Katibu Mkuu wa Shrikisho la mpira Afrka Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye |
Musonye akizungumza
na Mwananchi (Gazeti dada la Mwanaspoti), alisema Maximo aache woga wa kuhofia
kufungwa kwa kupeleka kikosi cha pili kwenye mashindano ya kombe la kagame
linaloanza leo jijini Kigali, Rwanda.
Musonye amemhukumu
Maximo kwa kumwita mwoga bila ya kuzingatia programu ambayo kocha huyo
amejipangia katika timu yake ya Yanga. Kauli aliyoitoa Musonye, pia imekuwa
ikitolewa na baadhi ya wadau wa soka hapa nchini ambao nao mara kwa mara
wanasema kocha huyo ni mwoga wa kufungwa.
Sitaki kuamini kama
Maximo anaogopa kufungwa kwa kuwa atashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na
atakutakana na upinzani, hivyo kama kufungwa atafungwa tu.
Naamini kocha huyo
anajipanga na kuamini kile anachokifanya kwa ajili ya timu yake na kazi
aliyopewa.
Watanzania wanaosema
Maximo ni muoga watakuwa bado hawajaelewa falsafa ya kocha huyo kwani hata
alipokuwa akiifundisha Taifa Starz, aliamnini katika kujenga timu kwa kuwatumia
wachezaji vijana.
Maximo anajua
anachokifanya katika kuandaa timu yenye ushindani tofauti na kauli ya Musonye.
Tatizo la watu wa
Afrika Mashariki na Musonye akiwamo, tumekariri majina ya wachezaji wa soka
tofauti na mipango ya kocha kama Maximo.
Tunapenda njia za
mkato, ndiyo maana Tanzania na Kenya zimetolewa na Msumbiji na Lesotho katika harakati za kuwania
kufuzu makundi kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)
zitakazofanyika Morocco mwakani.
Musonye alitaka
Yanga ishiriki Kagame kama Tanzania na Kenya zilivyoshiriki mbio za kwenda
Morocco dhidi ya Msumbiji na Lesotho, kwa kuwa hazikuwa na maandalizi ya
kutosha,
Maximo hajakaa na
kikosi chake chote na kuna wachezaji mpaka leo hii anaziona picha zao
magazetini tu. Wachezaji aliokaa nao ni hao aliowachagua kwenda Rwanda.
Lakini mtu kama
Musonye ambaye naamini hajui lolote kuhusu ukocha pamoja na kuwepo kwenye soka
kwa muda mrefu, anaendelea na kukariri majina ya akina Mrisho Ngasa!
Katimu Mkuu huyo wa
Cecafa hajiulizi kwa nini nchi za Malawi, Zambia, Lesotho na Zimbabwe zinapiga
hatua katika soka?
Kwa nini Musonye
anaendeleza siasa zilizozifanya nchi hizo kuanzisha shirikisho lao la Cosafa
ambalo linaonekana kuwa na nguvu kuliko Cecafa?
Ikumbukwe kwamba
wakati tukiwa pamoja, nchi zetu za Afrika Mashariki zilikuwa zikipata upinzani
wa kweli kutoka kwao, Tanzania haikuwa na uwezo wa kuifunga Zambia!
Baada ya nchi hizo
kujitoa na kuunda Cosafa, bado kina Musonye wanaendelea kupiga siasa
zilizotufikisha hapa.
Musonye hawataki
wachezaji vijana, eti hawawezi kufanya biashara anadhani kina Ngasa watacheza
soka mpaka lini?
Naamini biashara
ingeweza kuanguka kama timu mwenyeji angeingiza kikosi cha pili lakini kwa
Yanga siioni madhara zaidi faida ya kuzalisha vipaji vinavyopotea.
Katika hili siiuoni
uoga wa Maximo, kocha hawezi kuwabeba wachezaji kama mizigo kwenye mashindano.
Tanzania tunahitaji
vipaji vipya, Maximo alikuwa na mkakati wa kuvizalisha kwa ajili ya Yanga,
Taifa Stars na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Binafsi nitamhukumu
Maximo kwa uwezo wake wa kufundisha uwanjani siyo wa kwa tuhuma za woga.
Makala hii
imeandikwa na Mohamed Kuyunga kupitia Meseji Senti ya gazeti la Mwanaspoti
kuyungajunior@gmail.com
Post a Comment