JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA  

TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA

S. L.P. 4865,                                                                                                          
Dar es Salaam. 

Simu: 2150043-6/2150360   
Nukushi: (022) 2150047
Baruapepe: dgeneral@pccb.go.tz 
                                                                                                                   
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU ACHAGULIWA KUWA MAKAMU WA RAIS WA SHIRIKISHO LA TAASISI ZA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA DUNIANI

Wajumbe 460 wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani (International Association of Anti-Corruption Authorities – IAACA), kwa sauti moja wamemchagua Dkt. Edward G. Hoseah, Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU kuwa Makamu wa Rais wa shirikisho hilo.

Mkutano huo ambao umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 460 kutoka nchi mbalimbali duniani umefanyika nchini PANAMA – Amerika ya Kati kuanzia tarehe 22/11 – 24/11/2013. Wajumbe wa mkutano huu ni pamoja na Wakuu wa taasisi 98 za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani ambapo kauli mbiu ya mkutano huu ni “Utawala wa Sheria na Rushwa: Changamoto na Fursa Zilizopo”.

Dkt. Hoseah ambaye kabla ya kuchaguliwa kwake alikuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirikisho hilo, anakuwa Mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa katika tasnia ya mapambano dhidi ya rushwa duniani.

Uchaguzi huu ni heshima kubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.  Hii pia ni fursa nzuri kwa Tanzania kuonesha uwezo wake wa kuongoza mapambano dhidi ya rushwa kimataifa.

Nyadhifa nyingine za kimataifa ambazo Dkt. Hoseah anashikilia au aliwahi kushikilia ni pamoja na kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (2007-2008); Rais wa kwanza wa Jukwaa la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za SADC (SAFAC – 2010 - 2011) na Mwenyekiti wa Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri wa Masuala ya Rushwa (AU-ABC 2011-2012). Shirikisho la Kimataifa la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani ambalo linajumuisha Taasisi 298 pamoja na wanachama zaidi ya 2,000 kutoka katika Asasi mbalimbali zisizo za kiserikali, lilianzishwa Aprili 19, 2006 na Makao Makuu yake yapo Peking, China.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirikisho hilo ni kuziwezesha nchi wanachama kutekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 30, 2003.

Imetolewa na Doreen Kapwani, Afisa Uhusiano wa TAKUKURU, Panama. Novemba 26, 2013
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.