TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA SHAMBULIO LA KIKATILI DHIDI YA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI BW. ABSALOM KIBANDA
Machi
07, 2013
Mtandao wa watetezi wa
haki za binadamu ambao ni kusanyiko la zaidi ya asasi 70 za kiraia zinazotetea haki za binadamu chini ya mwamvuli wa THRD-Coalition unalaani
vikali shambulio la kinyama alilofanyiwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Absalom Kibanda usiku wa kuamkia jana Jumatano tarehe 6 Machi, 2013.
Usiku wa kuamkia
tarehe 6/3/2013 Bwana Kibanda alivamiwa wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwake
Mbezi juu. Watu hao walimteka na kisha wakamtesa kinyama kwa kumng’oa meno,
kucha, kidole na kuliharibu vibaya sana
jicho la upande wa kushoto. Huu ni ukatili, unyuma dhidi ya utu wa
binadamu.Baada ya kutekeleza azma yao walimtupa umbali wa mita 30 toka
alipokuwa amepaki gari lake.
Uchunguzi tulioufanya
bado haujatujapatia habari za undani zaidi na za uhakika wa tukio hilo. Lakini
kwa taarifa za awali kwa asilimia kubwa linahusiana na kazi yake ya utetezi wa haki za
binadamu kupitia katika taaluma yake ya uandishi wa habari. Hii ni kwa sababu
pia tayari alishafunguliwa kesi mahakani inayohusu uandishi wake.
Tunasema hivyo kwa
sababu vitisho dhidi ya wanahabari na watetetezi wengine wa haki za binadamu vinataka
kuzoeleka sasa hapa nchini jambo ambalo halikuwapo katika miaka ya nyuma. Takribani
ndani ya miezi 10 sasa zaidi ya watetezi wa haki za binadamu 10 wakiwamo waandishi wa habari wameshajeruliwa, wamepata vitisho na kuuwawa.
Matukio haya yanashiria lengo la kutaka kuzima sauti za watetezi wa
wanyonge kwa visingizio mbali mbali huku matukio ya aina hii wakati mwingine
yakipewa sura tofauti tofauti ikiwamo uhalifu wa kawaida, visa vya kudhulumiana
na visasi vya kimapenzi. Ni dhahiri
wanaofanya hivyo wana malengo mabaya ya kuchafua jina na taswira nzuri ya nchi
yetu katika Jamii ya Kimataifa kwa malengo binafsi.
Wakati tukio hili linapojitokeza
sasa, bado Mtandao wetu unafuatilia kwa karibu kufungiwa kwa gazeti la
Mwanahalisi na mazingira ya kukamatwa na kuhojiwa kwa waandishi wa gazeti la Tanzania Daima kulikofanywa na Jeshi la
Polisi hivi karibuni kwa kile kilichoitwa kwamba ni kuandika habari za
uchochezi.
Hatupendi kuingilia
wala kukwamisha utendaji kazi wa jeshi hilo, lakini pia hatupendi wanahabari na
watetezi wengine wafanye kazi yao katika mazingira ya woga. Tunaamini kwamba
zipo njia muafaka zaidi za kushughulikia masuala yanayohusu taaluma ya habari.
Kwa mfano lipo Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo linajukumu ya kusuluhisha
migogoro inayohusiana na taaluma hiyo na iwapo itashindikana basi mhusika au
wahusika bado wanakuwa na nafasi ya kwenda mahakamani.
Kinachoshangaza ni
kuona kwamba Jeshi la Polisi limefikia mahali pa kwenda kuwakamata waandishi na
wahariri wa Tanzania Daima ndani ya
chumba chao habari na kuwakagua hadi katika makazi yao na kuchukua nyaraka
kadhaa kama ilivyotokea kwaa Bw. Josephat Isango.
Hali hiyo ya mahojiano
ya kushtukiza na kuogofya imefanyika pia kwa wahariri Charles Misango na Edson
Kamukara wote wa gazeti hilo, ambapo hatima yao bado haifahamiki mpaka sasa.
Hali hii inaweza kusababisha woga kwa wanataaluma wengine na hivyo kuleta
athari kubwa katika sekta ya habari nchini.
Hata hivyo waandishi
hao kwa sasa wanaishi kwa woga na kubadilisha vyombo vya usafiri pamoja na
makazi ya kulala. Je kwanini tufikie hatua hii ya kufanya wenzetu waishi kwa hofu kama suala kwenye mbuga iliiyojaa
simba.Je ulinzi wa vyombo vya usalama upo kwa ajili ya nani? Kwanini wengine
wauawe, watekwe, wateswe na kudhalilishwa
huku vyombo vya usalama vikichukulia ni jambo la kawaida na kutupiana
mpira?
Je nini Jeshi la
Polisi na Serikali kwa ujumla wamelifanya kuhusiana na kutekwa na kuteswa kwa
Dr Ulimboka zaidi ya Kulifungia Mwanahalisi ambalo lilijitoa mhanga kuchunguza
suala hili? Ndugu Kibanda katekwa na kufanyiwa kile kile alichofanyiwa Ulimboka,
Je tume iliyoundwa itaanzia kwa Ulimboka
ama itarukia moja kwa moja tukio hili ambalo ni muoendelezo wa matukio lukuki
dhidi ya watetezi wa haki na waandishi kwa ujumla.
Rai
Yetu
1. Tunawataka
watu wote wanaotumika au wanaoendeleza
wimbi la mashambulizi kwa wanahabari na watetezi wote wa haki za binadamu kwa
ujumla, waache kufanya hivyo kwani wataliingiza nchi katika machafuko makubwa.
2. Tunalisihi
Jeshi la Polisi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubeba jukumu
lao la kuhakikisha usalama wa watetezi wa haki za binadamu, na raia na watu
wote waliomo ndani ya mipaka ya nchi hii kwa ujumla bila ubaguzi.
3. Tunaomba
uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wahusika wa mtindo huu wa kuteka kutesa
na kutelekeza kwani tukio hili la Kibanda linashabihiana kwa kiwango kikubwa na
lile la Dkt Stephen Ulimboka.
4. Tunaiomba
jamii yote ya watu waliostaarabika, makundi mbalimbali kutuunga mkono katika
jitihada zetu la kupigania amani, haki na uhuru kwa watu wote hasa hasa
watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari.
5. Tunawakumbushia
waandishi wa habari kujitahidi kupata mafunzo ya usalama ambayo yanaratibiwa na
kutolewa na Mtandao huu wa watetezi.
6. Vyombo
vyote vya habari na waandishi kwa ujumla wazidi kuwa pamoja
katika kipindi hiki kigumu cha kuelekea chaguzi za serikali za mitaa mwakani
pamoja na uchaguzi mkuu 2015. Pia wajieupushe na makundi ya kisiasa ili
kujiweka vizuri katika kufanya kazi zao kwa kufuata misingi ya taaluma zao.
Mungu
Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeletwa
kwenu na
Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu Tanzania
(THRD-Coalition)
K.n.y Watetezi Wote wa Haki za
Binadamu Tanzania
Post a Comment