Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali
ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu
yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani
mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi na zaidi ameacha
manung’uniko na mgawanyiko.
Rais Jakaya Kikwete anaondoka madarakani akiwa ameshindwa kuwatimizia waumini wa Kiislamu ahadi ya kuwaundia Mahakama ya Kadhi. Picha na Maktaba |
Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa
uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro
ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya
Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu
Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.
Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais
Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani
Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi,
vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na
Mahakama ya Kadhi.
Sheria ya Habari
Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo
vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini
haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi
katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo
mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia
Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.
Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi
anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini
wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia
gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013
gazeti la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa
siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni
(Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).
Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania
Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda
na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd
iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka
ya uchochezi.
Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa
kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa
mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia
na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa
gazeti la The EastAfrican nchini.
Katiba Mpya
Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010
haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8, 2010 siku
alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai
Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa
Watanzania Katiba Mpya.
Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete
alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata
walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema
kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, akaunda
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba
ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba.
Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika
Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua
BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa
CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba
ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.
Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK,
likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015
Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30.
Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR
kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni
ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mahakama ya Kadhi
Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza
ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali
haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama
hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.
Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni
rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais
Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na
wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka
iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo
yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.
Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na
uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao
lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.
Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna
uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi
nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za
kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake
hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya
nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa
maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.
Mgogoro Zanzibar
Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni
ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM
wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao
ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa
mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia
maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK).
Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa
umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia
na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa
kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu
wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani.
Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani
aliyepinduliwa mwaka 1964, Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha
masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi
mwaka 1964.
Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid
aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa
Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya
tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth,
kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.
Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia
katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni
kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha
kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho
wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta
ya ufugaji iwe ya kisasa.
Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya
Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika
pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma
za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi
iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika
ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.
Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya
kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa
wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali
ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji
katika maeneo tofauti nchini.
Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo,
waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine
zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira
na uhasama vimetanda kila mahali.
Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa
migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na
wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao
wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete
anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.
Vita ya ufisadi
Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania
aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa
mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima
ushahidi uwepo kwa asilimia 100.
Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa
tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya
Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa
kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa
kuwashughulikia.
Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na
Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa),
walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya
Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya,
waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa
Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.
Chanzo cha habari na gazeti la kila siku la Mwananchi
Post a Comment