ASEMA HATA CCM INAJUA MSIMAMO WAKE, WAZIRI KABAKA ASISITIZA KILIMO NI LAZIMA, PROFESA LIPUMBA, MBATIA WAMSHANGAA
Peter Edson
WAKATI
Serikali ikielekeza nguvu nyingi kutekeleza mkakati wa kuendeleza sekta
ya kilimo nchini uliopewa jina la Kilimo Kwanza, aliyewahi kuwa Waziri
Mkuu, Edward Lowassa ameibuka na kusema haungi mkono mkakati huo.Alisema
mkakati huo wa Kilimo Kwanza umekosa mashiko hivyo ili auunge mkono,
kuna haja ya kubadili dhana yake na kuwa, elimu kabla ya kilimo kwanza.
“Ni
vyema nikaeleweka hapa. Ninachomaanisha ni kuongeza elimu katika Kilimo
Kwanza ili wananchi wawe na elimu kwanza ndipo waweze kuboresha
kilimo,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika Kipindi cha Dakika
45 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV juzi usiku, Lowassa
alisema pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri ya kumkomboa mwananchi kwa
kuboresha mazingira ya kilimo, jambo hilo litakuwa si chochote kama
hatapatiwa elimu itakayomwongoza kwenye mapinduzi hayo ya kijani.
“Mpango
huu wa Kilimo Kwanza umekosa nguvu kwa sababu kuanzishwa kwake
hakukuzingatia dhana ya ukombozi wa mwananchi wa kawaida. Tangu awali
ndani ya chama (CCM) nilieleza kuwa sitaunga mkono hoja hiyo mpaka
kuongezwe mashiko na kuwa Elimu Kabla ya Kilimo Kwanza,” alisema Lowasa
na kuongeza:
“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitoa
uamuzi mgumu na wenye busara, ndiyo maana kilimo cha pamba, kahawa,
mkonge na mazao mengine vikaanzishwa. Hivyo ipo haja ya kufanyika
mchakato wa kuona mbali zaidi ili viongozi wetu waweze kutoa uamuzi
sahihi katika hoja hii ya Kilimo Kwanza, kwani nguvu nyingi pasipo elimu
inaweza kuligharimu taifa.”
Alisema kuwa ili mwananchi wa
kawaida aweze kunufaika na Kilimo Kwanza, anahitaji kupatiwa elimu ya
kutosha ya namna ya kuandaa mazingira ya kilimo na uelewa wa vifaa na
pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na dawa.
Alisema pamoja na kuwa
na mabwana shamba wachache, wananchi wamejikuta wakitumia mawazo yao
kufanikisha miradi ya kilimo katika maeneo yao na matokeo yake wanapata
mazao kidogo ambayo hayawakwamui kiuchumi.
Alitoa mfano wa nchi
ya Indonesia akisema inaendesha uchumi wake kwa kilimo cha michikichi,
ambayo mbegu zake zimetoka Tanzania... “Lakini Tanzania iliyotoa
michikichi hiyo sasa ni moja ya wateja wa mafuta hayo yanayotoka
Indonesia.”
Alishauri Serikali kuanzisha mashamba ya michikichi
maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha hivyo
kujitosheleza kwa mafuta hata ya kuuza nje.
“Ningelikuwa na uwezo
wa kutoa uamuzi, vijana wetu wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa), ningewapa
kazi ya kuanzisha mashamba ya michikichi nchi nzima kwani nchi yetu
imejaliwa kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba, mapori yapo mengi,”
alisema Lowassa.
Alisema wananchi wanaweza kupewa matrekta na
pembejeo mbalimbali za kilimo, lakini bila kupewa elimu elekezi ya namna
ya kuzitumia pembejeo hizo kuzalisha mazao bora, itakuwa kazi bure kwa
kuwa ongezeko la mazao litakuwa dogo kama ilivyo kwa kilimo cha jembe la
mkono.
Alitoa wito kwa Serikali kutumia fursa zilizopo za miradi
ya kilimo kuwaelimisha Watanzania ili baadaye waweze kupewa au
kukopeshwa zana za kilimo, akieleza kuwa nguvu kazi na elimu, ndivyo
vitakavyomkomboa mwananchi katika umaskini wa kipato.
Kabaka: Kilimo lazima
Alipotakiwa
kuzungumzia kauli hiyo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka
alisema kilimo ni lazima na Lowassa lazima akubaliane na mpango wa
Serikali wa kutekeleza Kilimo Kwanza.
“Lowassa lazima akubaliane
na msimamo wa Serikali wa kutekeleza Kilimo Kwanza. Kilimo ni lazima,”
alisema Kabaka na kuongeza kuwa sekta hiyo ndiyo inayotoa ajira kwa watu
wengi kuliko nyingine.
Alisema Tanzania ina wahitimu zaidi ya
800,000 wa elimu ya juu wa fani mbalimbali ambao moja ya ajira ambazo
wanapaswa kujiunga nazo ni kilimo na hakuna ambaye anaweza kutafuta
elimu akiwa na njaa... “Serikali itaendelea kusimamia Kilimo Kwanza na
tunamtaka Lowassa atuunge mkono.”
Waziri huyo alisema Serikali
haipuuzi elimu, lakini ukweli unabaki kuwa sekta ya kilimo ilisahaulika
kitambo hivyo kupitia Kilimo Kwanza ukiacha ajira za wakulima wa
kawaida, pia maofisa ugani wa kada mbalimbali wanaajiriwa.
“Hata
huko kijijini huwezi kusema unampelekea elimu mtu ambaye ana njaa.
Huwezi kueleweka, lakini tunajua watu wakishiba wataweza kufanya mambo
mengine hivyo kauli yake kuwa kwanza ingetolewa elimu haina tija,”
alisema.
Profesa Lipumba, Mbatia wamshangaa
Kauli hiyo ya
Lowassa imeonekana kumkera mchumi maarufu nchini na Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia. Kwa
nyakati tofauti jana, viongozi hao wa vyama vya upinzani walihoji
mamlaka ya kimaadili aliyonayo Lowassa ya kusema hayo.
Profesa
Ibrahim Lipumba alimponda akisema anachofanya kada huyo wa CCM ni
kujipapatua kisiasa kwani Kilimo Kwanza ni muhimu kwa maendeleo ya
Taifa.
Profesa Lipumba alisema kauli hiyo ya Lowassa inaonyesha
kana kwamba hafahamu vizuri mkakati huo wa Kilimo Kwanza hivyo ni bora
akachukua muda kujifunza kabla ya kutoa kauli hizo.
Profesa
Lipumba alisema katika kutekeleza Kilimo Kwanza, elimu pia hutolewa
hivyo haiwezekani kusema kuwa itolewe kwanza elimu kabla ya kutekeleza
mpango huo, kwa kuwa vyote vinakwenda pamoja.
“Huwezi kusema kuwa eti
utoe elimu kwanza kisha ndiyo uanze utekelezaji. Hivi vyote vinatakiwa
kwenda pamoja labda kasoro zilizopo ni kuwa Kilimo Kwanza kimewalenga
wakulima wakubwa wakitarajiwa wawainue wadogo jambo ambalo
haliwezekani,” alisema.
Alisema utekelezaji wa Sera ya Kilimo ni
jambo jema kutokana na ukweli kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 10
iliyopita, wakulima wamesahaulika na kufanya ukuaji wa kilimo kuwa
asilimia nne, kiwango ambacho ni cha chini kwa mahitaji ya ongezeko la
watu ambalo ni wastani wa asilimia moja kwa mwaka.
“Kilimo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa lolote duniani na kitendo
cha
kuwategemea wakulima wakubwa ni kasoro ambayo inapaswa kufanyiwa kazi
katika utekelezaji wa mpango huu wa Kilimo Kwanza,” alisema Profesa
Lipumba.
Mbatia alisema anamshangaa Lowassa kupingana na uamuzi
wa chama chake kwa kuwa mkakati wa Kilimo Kwanza ulipitishwa na chama
chake... “Lowassa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, hivyo Kilimo
Kwanza ni uamuzi wa CCM. Anapingaje wakati hata alipojiuzulu alisema
anafanya hivyo kulinda masilahi ya chama, leo anapinga mipango ya chama
hichohicho?”
Alisema kama anaona haendani na mambo yanayofanywa
na CCM ni vyema ajiondoe na kujiunga na chama kingine au kuanzisha chake
ili awe na fursa nzuri ya kupinga kazi za chama tawala.
Ajira
Lowassa
pia alizungumzia suala la ajira akisema viwanda vikifufuliwa
vitanufaisha Watanzania wengi kwa kupata ajira na hivyo kuondoa dhana ya
kuwepo kwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu wasiokuwa na ajira.
“Unapotangaza
kazi ya watu 20, barua za maombi ya kazi zinakuja 2,000, tusisubiri
maandamano, tutatue tatizo hili sasa,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Hili
suala linahitaji ufumbuzi wa haraka ingawa tumechelewa. Nilimshangaa
sana yule waziri niliposema kuna shida ya ajira, akasema hakuna tatizo
hilo.”
Tangu mwaka jana, Lowassa amenukuliwa na vyombo vya habari
mara kadhaa akisema ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo kubwa nchini,
akilifananisha na bomu linalosubiri kulipuka ikiwa halitatafutiwa
ufumbuzi.
Hata hivyo, Machi 21 mwaka huu, Kabaka katika mkutano na wanahabari alipinga kauli hiyo ya Lowassa akisema:
“Hali
halisi ya ukuaji wa uchumi nchini ni nzuri lakini, haiwezi kuonekana
kama wananchi wake ni maskini na hawana ajira. Hata hivyo, Serikali
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia suala hilo ikiwamo la
kuhimiza uwekezaji nchini,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Kitendo
cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu
linalosubiri kulipuka, siyo kweli na kudai Serikali haijafanya kitu
wanakuwa hawaitendei haki. Tatizo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka
2000/01 hadi asilimia 11.7, mwaka 2006.
Mbio za urais 2015
Alipotakiwa
kueleza iwapo ana mpango wa kuwania urais mwaka 2015, Lowassa alisema
suala hilo halipaswi kuzungumzwa sasa kwani linaweza kufungua uwanja wa
malumbano.
“Waingereza wana msemo mmoja unaosema, ‘tutavuka
daraja tutakapolifikia.’ 2015 bado ni mbali ukisema chochote sasa
utafungua uwanja wa malumbano, tusubiri 2015 bado ni mbali,” alisema
Lowassa.
source by Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/25822-lowassa-siungi-mkono-kilimo-kwanza.html