UAMUZI wa ushirikiano wa wanaotaka Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuamua kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba unatishia kusababisha kuvurugika na kuvunjika kwa  mchakato wa kuelekea Katiba mpya.
Viongozi wa wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)

Waraka huu basi ni kwa viongozi, wapenzi na mashabiki wa Ushirikiano huu ambao umekuwa ukitoa mawazo mbadala na yale ya viongozi walioko madarakani chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Kwa vile dalili zote zilizopo zinaonyesha kuwa mchakato huu umegota na kuendelea kwake kunategemea kwa kiasi kikubwa kupiga magoti kwa CCM basi nimeonelea niandike waraka huu wa wazi kwa uongozi wa UKAWA, wanachama na mashabiki.

Lengo la waraka huu wa wazi ni kutoa wito kwa UKAWA kujitoa mara moja kwenye mchakato huu kwani uwezekano wa wao kurudi na kusalimu amri mbele ya matakwa ya wenye nguvu ni sifuri.

Nimewahi kuandika huko nyuma mara baada ya wao kutoka kuwataka warudi wakapambane bungeni huko huko na baadaye warudi kwa wananchi.

Hata hivyo, naamini kama wangefanya wakati ule lingekuwa ni jambo zuri lakini sasa tukichukulia mambo yote ambayo yametokea hadi hivi sasa naamini hawawezi kurudi bungeni bila kuonekana wamegeuka na kula matapishi yao.

Uamuzi wa UKAWA kujitoa kwenye Bunge la Katiba ni wa lazima sasa hivi kwa sababu kubwa mbili; kwanza, kutaokoa mabilioni ya fedha ambayo yanaweza kuliwa tena bila huruma kwa kufanya vikao vya Bunge ambavyo havitaenda popote kwani uwezekano wa kupata Katiba mpya na kukamilisha mchakato huu kabla ya Uchaguzi Mkuu haupo.
Jambo la pili ni kuwa uamuzi huu wa kujitoa ukichukuliwa sasa utatoa nafasi mbili muhimu sana.
Nafasi ya kwanza utalazimisha CCM na uongozi wake wote na wale wanaokubaliana na misimamo ya CCM kuamua kuchukua hatua inayofaa kunusuru mchakato huu.

Ni wazi kuwa wajumbe wote wa UKAWA wakijitoa ni vigumu rasimu ya Katiba kupita kwani itakuwa vigumu kupata wingi wa wajumbe wanaotakiwa kupiga kura kupitisha vipengele na ibara za rasimu ya Katiba.

CCM italazimisha kubadilisha Sheria waliyoitunga bungeni ili kujipa uhalali wa kuendelea na mchakato huu.
Nafasi ya pili itakayotolewa ni kwa UKAWA kujiunganisha zaidi na kujipanga kushinda chaguzi zilizoko mbele – ule wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu – na hivyo kujiweka katika nafasi ya wao kuanzisha mchakato mzuri, sahihi, wa kina na halali wa kuandika Katiba mpya kuliko mchakato huu wa sasa ambao kama nilivyowahi kuonyesha nyuma ni mchakato haramu.

Hivyo, ombi langu kwa UKAWA ni kufikiria kama muungano wao ni wa kimkakati tu au ni muungano wenye lengo la kwenda zaidi ya hapo.
Kama UKAWA – na hili nimewahi kulionyesha nyuma – imeungana kwa lengo tu la kutaka Katiba mpya basi muungano au ushirikiano wao huu ni dhaifu sana na utawasumbua mbele hasa kama CCM itaamua kukubali matakwa ya UKAWA na kuwarudisha bungeni.

Chama cha Mapinduzi kinaweza kabisa kukubali kuwa kitakachojadiliwa iwe ni rasimu ya Warioba tu na maamuzi mengine na hivyo kuwafanya UKAWA wasiwe na hoja tena ya kusimamia.

Matokeo ya hili kimkakati ni kwa CCM kuhakikisha kuwa wajumbe wake kwenye Bunge la Katiba wanafuata maelekezo ya chama na kwa kutumia nguvu za kura – iwe ya wazi au ya siri,  si hoja – kuzima mapendekezo ya UKAWA.

Lakini kama ushirikiano huu ni zaidi ya suala la Katiba mpya; kwamba ni muungano ambao unataka kuleta sera na maono mbadala kwa taifa na hata kushirki uchaguzi basi suala la  kujitoa kabisa kwenye mchakato huu sasa hivi na mara moja na daima haliepukiki.

Haliepukiki kwa sababu kuendelea kwa namna yoyote ile kushiriki katika mchakato huu ni kuupa uhalali ambao sasa hivi unakosekana.
Endapo UKAWA wataamua kurudi na kushiriki wajue kabisa watakuwa chini ya huruma ya watawala.

Tumeshashuhudia kwenye hii midahalo na majadiliano yaliyofanyika siku hizi chache zilizopita na jambo moja liko wazi – tofauti baina ya pande hizi mbili ni kubwa sana kiasi kwamba njia pekee ya kuweza kuwasogeza karibu ni kutengeneza geresha ya kisiasa.

Geresha hii naamini itakuwa ni CCM na uongozi wake kukubali (compromise) bila kukubaliana. Yaani, itaonekana watu wamekubaliana lakini kumbe hawajakubaliana hasa kile wanachotakiwa kukubaliana.

Endapo UKAWA wataingia kwenye mtego huu wa kukubali bila kukubaliana (a compromise that’s not a compromise) watajikuta wanalazimika kuanza tena kubishana na watu wale wale, kuhusu mambo yale yale na wanaweza kuwa na wakati mbaya zaidi kusimamia hoja zao kuliko wakiamua kujitoa.

Wakijitoa sasa wataweza kujipanga kama nguvu ya kisiasa (political force) kukaa chini na kuzungumzia ushirikiano wa kisera na maono ya taifa na hatimaye kuweza kutengeneza ajenda moja ya kisiasa ambavyo ushirikiano huu utasimama pamoja kwenye chaguzi.

Ushirikiano wa aina hiyo utakuwa ni zaidi ya mapatano; utatakiwa uwe ni ushirikiano ambao vyama hivi vitakaa chini na kuandika makubaliano yao (memorandum of understanding) ili angalau kuwe na msingi wa kisheria wa ushirikiano huu kwani hivi sasa sidhani kama hili liko wazi zaidi.

Ni wazi kuwa endapo UKAWA utashindwa kusimama na kujipanga vizuri basi kwa mara nyingine tena Watanzania wanaotaka mabadiliko wanaweza kujikuta mioyo ikivunjika tena kwani nafasi adhimu kama hii haitatokea tena kwa miaka mingi ijayo.

Ni wakati wa wanachama na mashabiki kuanza kuweka shinikizo kwa viongozi wa kisiasa kuonyesha uthubutu zaidi ya ambao wameuonyesha ili hatimaye wao ambao wamekuwa wakidai Katiba mpya kwa miaka mingi sasa waweze kushinda uchaguzi na kuingiza Serikali ambayo kweli kabisa itakuwa tayari kuliongoza taifa kuandika Katiba mpya kutoka kwa wananchi, kwa ajili ya wananchi, na ya wananchi; ambayo itadumu kwa vizazi na vizazi!
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.