Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda (Kushoto) akizungumza na Waandishi wa habari alipokuwa akiwaonesha meno ya Tembo yaliyokamatwa juzi Mkoani humo. (Picha : Geofey Nyang'oro/Mwananchi)

KWA mara nyingine katika muda usiozidi wiki tatu, watu watatu wametiwa mbaroni kwa kosa la kusafirisha pembe 78 za ndovu kutoka wilayani Masasi, mkoani Mtwara. Tunaambiwa kuwa, Pembe hizo ambazo wataalamu wa wanyamapori wanasema zimetokana na tembo 39 zimekadiriwa kuwa na thamani ya Sh935 milioni.

Polisi wanasema askari waliokuwa katika moja ya vituo vya ukaguzi mjini Iringa walilisimamisha gari hilo lililokuwa na shehena ya pembe hizo za ndovu mapema wiki hii baada ya kulishtukia, lakini dereva wa gari hilo alikataa kusimama, hivyo kuwalazimisha askari katika kituo hicho cha ukaguzi kulifukuza gari hilo na kufanikiwa kulikamata katika Kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni ambapo polisi walikuwa wameweka kizuizi baada ya awali kupewa taarifa na wenzao wa mjini Iringa.

Mshikemshike na kashkashi iliyotokea katika kituo hicho cha Polisi mpaka majangili hayo yakatiwa mbaroni ilikuwa kubwa ingawa sasa ni historia. Hata hivyo, yafaa ifahamike tu hapa kwamba majangili hayo yalilitekeleza gari hilo lenye shehena na kujificha vichakani hadi wananchi walipoyakurupusha na kuwawezesha polisi kuyakamata pamoja na gari hilo lenye pembe hizo za ndovu zenye uzito wa kilo 212.

Tumezungumzia sakata hilo kwa kirefu kutokana na ukweli kuwa, kwa muda mrefu sasa matukio ya vitendo vya ujangili wa kutisha katika mbuga zetu za wanyama vimekuwa vya kawaida. Ilifika wakati majangili wakapata ujasiri wa ajabu wa kuwakamata wanyama mchana kweupe, wakiwamo twiga, na kuwasafirisha nje ya nchi kupitia katika viwanja vyetu vya ndege ambavyo vina ulinzi mkubwa pengine kuliko mahali popote hapa nchini.

Tukio hilo ambalo hakika lilikuwa la aina yake tangu nchi yetu ipate uhuru liliiacha Serikali katika aibu na mfadhaiko mkubwa, kwani lilionyesha pasipo shaka kwamba nchi yetu ina mtandao mkubwa wa ujangili unaohusisha baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, wanasiasa, vigogo serikalini na baadhi ya watumishi katika vyombo vya ulinzi na usalama.

Vitendo hivyo vya ujangili na usafirishaji nje wa pembe za ndovu na nyaraka nyingine za Serikali umeiacha nchi yetu katika aibu kubwa. Mwezi uliopita, Serikali ilikiri kukamatwa nchini China kwa pembe 569 za ndovu zenye thamani ya Sh2.24 bilioni kutoka Tanzania.

Hii ilitanguliwa na matukio mengi ya aina hiyo ambayo hakika yameifanya Tanzania kuonekana kituko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Wengi wanajiuliza, biashara ya pembe za ndovu inamilikiwa na kuwezeshwa na kina nani? Usafirishaji wa pembe hizo na nyaraka nyingine unaratibiwa na magenge gani katika bandari, stesheni za treni na viwanja vya ndege? Ni kwa kiasi gani vyombo vya kiserikali kama Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), vinahusika?

Hayo bila shaka ni maswali magumu yanayohitaji majibu. Haiwezekani nchi yetu iendelee kuporwa rasilimali zake, huku mamlaka husika zikitazama tu pasipo kuchukua hatua stahiki na kuwaacha wananchi wakiogelea katika umaskini wa kutisha. Pamoja na hatua za zimamoto zinazochukuliwa hivi sasa na wizara husika, ukweli ni kuwa, kwa muda mrefu Serikali imekosa utashi wa kisiasa wa kukomesha vitendo hivyo au kufanya ufuatiliaji wa namna fulani.

Ndiyo maana wengi wanadhani Serikali inajua kinachoendelea. Inakuwaje mamia ya watu wanaokamatwa kwa ujangili au usafirishaji wa nyara za Serikali hawabanwi vya kutosha ili wawataje wamiliki wa biashara hiyo au mawakala wao?

via gazeti la Mwananchi







































































Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.