Dar es Salaam. Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM),
Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni alinusurika kifo akidaiwa kulishwa
sumu akiwa London, Uingereza amesimulia jinsi tukio hilo lilivyomkuta.
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi |
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkono
alisema endapo uchunguzi wa suala hilo utakamilika na kuthibitisha
kwamba alilishwa sumu, atapambana na wahusika kwa kuwa wamehatarisha
maisha yake.
Mkono ambaye pia ni wakili maarufu nchini, alitoa
kauli hizo jijini hapa jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari kuelezea mwenendo wa afya yake.
Alidai kwamba, lengo la kumlisha sumu ni kuharibu figo zake ndani ya saa 72 wakati alipokuwa katika ziara ya nchini humo.
“Niko vizuri na afya njema… kama kuna mtu anawinda
jimbo langu mwambieni ameshindwa na wananchi wangu nawaeleza kuwa niko
salama wasiwe na hofu. Ninataka kujua nani kanilisha sumu na kwa nini?”
alisema Mkono.
Akisimulia tukio hilo alisema, Novemba 11 akiwa
miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
walisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Uingereza akiwa salama salimini.
Aliwataja baadhi ya wabunge walioambatana nao kuwa
ni William Ngeleja (Mwenyekiti wa kamati hiyo), Mbunge wa Temeke, Abbas
Mtemvu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utawala Bora), George Mkuchika.
“Tukiwa uwanja wa ndege nilipokea ujumbe mfupi wa
maandishi (hakutaka kuuweka wazi kwa sababu upelelezi haujakamilika),
ukinitahadharisha kuwa makini, ujumbe ule ulinishtua kwa kweli.”
“Niliwaonyesha wenzangu niliokuwa nao na pale
tulikunywa chai kabla ya kuondoka na tulipofika kule mimi nilikaa hoteli
yangu na wenzangu wakakaa ya kwao,” alisema.
Huku akisimama na kunyoosha mikono kuonyesha yuko
vizuri, Mkono alisema siku iliyofuata ratiba iliwataka kuhudhuria Bunge
la Uingereza.
“Niliamka na kwenda Ubalozi wetu na kwa kuwa
tulitakiwa kufika bungeni saa 5.00 asubuhi, niliwahi na wenzangu na
walipokuja tuliungana… tulipokuwa ndani katika Bunge la Uingereza,
ghafla nilianza kujisikia vibaya hali iliyonisababisha nipoteze fahamu
kwa saa sita. “Lakini kabla ya kupoteza fahamu niliwaeleza wanipeleke
nyumbani (Tanzania), wenzangu wanasema nilikuwa napiga kelele,
nirudisheni hawa wanataka kuniua,” alisema Mkono kwa sauti ya chini na
kuongeza:
“Hapa nasimuliwa sasa kuwa walinipeleka
hospitalini na waliponifikisha madaktari wa pale waliamua kuwasiliana
kwanza na Daktari wangu, (Lusangulila Kapitain) ili kujua kama wakati
natoka Tanzania nilikuwa na tatizo.”
Alisema, “Kapitain baada ya kuelezwa hali niliyonayo naye aliwaeleza kuwa huyo (Mkono) atakuwa amelishwa sumu kwani wakati anatoka huku alikuwa salama kabisa na akawaomba wanipatie dawa ambazo zilinirejesha katika hali yangu ya kawaida kuanzia saa 12 hadi saa moja jioni.”
Alisema, “Kapitain baada ya kuelezwa hali niliyonayo naye aliwaeleza kuwa huyo (Mkono) atakuwa amelishwa sumu kwani wakati anatoka huku alikuwa salama kabisa na akawaomba wanipatie dawa ambazo zilinirejesha katika hali yangu ya kawaida kuanzia saa 12 hadi saa moja jioni.”
Mkono alisema kitu ambacho hadi sasa hajakielewa
na anapenda kukifahamu ni kwa nini na malengo yapi akisema kama ni
sakata la escrow lilikuwa wazi bila kificho.
“Serikali ilikuwa ni mteja wangu katika kesi kati
ya Tanesco na IPTL… nikiwa bungeni siwezi kuongea hadi nipate kibali cha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana na maadili ya kazi zetu, lakini
uchunguzi ukibainika kwamba nililishwa sumu kwa sababu hiyo nitaweka
kando maadili ya kazi.”
chanzo cha habri na gazeti la www.mwananchi.co.tz
chanzo cha habri na gazeti la www.mwananchi.co.tz
Post a Comment