Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ubalozi wa Uholanzi Tanzania na wadau wa ufugaji wa kuku kwa pamoja wamezindua mradi wa kutathmini mtaala wa mafunzo ya ufugaji wa kuku kwa vyuo vya mifugo, unaolenga kuongeza ufanisi na uzalishaji wa kuku nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Utabibu wa Wanyama Tanzania (TVLA), Dkt Stella Bitanyi, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, alisema mradi huo unalenga kuweka misingi katika kuboresha mtaala wa ufundishaji wa ufugaji wa kuku.
Aliongeza kwamba mradi huo unakuja na majawabu ya namna bora ya kufundisha Watanzania wakulima, hasa wanawake na vijana jinsi ya ufugaji bora wa kuku wa kibiashara na kwa vitendo zaidi.
Alisema nchini Tanzania, asilimia 96 ya wakulima wa mifugo wanafuga kuku wa kienyeji, mara nyingi katika makundi madogo ya kuku kwa wastani wa hadi kuku 20, lakini hutoa chini ya asilimia 20 ya mahitaji ya nyama ya kuku na mayai nchini.
“Kasi ya ukuaji wa sekta hii ni ndogo, ikiwa ni wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka, uzalishaji wa mayai ni chini ya mayai bilioni 2.5 kwa mwaka, na kiwango cha matumizi ni sawa na yai moja kwa kila mtu kwa wiki,” alisema.
Alieleza kwamba kuku mmoja kwa kila mtu kwa mwaka, matumizi yanapendelea kwa wakazi wa maeneo ya mijini na wenye kipato cha kati hadi cha juu, lakini mahitaji ni makubwa nchi nzima.
Alisisitiza kwamba ufugaji wa kuku ni mojawapo ya njia bora za kupunguza umaskini hasa kwa wanawake na ajira kwa vijana katika ufugaji wa kuku.
Dkt Bitanyi aliongeza kwamba mradi wa kupitia mtaala wa tathmini ya ufugaji wa kuku ni muhimu kwa sababu unachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha lishe na usalama wa chakula ili kuhakikisha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.
“Sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania inakua kwa kasi kutokana na mahitaji ya protini yanayoongezeka kulingana na idadi ya watu inayokua kwa haraka, lakini sekta hii bado inafanya kazi kwa njia ya kiasili zaidi katika muundo usio rasmi,” alieleza.
Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi Dar es Salaam, Mshauri wa Masuala ya Uchumi, John Mike Jagger alisema wao kama Ubalozi na makampuni ya Uholanzi wanafurahi kuzindua mradi huu unaolenga kuharakisha maendeleo ya ufugaji wa kuku.
“Sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania ina uwezo mkubwa na inakua kwa kasi, ikiongozwa na mahitaji ya protini kwa sababu ya idadi ya watu inayokua kwa haraka,” alisema.
Aliongeza kwamba ingawa sehemu kubwa ya sekta hii bado inafanya kazi kwa njia isiyo rasmi, wakulima wengi wa kuku wanahama kutoka kwa kilimo cha kujikimu kwenda kwenye uzalishaji wa kibiashara.

Jagger alifafanua zaidi kwamba mradi wa tathmini ya mtaala wa ufugaji wa kuku utaleta fursa zinazovutia zitakazowezesha wakulima kupata maarifa sahihi, mafunzo, na maendeleo ya ujuzi katika sekta ya ufugaji wa kuku na kuongeza ajira nchini.
“Kuwekeza katika elimu na maendeleo ya ujuzi ni muhimu kwa kuboresha ufanisi, na uzalishaji endelevu katika sekta hii,” alisema.
Johan Hissink, kutoka Mradi wa Kituo cha Mafunzo cha Aeres, Uholanzi, alisema kwa kushirikiana na Wakala wa Mafunzo wa Vyuo vya Mifugo nchini (LITA) wataainisha changamoto, matatizo, na vikwazo vya sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania na kushirikiana kupitia mtaala ili kuyashughulikia kwa ufanisi.
“Tupo hapa kusaidia kukuza mtaala wa ufugaji wa kuku utakaosaidia sekta hii kushughulikia changamoto zake kuanzia kwenye vituo vya mafunzo ya ufundi hadi ngazi ya mashambani hasa kwa wakulima vijana na wanawake vijijini,” alieleza.
Afisa Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt Pius Mwambene alisema mradi wa kupitia mtaala wa tathmini ya ufugaji wa kuku utawafundisha wakulima na wadau wengine wa ufugaji wa kuku ujuzi zaidi na mbinu za kiufundi.
“Tuna mtaala katika sekta ya ufugaji wa kuku na kilimo lakini huu utaangazia zaidi maendeleo ya ujuzi kwa kuwafanya wakulima kuwa na ujuzi katika ufugaji wa kuku,” alisisitiza.
Dkt Mwambene aliongeza kwamba mradi huo unalenga kubadilisha mafunzo yawe ya vitendo zaidi na ubunifu katika ufugaji wa kuku kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta hiyo kama msingi wa ustawi wa jamii nchini.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.