MTANZANIA, Dar es Salaam --
KAMPUNI ya BAE System ya Uingereza, imekubali kuiuzia Tanzania kifaa
kipya cha rada ya kuongozea ndege iliyoharibika hivi karibuni. Taarifa
za kampuni hiyo kukubali kufanya biashara na Tanzania zimekuja baada ya
kuwepo taarifa, kwamba kampuni hiyo haiko tayari kufanya biashara na
Tanzania, ingawa ndiyo iliyoiuzia rada hiyo wakati wa awamu ya tatu ya
utawala wa Rais Benjamin Mkapa.
Akizungumza
na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA), Mhandisi Fadhili Manongi, alisema kuwa Agosti 20 mwaka huu,
alipokea barua kutoka Kampuni ya BAE ikiwaahidi kuwauzia kifaa kiitwacho
Power Supply Unit, kilichokuwa kimeharibika.
Alisema
kifaa hicho ambacho ni kwa ajili ya rada hiyo ya kuongozea ndege katika
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, kinanunuliwa kwa
gharama ya pauni 9,000 za Uingereza.
Mhandisi
Manongi alisema kutokana na barua hiyo kuwahakikishia kuuziwa kifaa
hicho, tayari mipango ya manunuzi inaendelea ili kifaa hicho kiweze
kununuliwa na kuletwa nchini haraka.
“Kifaa
cha rada kilichokuwa kimeharibika pale uwanja wa ndege tulikipeleka
Afrika Kusini ambapo Kampuni ya Tellumat imeweza kukitengeneza kwa
gharama ya Dola za Marekani 2,516 na kimerejeshwa nchini na kufungwa.
Hivi sasa hali ya uongozaji ndege imerejea kama ilivyokuwa awali na
tunaendelea kusubiri taratibu za ununuzi wa kifaa kipya kutoka Kampuni
ya BAE, napenda kuwahakikishia Watanzania wote, kwamba anga ya Tanzania
ni shwari. Unajua watu wengi hawafahamu rada yetu inaongoza ndege hadi
nje ya nchi, rada hii inaongoza ndege za Burundi na Rwanda ambapo sasa
ufanisi katika kazi umeongezeka na hakuna athari zilizojitokeza wakati
kifaa hicho kikiwa kibovu,” alisema.
Manongi
alisema Tanzania na Uingereza zina uhusiano mzuri, licha ya kuwapo
mvutano wa urudishaji wa chenji ya rada hiyo baada ya kubainika taratibu
na sheria hazikufuatwa katika ununuzi, hali iliyosababisha Serikali ya
Uingereza kuitaka Tanzania kuwafikisha waliohusika mahakamani.
Alisema
kwamba, wakati kifaa hicho kilipokuwa kimeharibika, wafanyakazi wa TCAA
walikuwa makini kuongoza na kuhakikisha abiria wanakuwa salama katika
safari zao, ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa ndege mara kwa mara.
Aliongeza
kwamba kuharibika kwa kifaa hicho kumetoa somo kwa TCAA kujiandaa kuwa
na akiba ya vifaa vya rada, ili kuwa na uhakika katika shughuli zao.
Agosti
17, mwaka huu, Mhandisi Manongi alitoa taarifa kwenye vyombo vya
habari, kwamba kifaa cha Power Supply Unit cha rada iliyoko JNIA,
kimeharibika na kwamba wakati huo ndege zilikuwa zinaongozwa kwa simu na
redio.
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka
Kampuni ya BAE kwa pauni za Uingereza milioni 29.5, sawa na Sh bilioni
70 za Tanzania. Hata hivyo ilibainika kwamba, mchakato uliotumika
kuinunua haukuzingatia taratibu na sheria, kitendo kilichosababisha
mvutano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo.
Post a Comment