Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewaachia huru
wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliokuwa
wakikabiliwa kwa pamoja na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali
tarehe Novemba 11 mwaka 2011, eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kusababisha uvunjifu wa amani eneo la chuo hicho.
Wanafunzi
hao waliachiwa jana na Hakimu Walialwande Lema aliyekuwa akisikiliza
kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka ulioongozwa na Wakili wa
Serikali, Ladslaus Komanya kushindwa kuleta mashahidi mahakamani huku
wakitoa sababu mbalimbali. Komanya alidai kuwa washtakiwa hao wakiwa
kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi
la Polisi waliwataka watawanyike, lakini hata hivyo wanafunzi hao
walikaidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hata
hivyo washitakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo chini ya
ulinzi mkali wa jeshi la polisi, walikana mashtaka hayo na waliachiwa
huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja
wa kuaminika ambaye alisaini bondi ya Shilingi milioni moja.
Baada ya kuachwa huru, wanafunzi hao waliondoka mahakamani hapo kwa furaha huku wakikumbatiana na wengine wakisali.
Akitoa
uamuzi huo jana, Hakimu Lema alisema kuwa anatupilia mbali maombi ya
upande wa mashitaka yaliyokuwa yakiomba ahirisho la kesi hiyo kwa mara
nyingine wakidai kuwa mashahidi wao ambao ni askari wako katika Sensa ya
Watu na Makazi.
Lema
alisema kuwa sensa ni muhimu kama ilivyo kesi hiyo, lakini maombi yao
hayakufuata taratibu za sheria ambapo kwa mujibu wa kifungu cha sheria
cha 225 (4) Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), sura ya 20
kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.
“Agosti
13 mwaka huu kulikuwa na ahirisho ambapo sababu ilikuwa hakuna
mashahidi kwa sababu wako katika mgomo wa madaktari, leo tena mnaleta
sababu kuwa wako katika sensa inaonesha mmedharau amri ya Mahakama,”
alisema Hakimu.
Alisema
amri ya mwisho aliyoitoa ilikuwa ahirisho la Agosti 13 mwaka huu hivyo
upande wa mashitaka umedharau amri ya Mahakama na kwa maana hiyo
anawaachia huru washitakiwa wote chini ya kifungu cha sheria ya Mwenendo
wa makosa ya jinai kifungu cha 225 (5) sura ya 20.
Awali
wakili wa upande wa mashitaka, Prosper Mwangamila alidai kuwa kesi
ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa akaomba iahirishwe hadi Jumatatu.
Wakili wa washitakiwa hao, Reginard Martin akijibu hoja hiyo aliiomba
Mahakama kutokubali ombi hilo na badala yake kesi ifutwe washitakiwa
waachiwe huru.
Baadhi ya majina ya wanafunzi walioachwa huru
ni Mwambapa Elias, Evarist Ambrose, Baraka Monas, Hellen Moshi, Alphonce
Lusako, Matrona Babu, Rolanda Wilfred, Godfrey Deogratius, Moris Denis
and Evon Gumbi.Others are Lugiko Mathias, Ndimbo Jabir, Evarist Wilson,
Cornel Rwaga Mushi, Mlazi Kumbuka, Rehema Munuo, Glory Masawe, Happy
Amulike, Elias Mpangala, Frida Timothy, Stella Mofe, Betwel Martin,
Mmasi Stephen na Lugemalila Venance na wengineo.
Post a Comment