Dar/Dodoma. Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kimemfungulia mashtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni kwamba wanaokaidi
maagizo ya dola wapigwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba akiwaonyesha waandishi wa habari, stakabadhi na hati ya mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam jana. Picha na Michael Jamson |
Hatua hiyo ya LHRC imepingwa vikali na Mkurugenzi
wa Mashtaka ya Umma (DPP), Dk Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa
mashtaka yoyote dhidi ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni
haikuwa piga ua.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alifungua mashtaka hayo katika Mahakama Kuu jana akisema kuwa wanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba Ibara 13 (1). Pinda ametajwa kuwa ni mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 24.
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold
Sungusia alisema jana kwamba, mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo
ya kikatiba iliyofunguliwa na LHRC na Chama cha Wanasheria Tanzania
(TLS) ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Alisema katika kesi hiyo, kuna jopo la mawakili
wasiopungua 20 na kwamba wamepata saini za wananchi 2,029 wanaopinga
kauli hiyo ya Pinda na kuunga mkono kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dk Ringo Tenga
alisema katika kesi hiyo wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi
za binadamu na kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki
hizo.
Kauli yenyewe
Wakati wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa
Waziri Mkuu bungeni, Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu
aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua
stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha
vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola
vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo
kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema...
mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo,
umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna
nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa
misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni
imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema
muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.” Kesi
hiyo itakayosikilizwa na majaji watatu, haina uhusiano na kesi nyingine
ambazo wajibu maombi hupewa siku 90 kujibu hoja zilizowasilishwa. Kesi
hiyo imefunguliwa kwa mujibu wa Katiba Sura ya Tatu.
Akizungumza juzi kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma baada ya
kufungwa kwa Warsha ya Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wa Serikali
ngazi ya mikoa, Dk Feleshi alisema hakuna uhalali wa mashtaka hayo kwa
sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
“Hii haikuwa kuchochea apige watu, alichosema ni
kupiga wale wasiotaka kutekeleza amri halali na zaidi alisema piga
lakini si kupiga na kuua,” alisema.
Mkutano huo uliendeshwa chini ya ulinzi mkali huku
kukiwa na udhibiti wa kuvuja siri kwa kiwango cha juu. Pamoja na mambo
mengine, ulikuwa ukijadili mbinu za kisasa katika kuendesha kesi pamoja
na kujiuliza sababu za Serikali kushindwa katika kesi nyingi.
“Kwa sababu lile neno kupiga ni lazima lipewe
maana pana huwezi kumpiga tu mtu hivihivi ambaye hakuvunja sheria lakini
nilivyoelewa, ilikuwa ni hivyo, ni sawa na mtu ambaye anamshambulia
askari,” alisema Dk Feleshi.
Alisema kuna sheria ya kutumia nguvu pale ambako
kuna mkusanyiko usiokuwa wa halali pindi raia wanapokaidi kutawanyika
kwa hiari hivyo hakuna shaka kauli ya Waziri Mkuu ililenga hivyo.
Hata hivyo, alisema hajapata taarifa za LHRC
kumshtaki Waziri Mkuu kimaandishi na kwamba akizipata atatoa ufafanuzi
baada ya kuona lengo la mashtaka.
Msimamo
Akizungumza baada ya kufungua mashtaka hayo, Dk
Bisimba alisema Waziri Mkuu anaweza kushtakiwa kwa kuwa alizungumza kwa
nafasi yake ya Waziri Mkuu na si mbunge na kusisitiza kwamba hakuna
aliye juu ya sheria na kudai kwamba kauli hiyo ni kinyume cha Katiba.
Alisema kuwa kila anayevunja Katiba lazima
ashughulikiwe kisheria na kwamba mahali pake ni mahakamani tu. Alisema
kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, kauli na amri kama hizo zinapotolewa
na kiongozi mwenye hadhi kama ya mdaiwa wa kwanza (Waziri Mkuu)
huchukuliwa kama sheria inayopaswa kutekelezwa na wakala wa utekelezaji
wa sheria kama vile polisi. Wadai hao wanadai kuwa kwa ufahamu wao
polisi wanaweza kuchukulia kauli hiyo kama amri halali kutoka kwa mkubwa
wao na hivyo kuwapiga na kuwatesa watu wasio na hatia, kinyume cha
Katiba.
Pia wanadai wanatambua kuwa Ibara ya 100 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa kinga kwa wabunge na
uhuru wa maoni bungeni. Hata hivyo, wanatambua kuwa Ibara ya 100 (2) ya
Katiba hiyo inawawajibisha wabunge wote chini ya masharti ya Katiba na
kwamba kauli aliyoitoa Waziri Mkuu Pinda inakiuka Ibara ya 12(12).
Hivyo wanaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa kauli na amri hiyo aliyoitoa Pinda inavunja Katiba.
Mkurugenzi wa taasisi inayofuatilia Mwenendo wa Bunge (Watch),
Marcos Albania alidai kwamba wamegundua kuwa kauli hiyo ya Pinda ni moja
kati ya matamko makubwa yanayovunja Katiba.
Alisema mbali na shtaka hilo, kuna la pili dhidi
ya Waziri Mkuu Pinda, ambalo hawajalifikisha mahakamani ambalo pia
linatokana na kauli hiyo aliyoitoa bungeni kwamba: “Sasa wamechoka.”.
Post a Comment