwenye Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) wakati wa mchakato wa maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2015/2016 na kufanya marekebisho stahiki. Hata hivyo, kwa kuwa suala hili litachukua muda ninawashauri Wafanyabiashara waanze kulipa robo ya kodi ilivyo sasa ili kuepuka kudaiwa malimbikizo baada ya Sheria kurekebishwa;

  1. Kwa kuwa Mfumo wa Matumizi ya Mashine za Kielektroniki  una  faida  nyingi  na manufaa makubwa kwa Wafanyabiashara  na  Serikali;  na  kwa  kuwa Mfumo huo unatumika katika Nchi nyingi Duniani;  tumekubaliana kuwa, Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) iendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha Wafanyabiashara wenzao kuhusu umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara zao kwa kutumia Mashine za Kielektroniki za EFD na kulipa kodi stahiki. Serikali inaahidi kuwa itaendelea kushughulikia changamoto za kimfumo na utawala zilizopo za Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD na tumesisitiza kuwa suala hili lijadiliwe kwenye Kamati ya Kitaifa iliyoundwa ili kuzipatia ufumbuzi kwa haraka;

  1. Kuhusu suala la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiasha Nchini, Bwana Johnson Estomihi Minja Kikao kilielezwa kwamba, Bwana Minja alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha Mikutano ya uchochezi ya kuzuia matumizi ya Mashine za Kielektroniki na kuhamasisha Wafanyabiashara kufunga maduka yao. Tuliwaeleza Viongozi wa Wafanyabiashara kwamba suala hilo lipo chini ya Mamlaka nyingine ambayo ni Mahakama; na kwamba Mhusika alirejeshwa rumande tarehe 26 Machi, 2015 kutokana na kukiuka mojawapo ya masharti ya dhamana aliyopewa na Mahakama. Hivyo, siyo busara kwa Serikali kuingilia uhuru wa Mhimili wa Mahakama. Serikali inaamini kuwa Mhusika atatimiza masharti ya dhamana kesi yake itakapotajwa tena leo tarehe 01 Aprili, 2015; na hivyo kuachiwa huru. Taarifa zilizopatikana mchana wa leo zinaonesha kwamba, Bwana Johnson Estomihi Minja amepata dhamana na yuko huru jioni ya leo;

  1. Mwisho, tulikubalina kuwa kwa sababu Serikali imeonesha nia njema  ya kushughulikia  mapema iwezekanavyo malalamiko na changamoto zinazowakabili Wafanyabiashara Nchini,       ni vyema Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara baada ya Kikao kile, kwenda kutoa maelekezo kwa Wafanyabiashara katika Mikoa yote Nchini kusitisha mara moja mgomo unaoendelea na wawatake Wafanyabiashara kufungua maduka yao ili Wananchi wapate huduma na bidhaa muhimu.

Mheshimiwa Spika,
  1. Serikali inathamini sana mchango wa Wafanyabiashara katika Kukuza Uchumi na kuchangia Mapato ya Serikali. Napenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, Serikali ipo tayari kukaa pamoja na Wafanyabiashara kuzungumzia changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka. Naomba nitumie fursa hii kutoa Wito kwa Wafanyabiashara wote Nchini kufungua Maduka yao ili waweze kutoa huduma muhimu za kuuza bidhaa kwa Wananchi. Nasisitiza kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha kulipa Kodi Stahiki.

Mheshimiwa Spika,
  1. Natoa Wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi  zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za EFD na kujenga tabia ya kufanya biashara kwa kutunza kumbukumbu za mauzo ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta Maendeleo Endelevu kwa kulipa Kodi Stahiki.

X: MALALAMIKO KUHUSU USAJILI MPYA WA BODABODA

Mheshimiwa Spika,
  1. Pamoja na malalamiko hayo, yapo pia malalamiko ya Wafanyabiashara wa Pikipiki na Bajaj ambao wanailalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwamba inawatoza Shilingi 250,000 hadi 300,000 kwa kusajili upya Pikipiki moja. Wafanyabiashara ya Bodaboda wamesema Mmiliki mpya wa Pikipiki au Bajaj anatakiwa kulipia leseni yake ya barabara pamoja na kodi nyingine ambazo ama Mmiliki wa zamani hakuzilipia; au Makampuni yaliyowauzia Pikipiki na Bajaj hizo hawajalipa kodi. Tulipokutana na Wafanyabiashara na Wenye bodaboda wanauliza kwa nini Mamlaka ya Mapato Tanzania, isiwatafute wale Wamiliki wa zamani na kuwadai Kodi husika.

Mheshimiwa Spika,
  1. Nilikutana na Wafanyabiashara husika pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo maelezo ya Kitaalam tuliyopewa ni kwamba tangu tarehe 1 Julai, 2014 Serikali ilifuta Leseni ya barabara kwa Pikipiki na kuwataka Wamiliki wote kufanya Usajili upya. Katika zoezi hilo, Wamiliki wote wanatakiwa kuhakikisha kuwa wamelipa ushuru na ada zifuatazo:-

Kwanza: Kulipa Kodi ya Usajili (Registration Fees) ambayo ni Shilingi 10,000/= (kwa Wamiliki Wapya);

Pili: Kulipia Ada ya Leseni ya Barabara (Road Licence) ya Pikipiki mpya ambayo ni Shilingi 50,000 kwa Mwaka;

Tatu: Kulipa Ada ya Zimamoto ambayo Sh.10,000 kwa Mwaka;

Nne: Kulipa Ushuru wa Stampu (Stamp Duty) ambao ni Asilimia moja (1%) ya   thamani ya Pikipiki;

Tano:    Kwa wale walionunua Pikipiki kutoka kwa Wamiliki wa zamani wanatakiwa pia kulipa Kodi ya Uhamisho wa Umiliki ambayo ni takriban Shilingi 27,000/= pamoja na ushuru wa Stempu (Stamp Duty) wa Asilimia moja (1%) ya thamani ya pikipiki husika.

Mheshimiwa Spika,
  1. Ili kuwezesha Wamiliki wa pikipiki kulipa kodi hizo kwa urahisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuzingatia Sheria husika, ilitoa unafuu wa kumruhusu Mlipa Kodi, kulipia Tozo na Ada hizo nilizozitaja kwa Awamu Nne (4) kwa mwaka. Ukomo wa muda wa kulipia kodi hizo ilikuwa imepangwa kuishia tarehe 31 Machi, 2015. Baada ya Serikali kutatafakari kuhusu malalamiko hayo ya Wamiliki wa bodaboda, imeamua kusogeza mbele muda wa ukomo wa Usajili mpya wa Namba za Pikipiki hadi Mwezi Desemba, 2015.


XI: HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa kumalizia na kama ilivyo ada, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa kutuongoza vizuri na kwa busara kubwa.  Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri wanayofanya kila wanapopata nafsi ya kukalia kiti cha Spika.  Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri ya kujadili na kupitisha Miswada yote iliyowasilishwa wakati wa Mkutano huu.

Mheshimiwa Spika,
  1. Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu.


  1. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.

Mheshimiwa Spika,
  1. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana tena katika Mkutano wa 20 wa Bunge lako Tukufu ambao ni mkutano wa mwisho Kikatiba wa Bunge la Kumi na ambao utakuwa mahususi kujadili Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika,
  1. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 12 Mei,  2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 20 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika,

  1. Naomba kutoa Hoja.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.