Nami najaribu kuyapa maana machungu yaliyomo kwenye kashfa ya Tegeta Escrow Account, ambayo – kwa sababu ya mfumo – sisi Wazanzibari hatujioni kuguswa nayo. “Baada ya yote, hizo si ni pesa za TANESCO, ambalo ni shirika la umeme la Bara. Linatuhusu nini sisi tunaoelea kwenye visiwa vya Bahari ya Hindi?“ Ndivyo wenzangu wengi wanavyodhani.
Lakini hili linatuhusu, kwa pande na rangi zake zote. Kwanza, na kubwa kuliko yote, ni kwamba bado tunabakia kuwa Watanzania – kwa sheria na kwa kodi tunayolipa. Hata kama tupo ambao utiifu wetu kwa huo Utanzania ni mdogo sana na tunajinasibisha zaidi na utiifu kwa Uzanzibari, ambao hauna jeshi, mizinga wala jela.
Pili, ingawa sijui ni wangapi miongoni mwa wanaoshukiwa kujipatia manoti hayo ya TANESCO ni Wazanzibari, lakini nafahamu kuwa Waziri wa Fedha Saada Salum Mkuya ni Mzanzibari na sasa anatakiwa awajibike kwa kuzembea kwake kusimamia fedha za wananchi. Namuhurumia Da Saada, mwalimu mwenzangu wa muda wa ziada pale kwenye kituo cha Ruec Center, Mlandege.
La tatu, na ndilo ninalokusudia hasa, ni kuwa juu ya uwazi wa kashfa hii ambao hautugusi Wazanzibari, kuna uficho wake ambao unatuhusu sana – ambao unahusiana na siasa za Muungano kuelekea Zanzibar.
Unakumbuka kuwa Alhamisi iliyopita ya tarehe 20 Novemba, wabunge kadhaa kutoka upinzani na kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) walisimama bungeni Alhamisi iliyopita (20 Novemba) kuhoji kile walichosema ni barua ya mahakama kuzuia mjadala wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Moja ya hoja iliyorejewa takribani na wote, akiwamo Naibu Spika Job Ndugai, ni kwamba kumekuwa na tabia ya mahakama kutumika kwa maslahi ya kifisadi nchini Tanzania. Kwamba vita dhidi ya ufisadi vimekuwa vigumu kwa kuwa chombo kinachopaswa kusimamia utekelezwaji wa sheria zinazopitishwa na bunge, nacho kimevamiwa na mafisadi. Kwa hakika, katika orodha ya waliopokea fedha za akaunti hiyo ya Tegeta Escrow ni pamoja na majaji wa ngazi za juu.
Kama nilivyosema, suala zima la kashfa hii ni shari lakini ndani yake inaweza ikazalika kheri, hasa kwetu Wazanzibari. Kwa nini? Kwa kuwa hili linatupa hoja ya kuhoji uadilifu wa mahakama za Tanzania Bara, ambako hivi sasa Wazanzibari wenzetu wamekuwa wakipelekwa kushitakiwa kwa makosa ya ugaidi.
Ni sisi wenyewe raia wa kulisemea na kulifanyia kazi hili, na tusitegemee serikali, maana kiongozi wake mkuu, Rais Ali Mohamed Shein, ameshasema wazi kwake hilo ni sawa tu. Sisi kwetu si sawa. Halikuwa sawa tangu awali. Awali tulilipinga kwa kuhoji uhalali wa kisheria wa kuwachukuwa Wazanzibari wanaotuhumiwa kufanya makosa ndani ya ardhi ya Zanzibar yenye mamlaka yake tafauti kisheria na kuwapeleka na kuwafungulia mashitaka Bara kwenye mamlaka nyengine ya kisheria.
Sasa tuna hoja ya ziada. Hii inahusu kuhojika kwa uaminifu na uadilifu wa mahakama hizo, ambazo tayari Bunge limeambiwa kuwa ni vichaka vya mafisadi. Hoja yetu ni kuwa kamwe mahakama hizi haziwezi kuaminika kuendesha kesi inayowahusu washukiwa ambao tangu hapo kesi yao ni ya kisiasa zaidi kuliko ya kisheria. Mahakama ambazo kesi zake huendeshwa kwanza kwenye vikao vya baa, vyumba vya hoteli au ofisi za mabwana walio nje na juu ya sheria, hazina uhalali wa kusikiliza mashitaka haya.
Ndio maana kwa msingi huo wa uadilifu, sasa sisi Wazanzibari tunaoamini kuwa kesi dhidi ya Wazanzibari wenzetu waliopelekwa Bara ni ya kisiasa, tuna wajibu wa kuanzisha kampeni ya BringBackOurPeople.
Hiyo ni kheri moja miongoni mwa yatokanayo na shari za kashfa ya Tegeta Escrow Account kwa Zanzibar.
Iko kheri nyengine pia. Hivi umewahi kulisikia jina la Dokta Thomas Kashililah? Huyu ni Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mkasa huu wa Escrow, ripoti za magazeti zinasema kwamba kumbe ndiye huyu aliyeiandikia Mahakama Kuu kuiomba kile alichokiita “orodha ya kesi za Escrow zilizoko mahakamani ndani na nje ya nchi.“ Wachambuzi wanasema kuwa barua hiyo ilikusudiwa kupata idhini ya Mahakama Kuu kuzuia mjadala wa ripoti ya CAG juu ya kashfa hiyo usifanyike bungeni.
Ni kuwepo kwa barua hiyo ndiko kulikotaka kutumiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuuzuia mjadala huo. Yaliyobakia ni hadithi moja ya aibu sana kwa Mwana wa Mkulima Pinda, kwani hajawahi “kukosewa adabu“ na wabunge hata wa chama chake, kama siku aliyoonesha muelekea huo bungeni!
Lakini yalianza na Dk. Kashililah, yumkini kwa kimbelembele chake au kwa kufuata maagizo ya nguvu zisizoonekana nyuma yake.
Sasa Mzanzibari mwenzangu nikurudishe nyuma kidogo kwenye ‘ilivyopatikana‘ thuluthi mbili ya kura za Zanzibar kupitisha Katiba Iliyopendekezwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, wakati huyu huyu Dk. Kashililah akiwa ndiye Katibu Mwenza wa Bunge hilo akishirikiana na Yahya Hamad wa Baraza la Wawakilishi.
Mimi na wewe tunajuwa kuwa bunge hilo lililoongozwa na Samuel Sitta halikuweza kupata thuluthi mbili kutokea Zanzibar kupitisha Katiba Iliyopendekezwa na iliyoandikwa chini ya uwenyekiti wa Andrew Chenge, ambaye mwenyewe anatuhumiwa kupokea shilingi bilioni 1.6 kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Uliofanyika ulikuwa ni udanganyifu. Udanganyifu, kwa mfano, wa kuigeuza kura ya Zakia Meghji kuwa ya Zanzibar, ilhali mwenyewe hakutokea Zanzibar (kwa nafasi yake ya ubunge wala kisiasa). Udanganyifu, kwa mfano, wa kuipiga kura ya Ambar Khamis kuwa ya ndiyo, ilhali mwenyewe hata hakupiga kura. Udanganyifu, kwa mfano, wa kura hewa za mahujaji waliokuwa Makka, ambao ushahidi wa ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, unasema wazi kwamba hawakuweza kupiga kura. Udanganyifu, kwa mfano, wa Mohamedraza Dharamsi na Mohamed Turki, ambao kura zao hazikupigwa lakini zilihisabiwa kupigwa na zikaitwa ni za NDIO.
Hili unapoliunganisha na jitihada za kuzuia mjadala bungeni juu ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, hapana shaka, linakupa jawabu inayohoji uadilifu wa watendaji wa bunge, akiwamo Dk. Kashililah.
Na hili nalo linatupa hoja na haja ya kuanzisha kampeni nyengine kama Wazanzibari – BringBackOurKatiba!
- Makala: Faida ya kashfa ya Escrow kwa Mzanzibari imeandikwa na Mohammed Ghassani via Zanzibar Daima Online.
Post a Comment