KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni nzito, hivyo anajipanga kuijibu.

Dk Slaa aliliambia gazeti hili jana kuwa asingependa kuzungumzia kauli hiyo sasa kwa kuwa yuko ziarani vijijini, lakini ataitolea tamko wakati mwafaka ukifika.Habari ambazo baadaye gazeti hili lilizitapa zinasema kuwa Dk Slaa huenda akamjibu Sitta leo, atakapokutana na waandishi wa habari mjini Iringa.

Dk Slaa mwenyewe jana jioni alithibitisha kwamba atakutana na waandishi wa habari leo mjini Iringa, lakini hakuwa tayari kueleza kama atazungumzia kauli ya Sitta au la.

Kauli ya Dk Slaa imekuja baada ya gazeti hili kumtaka azungumzie kauli ya Sitta kuwa muda wa Chadema kutawala nchi bado, kwa kuwa chama hicho hakina viongozi makini wa kufanya kazi za Serikali.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana Dk Slaa alisema,"Nimemsikia, lakini sijamwelewa. Naomba nipate muda wa kusoma vizuri alichosema, halafu nitamjibu tu."

Aliendelea:"Mimi sasa nipo huku Mufindi, sina mawasiliano yoyote ya msingi, naomba nipate muda zaidi wa kujiridhisha maneno yake kabla sijamjibu, nikiwa tayari nitawajulisha (waandishi).”

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza na gazeti hili jana alisema mkutano wa Dk Slaa na waandishi wa habari utalenga kueleza jinsi Chadema kinavyoendesha Operesheni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), baada ya kuzuiwa kwa mikutano yake ya hadhara.

“Kwenye mkutano na wanahabari, mambo mengi yanaweza kutokea. Kwa hiyo siwezi kukujibu moja kwa moja kama hilo unaloulizia (kauli ya Sitta) nalo litajibiwa au la,”alisema Makene. 


Sitta alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera juzi, alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi ya Chadema, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake wana baadhi ya watu wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki.

Sitta alisema ukimwondoa Dk Slaa, hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza na kukifanya chama hicho kikubalike kwa umma.

“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanae Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri,” alisema Siita na kuongeza:

“Wote hapa mnasikiaga kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”


Kuhusu M4C

Katika hatua nyingine, Dk Slaa alizungumzia Operesheni inayojulikana kama M4C akisema Chadema imewabwaga polisi, kutokana na chama hicho sasa kubuni mbinu nyingine ya kujiendesha.

"Tuko huko Mufindi tunajenga chama, vikao kila wakati," alisema Dk Slaa alipoulizwa yuko wapi na anafanya nini.

Dk Slaa alisema CCM na Serikali yake, itajuta kuzuia mikutano ya hadhara ya Chadema kwani baada ya uamuzi huo, chama hicho kimekuja na njia nyingine ya kujijenga maeneo ya vijijini.

"Hawa watajuta (CCM na Serikali) kuzuia mikutano yetu. Sisi tumekuja na njia nyingine ya kukijenga chama vijijini," alisema Dk Slaa ambaye hata hivyo, hakubainisha njia gani anayotumia sasa kukijenga chama hicho cha upinzani.

Alipoulizwa atamaliza lini ziara yake hiyo ya kukijenga chama kwa njia mbadala, alijibu," Tulipanga kutumia siku 44 katika mikoa mitano, lakini nadhani siku hizo zitaongezeka baada ya mikutano yetu kuzuiwa.”

Mwanzoni mwa mwezi huu, Chadema kilianza ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini katika kile wanachokiita Movement for Change (M4C).

Hata hivyo, wakiwa mkoani Morogoro, chama hicho kiliingia katika mgongano na polisi katika vurugu zilizosababisha kifo cha mfuasi wake mmoja na majeruhi wawili.

Baadaye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Said Mwema aliipiga marufuku mikutano na maandamano ya chama hicho iliyopangwa kufanyika mkoani Iringa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupisha Sensa ya Watu na Makazi.



chanzo Mwananchi
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.