ZANZIBAR IJUMAA AGOSTI 24, 2012
 Wavuvi wawili Raia wa Komoro, wamekutwa katika Kisiwa Kidogo cha Pungume nje kidogo ya Zanzibar wakiwa hoi kwa uchovu na njaa baada ya kupotea na kuishi baharini kwa muda wa siku 11 bila ya chakula.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar Kamishna Msaidizi ACP Yusufu Ilembo, amewataja wavuvi hao kuwa ni Othman Inzudin(24) na Nurdin Ahmed(18) ambao wote ni Raia wa Komboro.

Amesema kuwa wavuvi hao wakiwa na boti ndogo katika shughuli zao za uvuvi huko nchini Komoro, walipatwa na misukosuko ya mawimbi na upepo mkali na kupotea baharini hadi boti yao kuishiwa mafuta.

Amesema kutokana na hali hiyo, vijana hao walijikuta wakiishi majini kwa muda mrefu bila ya chakula wakinywa maji chumvi ya bahari huku wakienda kwa kufuata mwelekeo wa upepo na mawimbi ya bahari hadi walipohika katika kisiwa hicho cha Pungume kilichopo kusini mwa Zanzibar.

Amesema vijana hao wamelazimika kufungua ingini ya boti yao na kuitosa majini kama njia ya kuifanya boti yao kuwa nyepesi ili isukumwe na mawimbi kwa urahisi na kuweza kutokea nchi kavu kunuusuuru maisha yao.

Hata hivyo Kamanda Ilembo amesema kuwa baada ya kuokolewa, wavuvi hao walipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu.

Lakini amesema kwa bahati mbaya Nurdin Ahmed alipoteza maisha wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.

Amesema Jeshi la Polisi limewasiliana na ubalozi wa Komoro hapa nchini ili kuona uwezekano wa kumsafirisha kijana mmoja aliyebaki pamoja na mwili wa marehemu hadi nchini kwao Komoro ambako zitafanyika taratibu za mazishi.

Nao Madaktari na Wauguzi wa zamu katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Dk. Mohammed Hassan Haji na Dk. Mkasi Khatib Makame, wamesema jambo lililosababisha kifo cha kijana huyo ni uchovu, njaa na hali ya kukata tama kwa wasiwasi.

Hata hivyo Wauguzi hao wamesema kuwa hali ya kijana mmoja aliyebaki wodini hapo inaendelea vizuri baada ya matibabu ikiwa ni pamoja na kumuongezea maji mwilini na kupatiwa chakula ili kurudisha nguvu mwilini. 

Mwisho

 Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.