Hoja kuwa hali ya elimu ya taifa hili ni mbaya imeendelea kuungwa mkono na wadau mbalimbali, safari hii Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameeleza kushangazwa kwake kuwa kwa Tanzania kadri mtu anavyozidi kusoma ndivyo anazidi kuwa tegemezi kwa ajira.

Alisema kipimo cha elimu kuporomoka ni hali iliyopo katika vyuo vikuu ambavyo viongozi wake wanakiri kutopata watu wenye viwango vinavyotarajiwa kuingia vyuo vikuu.
Katika mahojiano maalum na NIPASHE wiki iliyopita, Sumaye alisema ubora wa elimu nchini unazidi kuporomoka.

Kauli ya Sumaye inashabihiana na ile aliyotoa Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani, katika mahojiano maalum na NIPASHE akisema kuwa baadhi ya mahakimu wa mahakama nchini hushindwa kuandika hukumu za kesi wanazoziendesha kiasi kwamba zinapofikishwa Mahakama ya Rufaa huwa hazieleweki.

Sumaye naye alisema kuwa tatizo halipo kwa mahakimu tu bali pia kwa wahitimu wengine wa fani mbalimbali wanaoingia katika soko la ajira kwani hushindwa kuonyesha uwezo wao wa kitaaluma kwa sababu wengine hufundishwa kwa mtindo wa bora liende alimrad wanamaliza vyuo vikuu.
“Ukweli ni kwamba siyo jambo linalojificha na wala hatuwezi kulikwepa … elimu imeshuka na ndiyo maana idadi ya wanaofeli ni kubwa na ili waonekane wanafaulu, viwango vya ufaulu vimerekebishwa,” “Mtu ambaye zamani alikuwa anafeli (katika baadhi ya alama), sasa tunaambiwa amefaulu. Lakini ukweli uko pale pale kuwa kichwani hakuna kitu… kurekebisha madaraja ndiko kumemfanya naye aonekane miongoni mwa waliofaulu.”
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa, alisema kiwango cha elimu kinazidi kuporomoka kutokana na wanafunzi kutokuwa na maandalizi ya kutosha.
Aidha, alisema wapo wanaosema anapiga vita shule za kata, lakini siyo kweli kwani huwezi kuwa na shule nyingi kwa mara moja wakati hujaandaa walimu, vitabu na mahitaji mengine.

Alisema mpango wa maendeleo wa Dira ya Taifa 2025, imepanga mambo vizuri na hakuna kurukia jambo bila utaratibu, na imeelezwa elimu iongezeke kwa kiwango gani na uchumi kwa kiwango gani ili viweze kutegemeana.

“(Dira) imepanga mambo vizuri, hakuna kurukia kitu bila utararibu, inaeleza elimu iongezeke kwa kiwango gani na uchumi, ili jinsi kadri elimu inavyopanuka kuwe na mahali vijana wanakwenda na pia walimu wawepo wa kutosha,” alisema.

Alisema kwa sasa vimeanzishwa vyuo vikuu vingi nchini, lakini hakuna walimu wa kutosha na hivyo kutoa baadhi ya wahitimu wasio na viwango.

“Kila mwenye kinyumba kidogo tumemwambia fanya chuo kikuu, hata aliye na nyumba kama hii yangu tumemwambia aanzishe chuo kikuu… hakuna walimu, kuandaa mwalimu wa Chuo kikuu siyo jambo la haraka, unahitaji kuwafundisha kwa muda mrefu na (tena) katika taaluma nyingi,” alifafanua.

Sumaye ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo la Hanang’ kwa takribani miaka 20, alisema kwa sasa ni kawaida kukuta mwalimu mmoja akifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na Iringa, na kwamba matokeo yake, mwalimu wa aina hiyo muda wote huwa yupo barabarani na mwishowe, wanafunzi wanaishia kukosa elimu inayotakiwa.

“Niliongea na mwalimu mmoja wa Udom (Chuo Kikuu Dodoma), akaniambia anafundisha wanafunzi 1,000… sasa utawezaje kuwamudu wanafunzi wote hao? Elimu imeshuka, lakini yote ni matokeo ya kupanua elimu bila kuwa na maandalizi ya kutosha,” alisema.

Alisema kwa sasa serikali imeanza mpango wa ujenzi wa maabara kwenye kila shule ya sekondari, lakini kama hakutakuwa na vifaa vya maabara, itakuwa ni sawa na madarasa ya kawaida na mwishowe kurudi kwenye hali ile ile ya shule za kata.

Sumaye alisema enzi zake akiwa anasoma, waliokuwa wanafanya vizuri wanakwenda shule za serikali na waliofahuu kwa kiwango cha kawaida wanakwenda shule binafsi, lakini hali ni tofauti sasa kwani wanaofanya vizuri wanakwenda shule binafsi na wa kawaida shule za serikali na mwishowe shule nyingi za serikali kuonekana zikiwa na kiwango kisichoridhisha.

“Ukitaka kujua kwamba elimu ya nchi ni nzuri lazima upimie hapo… tunayo kazi kubwa. Lazima tuboreshe elimu yetu ili ifanane na wengine. Tuache kujitengenezea viwango vyetu, (elimu) haiwezi kuwa yetu pekee. Ifanane na Afrika Mashariki ambao tunashindana nao katika soko la ajira,” alisema.

Alisema kwa sasa tunaingia katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo ni lazima kutakuwa na ushindani wa elimu ambao viwango vya nchi husika vitawezesha Tanzania kushindana vyema.

“Una shahada mbili, lakini ulifundishwa kwa muundo wa chapchap (haraka haraka), hakukuwa na walimu, mwisho wa siku ataajiriwa aliye na shahada moja, lakini anayefanya vizuri kuliko mwenye shahada tatu au mbili… hili tunaliona sasa katika mahoteli na shule binafsi.

“Wengi wa waajiriwa ni kutoka nchi jirani. Hicho ni kipimo cha tofauti ya utoaji wa elimu. Katika utandawazi lazima tuwe na utaalamu unaoheshimika duniani. Hatuwezi kuwa na utaalamu wetu tu na hilo litawezekana kwa kuboresha elimu yetu,” alisema.

TATIZO LA AJIRA

Sumaye alisema ni lazima mitaala ya sasa katika elimu ipitiwe upya na kubadilishwa kwa kuwa elimu yetu kwa sasa humfanya mwanafunzi aamini kuwa akimaliza shule tu, basi jambo linalofuata ni yeye kuajiriwa.

“Huko nyuma nafasi zilikuwa nyingi. Mtazamo ulikuwa ni huo. Lazima tuwe na mitaala ambayo itamfanya mwanafunzi anayemaliza kidato cha nne awe na uwezo wa kujitegemea kuliko aliye mbele yake,” alisema na kuongeza:

“Hivi sasa ni tofauti. Jinsi mtu anavyozidi kupanda juu anazidi kuwa tegemezi kwa ajira. Lazima tutoke hapo, vinginevyo taifa halitafanikiwa, mitaala yetu ijibu tatizo la ajira,” alisema.

Alisema kwa sasa hakuna viwanda vya kutosha vinavyoajiri watu na hivyo kwamba sekta zilizojibana kama za mawasiliano na miundombinu ndizo zinakuza uchumi. Alisema ili kuimarisha eneo hilo, ni lazima kuwa na viwanda vyenye kuajiri watu wengi.

Alisema sekta binafsi lazima itawale, lakini haijaandaliwa vizuri kwa kuwa hakuna sera na sheria nzuri ili iweze kushika gurudumu vizuri zaidi na kuwezesha vijana wengi kujiajiri.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.