Roho ya mpendwa wetu Dk Edmund Sengondo Mvungi imetoweka duniani alasiri ya leo katika hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kupelekwa huko siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi ya afya yake kutokana na majeraha makubwa aliyoyapta kwa kuvamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Picture

Edmund Sengondo Mvungi (1952 - 2013)
Taarifa ya msiba huu imethibitishwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na ile iliyotolewa na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid (imepachikwa hapo chini).

Tume imewaomba Watanzania wote kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kuomboleza msiba huu.

Mtaalamu wa sheria, marehemu Dk Mvungi alikuwa pia Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alikuwa Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya  NCCR-Mageuzi.

Aliwahi kugombea kiti cha Urais wa Tanzania kupitia NCCR-Mageuzi mwaka 2005.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ametuma salaam za rambirambi ya kifo cha Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, akitoa pole kwa familia, uongozi na wanachama wa NCCR-Mageuzi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na wananchi wote walioguswa na msiba huo.

Akitoa kauli hiyo kwa niaba ya CHADEMA na wanachama wa chama hicho, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa amepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi, akimwelezea kuwa alikuwa mwanasiasa mwenye msimamo ambaye hakuwahi kutetereka kusimama na chama chake tangu alipojiunga nacho na kuanza kushiriki siasa za mageuzi nchini.

“Kwa niaba ya CHADEMA na wanachama wetu nchi nzima, napenda kutoa salaam za pole sana kwa familia ya marehemu, mjane na watoto. Natoa pole kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wanachama wa chama hicho, pia tunatoa pole kwa Jaji Mstaafu Joseph Warioba na makamishna wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwakifo cha Dkt. Mvungi. Tunaomba Mwenyezi Mungu awatie nguvu sana wakati huu wa majaribu na majonzi makubwa.

“Dkt. Mvungi alikuwa mwanasiasa mwenye misimamo ambaye hakuwahi kukihama chama chake tangu alipoanza siasa za mageuzi nchini. Ni kati ya wasomi wachache waliokuwa na ujasiri na kuthubutu kujiunga na vyama vya upinzani tangu mapema.

"Mvungi pia alikuwa mmoja wa wanasiasa wa mwanzo kabisa kupigania nchi yetu iwe na Katiba Mpya, ili hatimaye siasa zetu, hususan demokrasia ya vyama vingi nchini iendeshwe kwa misingi iliyo imara,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;

“Mwenyezi Mungu alimjalia marehemu akaweza kushiriki kutimiza ndoto hiyo baada ya kuteuliwa kuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Mpya, kazi ambayo ameifanya hadi siku alipokutwa na tukio lililosababisha mauti yake.”

Mwenyekiti Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, amesisitiza kuwa kwa namna ambavyo Dkt. Mvungi alikuwa mstari wa mbele katika suala hilo, Tume ya Katiba Mpya inao wajibu wa kuthamini mchango wake katika hatua iliyofikia sasa ya mchakato huo nyeti hadi utakapofika mwisho.

“Wakati tukimwombea marehemu kwa Mungu, alazwe mahali pema peponi, ni matumaini yetu kuwa serikali kupitia vyombo vyake itahakikisha kuwa wale wote waliohusika katika tukio la lililosababisha kukatisha uhai wa Dkt. Mvungi wanapatikana na kuchukuliwa hatua zote zinazostahili kisheria,” amesema Mwenyekiti Mbowe.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Dkt. Sengondo Mvungi Amefariki Dunia Leo nchini Afrika Kusini

Jumanne, Novemba 12, 2013

Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo (Jumanne, Novemba 12, 2013) saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.

Taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini kwa mazishi zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa.

Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.

Tume inawaomba watanzania wote kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dkt. Mvungi katika kuomboleza msiba huu.

Mwisho.

Imetolewa na:
Ndg. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
+255 757 500800

Source: http://www.wavuti.com
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.