Dar es Salaam. Rais wa Mstaafu wa Marekani, Bill Clinton jana
alifanya ziara katika makazi ya watu duni eneo la Vingunguti, wilayani
Ilala Dar es Salaam, ambapo alikagua miradi midogomidogo ya wananchi
inayofadhiliwa na mfuko wake (Bill Clinton Foundation).
Rais Jakaya Kikwete akimpokea mgeni wake rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton anayepanda kwenye gari |
Clinton alitembelea eneo hilo akitokea moja kwa
moja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam
(JNIA), alipowasili akiwa katika ziara ya nchi mbalimbali za Afrika
kukagua miradi inayoendeshwa na mfuko wake.
Katika eneo hilo rais huyo mstaafu alipokewa kwa
shamrashamra mbalimbali ikiwamo ngoma za kiasili huku baadhi ya wananchi
wakipigwa butwaa na kutoamini macho yao kwa kiongozi huyo kutembelea
makazi yao.
Aidha, Clinton alipata wasaa wa kusalimiana na
wakazi wa Vingunguti wakiwamo watoto ambao walishindwa kuzuia hisia zao
wakijaribu kumsogelea, hali iliyomsukuma Clinton kuwasogelea na
kuwasalimia kwa kuwashika mikono.
Maneno ya ‘Welcome Vingunguti Clinton‘ yalisisika
kutoka kwa wananchi kuashiria kumkaribisha rais huyo wa 42 wa Marekani
wakati alipowasalimia akitumia takriban dakika 15.
Clinton alikagua miradi ya midogomodogo ya
wananchi iliyo chini ya mfuko wake ikiratibiwa na kutekelezwa na Shirika
la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Plan) pamoja na Benki ya Barclays
kupitia Vikoba.
Miradi aliyokagua ni pamoja na saluni za kinamama,
ushonaji na chips ambapo pia alishuhudia mmoja wa wanachama wa vikundi
hivyo akikabidhiwa mkopo wa Sh100,000 ambaye alieleza mbele ya Clinton
kuwa atazitumia kwa mradi wa maandazi, hali iliyomfanya rais huyo na
umati wa watu uliohudhuria kucheka.
Akizungumza katika ziara hiyo Clinton alizishauri
benki nchini, kuwekeza kwenye vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba)
akieleza kuwa ndiyo mkombozi kwa wananchi hasa wanawake.
“Nimekuwa kwenye miradi hii kwa miaka 30 kabla
sijawa rais, hivyo basi najua umuhimu wake. Benki zinatakiwa zisaidie
Vikoba kwani vikundi hivyo huwafikia wananchi kwa haraka na wepesi hivyo
basi kunahitajika njia mbadala za kuhakikisha vinakuwa imara,” alisema
Clinton na kuongeza;
“ Raha ya maendeleo ni kuona watu wanajitegemea wenyewe katika shughuli za kujiingizia kipato.”
Mmoja wa wananchi walionufaika, Zainab Paul ambaye
ni mwanachama wa Kikundi cha Amani Hisa alisema kuwa kupitia Mfuko wa
Bill Clinton na Vikoba ameweza kujikwamua kimaisha ikiwamo kumlipa mtoto
wake karo ya shule.
“Kikundi chetu kina wanachama 30 na huwa tunanunua
hisa kwa Sh2000 na kila mwanachama anaruhusiwa kukopa zaidi ya mara
tatu,” alisema Paul.
Clinton alieleza kufurahishwa kwake na hatua walizofikia wakazi
hao wa Vingunguti akiwapongeza kinamama kwa jitihada zao na baada ya
ziara hiyo alielekea Ikulu kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Plan, Tanzania, Jorgen
Haldorsen alisema shirika lake limekuwa likihudumia nyanja za kiuchumi
na kijamii kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa kada ya chini wanapata
huduma mbalimbali ikiwamo afya.
Naye, Mshauri wa Mambo ya Kujikimu wa Plan Stella
Tungaraza aliwataka wananchi kujiunga zaidi na Vikoba na kwamba shirika
lake limepanga kuanza kutoa mafunzo ujasiriamali kwa vijana ili waweze
kujikwamua kiuchumi.
Baadaye Rais Clinton alitia saini makubaliano ya taasisi yake ya Bill Clinton Foundation kusaidia sekta ya kilimo nchini.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Ikulu jijini Dar
es Salaam na Sophia Kaduma ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
na Chakula pamoja na mwakilishi wa taasisi ya rais huyo mstaafu, Walker
Morris.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Clinton
alisema wakulima wa Tanzania wanatakiwa kutambua kuwa kuna nchi nyingine
zinashindwa kuendesha shughuli za kilimo kutokana na uhaba wa ardhi au
kuwa na ardhi isiyokuwa na rutuba na kuwataka watumie fursa hiyo kukuza
uzalishaji wa kilimo .
Alisema kama wakulima hao watajituma Tanzania inaweza kuzalisha chakula ambacho kinaweza kulisha dunia.
Chanzo cha habari na gazeti la Mwananchi.
Post a Comment