VIONGOZI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliovuliwa nyadhifa zao
hivi karibuni Dkt. Kitila Mkumbo na Zitto Kabwe wamesema kwamba njama
zilizotumika kuwavua madaraka ni mkakati wa viongozi wa juu wa chama
katika kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa chama unaotarajiwa
kufanyika mwishoni mwa mwaka huu. MOblog inaripoti.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo asubuhi jijini Dar es Salaam katika hoteli
ya Serena, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dkt. Kitila Mkumbo
amesema waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013
uliandaliwa na kuhaririwa na yeye kwa kuwa katika siasa za ushindani
kuandaaa mkakati wa ushindi si uhaini.
“siamini
hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha
siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa Chadema ni Demokrasia
na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa Demokrasia zaidi ya kuruhusu
ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa,”
amesema Dkt. Mkumbo
Amesema
kwamba viongozi wa juu wa Chadema wana hofu ya siasa za ushindani baada
ya kukaribia kwa uchaguzi mkuu ndani ya chama na yeye pamoja na Samson
Mwigamba wanaamini kwamba madadiliko ya uongozi wa juu wa chama ni
lazima.
Dkt.
Mkumbo aliendelea kusema kwamba mkakati kwa ajili ya uchaguzi iwe ndani
ya chama au nje ya chama ni haki ya kikatiba kwa sababu ni mkakati wa
uchaguzi hata viongozi wa juu wa sasa wa Chadema walikuwa na mkakati wao
katika kujiandaa na uchaguzi ndani ya chama.
“Siasa
za ushindania ndani ya chama cha siasa ni kujenga Demokrasia ya kweli
na kama chama kikuu cha upinzani kinakataa kujenga Demokrasia
kinachoililia kila siku kwenye chama tawala ni Udikteta usiokubalika
katika dunia ya leo,” alisisitiza Dkt. Mkumbo
Amesema
waraka wa Mkakati wa mabadiliko 2013 uliandaliwa na watu wanne tu bila
Zitto Kabwe kujulishwa ingawa alikuwa mlengwa mkuu wa mkakati ambapo
waandaji walipanga kumfuata na kumshawishi ajiunge.
Kwa
upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema kwamba
hatarajii kutoka ndani ya chama na hana mpango wa kuvunja chama chake
kilichomlea na kumkuza miaka nenda rudi kwa sababu yeye ni muumini
mwaminifu wa chama.
Amesema
kuwa cha kushangaza ni waraka wa siri uliomuhusisha yeye na viongozi wa
Chama cha Mapinduzi na wa Usalama wa Taifa kwamba anatumika kuhujumu
chama chake na waraka huo ulisambazwa na viongozi wa juu wa chadema kama
mkakati wao wa kumdhoofisha kisiasa kuelekea mbio za kugombea uongozi
katika uchaguzi wa chama mwishoni mwa mwaka huu.
Amesema
sababu ya pili ni kuwakosoa viongozi wa Chadema yakutokupeleka hesabu
za chama kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
kamati kuu ilidai alipaswa kuwatonya kwanza kabla ya kwenda kwa umma na
waandishi wa habari.
“dhamira
yangu ilikataa na nitaendelea kusimamia ukweli kwamba hesabu za vyama
vya siasa lazima zikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za
Serikali kama sheria inavyotaka,” amesema
Zitto
aliendelea kusema kuwa kama kuchagua kati ya chama na nchi yake
atachagua nchi kwanza kabla chama na kwamba ataendelea na msimamo wake
pia wa kukataa posho ya kukaa yaani (Sitting Allowance) kwa sababu
analipwa mshahara na fedha za kujikimu.
Mgogoro
ndani ya Chadema ulipamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi
Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi
akiandika barua ya kujiuzulu Ijumaa ya wiki hii.
Zitto
alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati
Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.
Taarifa
zilisema hoja ya kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa
kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika
uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi
ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali
ya kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14
wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki
na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye
Kamati ya Bunge.
Kujiuzuru kwa Arfi
Makamu
Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda
Mjini, Ijumaa ya wiki hii aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya
uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya
chama. Napenda ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura, wakazi na
wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika
kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika
barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa
kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa
katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa
kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka
uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na kulijadili katika
vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita
bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo,
lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila
kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki wa kupindukia.
Vilevile,
katika barua hiyo, Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa
chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha
mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei
kutuchagulia viongozi. Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo
wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu
uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama
kuwa mali binafsi.
Chanzo cha habari na www.dewjiblog.com.