Jaji Warioba akiwapungia mkono wananchi waliokuwa wamefurika nje ya jengo la Ubungo Plaza ambako mdahalo wa kujadili Katiba inayopendekezwa ulikuwa ukifanyika. |
Shikamoo mzee wangu Warioba na pole sana kwa masaibu yaliyokukuta jana.
Mimi mjukuu wako pasi na shaka ukiangalia kwenye diary yako utanikumbuka kwani niliwahi “kukutupia” swali moja pale chuo kikuu Mzumbe siku ya tarehe 16 mwezi Novemba 2011.
Tangu hapo hatujapata kuonana tena ingawaje nimekuwa nikifatilia harakati zako zote tangu hapo? Kwanini nimekuwa nikifatilia? Jibu ni moja tu, kwa namna ulivyonijibu siku ile sikutia shaka uelewa wako mkubwa sambamba na uzalendo wako usio na doa kwa taifa hili.
Ulizidi kunifurahisha zaidi kwa namna ulivyoratibu mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya na uandaaji wa rasimu. Najua wapo baadhi ya “wakubwa” hawafurahishwi na namna unavyotetea kile
unachoamini ni chema kwa vizazi vijavyo vya Tanzania, Mungu akubariki sana.
Vitimbi ulivyofanyiwa na maneno ya kejeli uliyojibiwa yanaonyesha kuwa hayajakuvunja moyo hata kidogo, kwani jana nilikuona ukiongea kwa uso uliojaa bashasha huku ukidhihirisha kuwa ungali na ari ileile ya kupigania katiba ya wananchi.
Sitaki kukuchosha kwa maneno mengi mzee wangu lakini nina uhakika Mungu yuko upande wako katika hili, tuliotega sikio na kukusikiliza tunajua unaongea ukweli mtupu na MSEMA KWELI NI MPENZI WA MUNGU.
Hata manabii walipingwa na kudhihakiwa hivyohivyo lakini leo tunawasoma na kuwaheshimu kama mashujaa wa imani, ni ukweli kuwa katiba lazima iwe mwafaka wa kitaifa na siyo mpasuko wa kitaifa,
wanaokupinga wanalijua hili?
Wasalam,
Ni mimi Mjukuu wako mtiifu,
Nova Kambota
0712-544237, novakambota@gmail.com
novakambota.wordpress.com
Jumatatu Novemba 3, 2014
Post a Comment