TAMKO LA FEMACT KUHUSU VURUGU ZILIZOTOKEA KATIKA MDAHALO KUHUSU KATIBA PENDEKEZWA KATIKA HOTEL YA BLUE PEARL UBUNGO DAR ES SALAAM TAREHE 2 NOVEMBER 2014
Sisi Mashirika yapatayo 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Demokrasia, Utawala bora, Maendeleo na Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi (FEMACT) tumekuwa tukifuatilia kwa karibu mchakato wa katiba unavyokwenda tangu ulipoanza pamoja na changamoto zinazojitokeza bado kuna fursa ambazo wananchi wameweza kushirikishwa na kutia matumaini ya kupata katiba mpya.
Jambo la kusikitisha ni kwamba wakati mchakato ukikaribia mwisho kumeanza kujitokeza matukio ya aibu naya kusikitisha ambayo yanaweza kuuchafua kabisa au kuharibu kazi nzuri ambayo ilikuwa imeanza kufanyika.
FemAct imesikitishwa na vurugu za hivi karibuni zilizosababisha kukatishwa kwa mdahalo wa kujadili mchakato wa katiba mpya ya Tanzania huku baadhi ya watu wakipigwa na kujeruhiwa akiwemo mwandishi wa habari wa BBC aliyeumizwa, mwanamke moja aliyepigwa na kuangushwa pamoja na kuzingirwa kwa mlemavu wa macho aliyekuwa akishiriki katika mjadala huo.
Mdahalo huo uliokuwa ukirushwa moja kwamoja na redio na televisheni ulivurugika kutokana na kundi la vijana kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha hoja zake.
Zomeazomea hiyo ilifuatiwa na vurugu ambazo zilisababisha mtafaruku na bugdha kubwa kwa washiriki wa mjadala huo.
Hali hii ni tishio kwa uhuru na haki kwa wananchi kujieleza, kutoa maoni na kujumuika katika kujadili masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa nchi yao. FEMACT kama muungano wa mashirika na asasi mbalimbali za kiraiya, inalaani vikali vurugu hizo kwani zinaweza kusababisha machafuko nchini hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na mchakato wa kura ya maoni ya katiba pendekezwa.
Vurugu kama hizo zinaweza kuwa tishio kwa wananchi hasa makundi yaliyoko pemebezoni, wakiwemo wanawake, wazee, walemavu na makundi mengineyo.
Ni dhahiri kuwa, makundi hayo na watanzania kwa ujumla watakuwa na hofu ya kushiriki katika kujadili katiba pendekezwa ambayo ni mustakabali wa nchi yao.
Hii inaweza kusababisha watu au makundi yanayopenda kushiriki katika kujadili katiba pendekezwa kutojitokeza tena kwa hofu ya kufanyiwa fujo.
Aidha, kuhusu kufanyiwa fujo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jani mstaafu Joseph Warioba, na watu wengine akiwemo mwanamke na mlemavu wa macho waliokuwa wanashiriki katika mjadala huo, kitendo hicho ni cha kidhalilishaji kinacholenga kufifisha maoni ya wananchi.
FEMACT kama watetezi wa haki za kijamii inaamini kuwa mtu yeyoye ana uhuru wa kutoa maoni yake na kusikilizwa na watu wengine bila kufanyiwa vurugu, kudhalilishwa au kudhuriwa kwa namna yoyote.
Hofu yetu ni kwamba matukio kama haya yanawatisha wanawake na walemavu kushiriki hatua zinazofuata kama uchaguzi wa serikali za mitaa, kura za maoni na uchaguzi mkuu 2015 kikamilifu kwa sababu watahofia kufanyiwa vurugu.
Kwa takribani miaka 10 iliyopita tumeshuhudia idadi ya wapiga kura nchini ikizidi kushuka badala ya kuongezeka licha ya kuwa idadi ya watu nchini kuongezeka, sababu kama hizi za kuvuruga mikusanyiko ya wananchi, mikutano ambayo wananchi wanapashana taarifa inafifisha ari ya wananchi kujitokeza.
Ili kuhakikisha mchakato huu unafanyika katika hali stahiki, na wananchi kushiriki kikamilifu chaguzi zinazokuja FEMACT inapendekeza yafuatayo;
1. Uhuru wa kujieleza na kutoa maoni uheshimiwe katika kujadili mambo yanayohusu mustakabali wan chi yao ikiwemo katiba pendekezwa na makundi yote yakiwemo yaliyoko pembezoni yapewe nafasi na kuhakikishiwa usalama.
2. Vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa, usalama unakuwepo kwa wananchi wakati wanaposhiriki katika mchakato wa kujadili na kupiga kura ya maoni ya katiba pendekezwa pamoja na chaguzi zijazo.
3. Vijana ambao ni zaidi ya asilimia 65% ya idadi ya watu nchini, waepuke kutumiwa na watu binafsi, vyama vya siasa au makundi fulani katika jamii ili kuepukana na kuharibika kwa hali ya usalama katika nchi yetu.
4. Vyama vya siasa au makundi yoyote kuacha mara moja kushiriki katika vitendo vya kiuchochezi au vinavyoweza kusababisha vurugu katika nchi yetu.
5. Wananchi waachwe wajadili kwa mapana maudhui ya Katiba Pendekezi bila kuwekewa mipaka au ukomo ili waielewe kabla ya kushiriki upigaji kura kama ilivyopendekezwa.
Imetolewa na
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji -TGNP Mtandao
Kny Sekretarieti ya FemAct
Post a Comment