Inahuzunisha lakini kuna fundisho kuu kwetu sote.
“Nilipofika nyumbani usiku ule, mke wangu aliponitayarishia
chakula, nilimshika mkono na kumwambia, Kuna kitu nataka nikwambie. Mke wangu
alikaa chini na kula chakula kimya akiwa tayari kunisikiliza. Tena nikagundua
macho yake yalionyesha anaumizwa. Nilishindwa hata namna ya kuanza kufumbua
kinywa changu. Lakini ilibidi nimwambie ili ajue nilikuwa nikifikiri nini juu
yake.
Nataka kukupa talaka. Nilianza kusema kwa utulivu.
Alionekana kutokereka na maneno yangu badala yake aliniuliza kwa sauti ya upole
‘kwa nini?’ Sikumjibu swali lake. Kutojibu kulimfanya akasirike. Akatupa kijiko
na akanikaripia, ‘wewe si mwanamume!’ Usiku ule, hakukuwa na maongezi kati
yetu. Alikuwa akilia kwa kwikwi. Nilifahamu kwamba alitaka kujua ni nini
kimetokea kwenye ndoa yetu. Lakini kwa hakika nisingeweza kumpa jibu wala
sababu ya kuridhisha; alionekana si mali kitu kwangu penzi langu lilihamia kwa
Jane. Sikumpenda tena mke wangu mawazo yote yalikuwa kwa Jane. Kwa kweli
nilimdharau mke wangu!
Huku moyo wangu ukijua wazi kwamba nafanya kosa, niliandika
talaka ambayo ilionyesha kwamba yeye (mke wangu) angepata nyumba yetu, gari na
atakuwa na hisa 30% ya kampuni yetu. Aliangalia talaka ile na kuichana vipande
vipande.
Mke ambaye tumeishi nami kwa miaka 10 alionekana mgeni
machoni mwangu. Nilimuonea huruma kwa muda, rasilimali na nguvu alizopoteza
lakini sikuweza kurudi nyuma kwa sababu Jane aliuteka moyo wangu kisawasawa.
Hatimaye mke wangu alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo kwa hakika
nilitarajia. Kwangu mimi kilio chake kilinipa nafuu.
Wazo la kuachana na mke wangu limenisumbua kwa majuma kadhaa
na sasa limeendelea kuimarika na kuwa jambo la hakika zaidi.
Siku iliyofuata nilikuja nyumbani kwa kuchelewa sana
nikakuta mke wangu akiandika jambo mezani. Sikutamani hata kula chakula
alichonipikia nilikwenda moja kwa moja chumbani na usingizi ulinichukua mara
moja kwa sababu nilikuwa nimechoka baada ya kula raha za kufa mtu na Jane.
Usiku nilishtuka usingizini mke wangu alikuwa bado akiandika.
Sikujali kabisa nikajifunika vyema shuka na kulala tena. Asubuhi yake
alinikabidhi masharti ya talaka yake: hakutaka kitu chochote kutoka kwangu
lakini alihitaji apate angalau mwezi mmoja wa kujiandaa kabla hajaachika.
Akaomba kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja sote mimi na yeye
tujitahidi kuishi maisha ya upendo au kawaida kwa kadiri itakavyowezekana.
Sababu yake ilikuwa ndogo lakini muhimu: mwanetu wa kiume alikuwa akikaribia
kufanya mtihani katika mwezi uliofuata kwa hiyo hakupenda mtoto aathirike
kisaikolojia kwa sababu ya kuachana kwetu. Hili halikuwa tatizo kwangu,
nilikubali mpango wake. Lakini alikuwa na sharti la ziada, aliniomba nikumbuke
jinsi nilivyombeba siku za fungate yetu hasa siku ya harusi yetu. Akaniomba na
kunisihi kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja niwe nambeba kutoka
kitandani kwetu mpaka mlango wa kutokea kila asubuhi. Nilidhani anakaribia kuwa
kichaa. Ili kufanya siku zetu za mwisho zisiwe na migogoro nilikubaliana na
masharti yake ya ajabu.
Nilimsimulia Jane kuhusu masharti ya kuachana na mke wangu.
Jane alicheka sana, aliona ni ujinga. ‘Hata akitumia ujanja wa namna gani
talaka ni lazima’, alisema Jane tena kwa dharau. Mimi na mke wangu hatukuwahi
kugusana tangu nilipomweleza dhamira ya kumtaliki. Kwa hiyo nilipombeba kwa
mara ya kwanza sote tulinuniana. Mwanetu alifurahi sana na kupiga makofi nyuma
yetu, ‘aah baba kambeba mama mikononi mwake’. Maneno yake yalinichoma moyoni
moja kwa moja. Kutoka chumbani kwetu hadi sebuleni, halafu tena mpaka mlangoni,
ni zaidi ya mita kumi nimembeba mke wangu. Alifumba macho na kusema kwa sauti
laini na ya upole; usimwambie mwanetu juu ya talaka. Nilikubali kwa kichwa,
ingawa nilijisikia vibaya. Nilimuweka chini nje ya nyumba.
Alienda kituoni kusubiri basi la kazini kwake nami
nikaendesha gari kwenda ofisini kwangu. Siku ya pili, zoezi lilikuwa rahisi
kwetu sote. Aliegemea kifuani pangu. Nilisikia harufu nzuri ya uturi aliofukiza
kwenye blauzi yake. Nikagundua kwamba sijamuangalia kwa makini mke wangu kwa
kipindi kirefu sana. Nikagundua hakuwa binti tena. Kulikuwa na mikunjo usoni na
nywele zake zilianza kuwa nyeupe! Ndoa yetu imekula urembo wake. Kwa dakika
moja nikafikiri kwa nini namfanyia hivi.
Siku ya nne nilipombeba hisia za mapenzi kati yetu
zilirejea. Huyu ni mwanamke aliyejitoa kuishi nami na tumeishi kwa miaka kumi
sasa. Siku ya tano na ya sita ilikuwa wazi kwamba mapenzi yetu yalikuwa yakimea
upya. Sikumwambia Jane kuhusu jambo hili. Kadiri mwezi ulivyokaribia kwisha
niliona raha kumbeba mke wangu na zoezi likawa rahisi zaidi. Pengine kufanya
kazi hii kila siku kuliniimarisha zaidi.
Alikuwa akichagua nini cha kuvaa asubuhi. Alichagua mavazi
kadhaa hakupata linalomfaa. Kisha akaguna, ‘nguo zangu zote zimekuwa kubwa’.
Nikagundua kwamba mke wangu amepungua sana, nadhani ndiyo maana niliweza
kumbeba kirahisi. Ghafla jambo likanichoma… mke wangu ana uchungu na maumivu
makuu moyoni mwake. Bila kujitambua nikamgusa kichwa chake. Mara mtoto wetu
akatokeza na kusema ‘baba ni wakati wa kumbeba mama muende kazini’. Kwake
kumuona baba akimbeba mama likawa ni jambo la furaha sana. Mke wangu
alimuonyesha ishara mwanetu asogee karibu na akamkumbatia kwa upendo mkuu.
Niligeuza uso wangu nisije nikabadili mawazo katika dakika ya mwisho. Kisha
nikambeba mikononi mwangu kutoka chumbani, sebuleni halafu mpaka mlangoni.
Mkono wake laini ulikuwa umeizunguka shingo yangu kwa upendo. Nilimkumbatia
mwili wake; ilikuwa ni mithili ya siku ya ndoa yetu. Lakini wepesi wake
ulinitia mashaka.
Siku ya mwisho nilipombeba nilipata shida hata kupiga hatua moja.
Mtoto wetu alishakwenda shuleni. Nilimshika kwa karibu na kumwambia sikubaini
kwamba maisha yetu yalikosa upendo. Nikaenda zangu ofisini…. Nikashuka garini
hata bila kufunga mlango. Maana nilihisi nikichelewa tu ninaweza kubadili
nilichoamua…. nikapand ngazi. Jane alifungua mlango nikamwambia, ‘Samahani,
Jane, sihitaji tena kumtaliki mke wangu’. Akaniangalia kwa kustaajabu, halafu
akagusa kichwa changu. Akaniuliza ‘Unaumwa?’ Nikaondoa mkono wake kichwani
kwangu. ‘Samahani, Jane, nimesema sitaki kumtaliki mke wangu. Nadhani ndoa
yangu haikuwa na furaha kwa sababu sikuthamini undani wa maisha yetu, mimi na
mke wangu, si kwamba hatupendani. Nimetambua hilo tangu nilipombeba siku ya
ndoa yetu nilitakiwa kumbeba siku zote za maisha yetu, nampenda mke wangu sitamuacha
mpaka kifo kitakapotutenganisha.’
Ikawa kama Jane alizinduka usingizini. Akanizaba kibao cha
nguvu, akajiegemeza mlangoni na kuanza kulia. Nikashuka ngazi na kuondoka
zangu. Nikaingia kwenye duka la maua nikaagiza maua mengi mazuri kwa ajili ya mke
wangu. Muuzaji akaniuliza aandike nini kwenye kadi. Nikatabasamu na kuandika
“Nitakubeba kila asubuhi mke wangu mpaka kifo kitakapotutenganisha”. Jioni ile
nilifika nyumbani na maua mikononi mwangu, tabasamu kubwa usoni nikakimbia
mpaka chumbani, nikapokelewa na maiti ya mke wangu kitandani.
Kumbe mke wangu alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa miezi
kadhaa nami nilishindwa kubaini kwa sababu nilihamishia akili yangu kwa Jane.
Alijua kwamba angekufa karibuni na alitaka asiniingize katika chuki na mwanetu
kama ningelazimisha talaka mapema.
Angalau machoni mwa mwanangu naonekana ni mume mwema….
Jamani vitu vidogo vidogo vizuri ni vya msingi sana katika
mahusiano yetu… Siyo majumba au magari au fedha zilizoko kwenye benki. Hivi
vitakupa tu mazingira ya kufurahi lakini vyenyewe siyo furaha. Kwa hiyo
jitahidi kuwa na muda mzuri na mazingira rafiki ya kuwa na mwenzi wako, kuwa
rafiki wa mwenzi wako. Fanya vitu mlivyofanya wakati wa uchumba na wa ndoa
yenue ambavyo vitawaweka karibu siku zote. Muwe na ndoa yenye furaha. Mara
nyingi watu hushindwa katika ndoa kwa kutotambua ni kwa kiasi gani walikuwa
karibu wakati wa kujenga uhusiano wao
Mungu awabariki nyote mliosoma na kujifunza hapa.
–Ntwa Ntumwalisa
Post a Comment