Licha ya harakati mbalimbali za kumkomboa mwanamke, bado kuna
mabosi nchini wanawanyanyasa wanawake kwa kuwalazimisha kufanya nao
ngono.
Wapo wanaonyanyaswa au hata kuteswa ikiwemo
kusemwa maneno machafu au kutishiwa kufukuzwa kazi kwa sababu tu
wamekataa kutoa penzi kwa bosi.
Wale wanaokubali, wengine wanaishia kupewa ahadi
hewa za kufundishwa magari, kupelekewa kozi mbalimbali. Hata hivyo mbaya
zaidi ni kwamba mabosi wengine hata kama wameoa, hupenda kuwamiliki
wanawake hao kana kwamba ni wake zao kwa kuwafuatilia sana nyendo zao.
Ukahaba wa mabosi hufanywaje?
Baadhi ya wanaume kwa mwonekano ni vigumu kuamini
kama ndiyo wanaofanya vitendo vichafu kwa wafanyakazi wao. Wanaposimama
kwenye vikao, utasema mtu huyu, lakini wafanyakazi wa kike wamekuwa ni
wenye kuwanyanyasa mno.
Baadhi ya mabosi wamekuwa wakitoa vitisho kuwa
‘kama hunipi penzi nitakuporomosha cheo au hata kukufanyia visa vyovyote
hadi uhame’.
Katika baadhi ya ofisi badala ya mabosi kutumika
kama washauri wa wafanyakazi wao kuzipenda ndoa na nyumba zao, ndio
wamekuwa wakitumia fedha zao kuwahonga wanawake hata magari, huku
makatibu muhtasi wakidaiwa kuwa ndio wanaosumbuliwa zaidi.
Wapo mabosi huwaingia wanawake wakiwemo wake za
watu kwa kuwapangia safari za mikoani au nje ya nchi hasa wanapoona
hawana wepesi wa kukubaliana na matakwa yao.
“Nakumbuka kuna bosi mmoja katika ofisi moja nyeti
aliwahi kudaiwa kumnunulia gari mke wa mtu kabla ya kuhama chombo
hicho,” anasema mkazi mmoja wa Kimara.
Bosi aliweza kumpa safari ya nje mwanamke na kisha kumnunulia gari zuri kuliko la mumewe.
Hii ni moja ya kati ya matukio mengi ya mabosi
kuwaingiza wafanyakazi wao katika ngono badala ya kuwa ndio washauri
wema kwa wafanyakazi ili waweze kuziheshimu ndoa zao.
Sifa zifaazo kwa mabosi
Kwa mujibu wa msomi maarufu katika tansia ya uongozi,
Christopher Rocchio wa Marekani, katika chapisho lake la ‘Secret
Millionaire’, mabosi wanapaswa kutoa miongozo mizuri ya namna ya kuishi
vema ndani na nje ya sehemu za kazi, kwa bahati mbaya, baadhi yao
wamekuwa sababu ya kuharibika kwa ndoa za wafanyakazi wao.
Wataalamu wengine katika masuala ya uongozi na
utawala, Ruth Faulkner katika chapisho lake la “Viridor boss’ na
Fernandez, Maria-Elena katika gazeti la Los Angeles Times, mabosi
wanaweza kuchangia kuharibu au kujenga ndoa za wafanyakazi wao kutokana
na mafundisho au namna wanavyoendesha mambo sehemu za kazi.
Je, wewe ni bosi wa namna gani au ofisini kwenu
mabosi wenu wakoje? Kila mtu aliyeko kwenye ajira analo jibu lake. Hata
hivyo kwa vyovyote inavyokuwa ni suala la msingi kila bosi kutafakari
kwamba dhamana aliyonayo si kufanya ngono wala kutongoza wafanyakazi na
kuwatisha, bali kushirikiana nao kuongeza mafanikio katika eneo la kazi.
Simulizi ya mmoja wa wanawake
Mwajuma Sabuni (sio jina lake halisi), ni
mfanyakazi katika kiwanda kimoja jijini Dar es Salaam (jina
linahifadhiwa) analalamikia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wenye
vyeo vya juu yao.
“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba
sasa. Sisi wafanyakazi wa kike imekuwa ni kawaida kulazimishwa kufanya
ngono.Baadhi ya wasimamizi wa vitengo ndio wahusika wakuu wa kulazimisha
wapewe ngono, ukiwakataa ajira yako inakuwa hatarini”.
Haya ni baadhi ya mambo mabaya wanayofanyiwa wanawake sehemu za kazi.
Baadhi yao hulazimika kujiingiza kwenye ngono
zisizo salama kwa sababu tu wanaogopa kuwaambia mabosi wao watumia kinga
kwa hofu kwamba itaonekana kama ni kuwadhalilisha kuwa huenda wana
Ukimwi.
Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa
Ukimwi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wanawake wako kwenye hatari
zaidi ya kuathirika na ugonjwa huo kwa sababu baadhi ya hao mabosi
hawatumii kinga na huwa hawako tayari kupima, kwa bahati mbaya zaidi
wale wanaofanya nao baadhi yao huogopa kuhoji chochote hivyo mabosi
hufanya watakavyo ikiwemo kutotumia kinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti Ukimwi
nchini (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema, “Hatari ya wanawake
kuathirika na Ukimwi ni kubwa mno. Pia ni changamoto kubwa inayohitaji
jitihada za kila mmoja wetu.”
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi nchini (Tucta), Hezron Kaaya anapendekeza mifuko ya hifadhi
ya jamii kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wanawake na wasichana.
Mkurugenzi wa Sera na Utetezi wa Chama cha Waajiri
nchini (ATE), Justina Lyela ambaye amewataka waajiri nchini kuepuka
kuwapunja wafanyakazi wa kike ukilinganisha na wanaume ili kuwawezesha
kiuchumi.
Tamwa na unyanyasaji
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa),
katika moja ya mpango mkakati wake wa miaka mitano 2010-2014, pamoja na
mambo mengine kimepanga kufanya shughuli ambazo zitaimarisha elimu kwa
mtoto wa kike kwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Unyanyasaji wa kijinsia
Unyanyasaji wa kijinsia ni tendo baya kwa haki za
binadamu na linasababisha maumivu kwa wahusika. Vilevile, linahusisha
kumlazimisha mtu kufanya nae mapenzi bila ridhaa yake. Lakini kufanya
mapenzi na watu kama baba, mama, kaka, dada, babu au bibi ni aina
nyingine ya unyanyasaji wa jinsia.
Unyanyasaji wa kijinsia ni kosa la jinai.
Unyanyasaji huo ni pamoja na kutumia maneno kwa mfano baadhi ya mabosi
huwatishia wafanyakazi wa kike kwamba wasipokubali kufanya nao ngono
watawafukuza kazi.
Unyanyasaji sio unahusisha sauti, ishara au
maonyesho ya sehemu za mwili kwa makusudi kinyume na matakwa ya mtu,
kwamba kwa mfano mtu anaweza kukuonyesha sehemu za siri au kukuvamia kwa
kugusa sehemu zako za siri kama njia ya kukushawishi mfanye ngono.
Kanuni za adhabu (sura ya 16) kama zilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002, zipo wazi kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa
kujamiiana na mtu mwingine bila ya ridhaa yakeÖ.anayefanya hivi maana
yake ni sawa na ubakaji.
Ni kosa kupigwa busu bila ridhaa
Sheria ziko wazi kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kushika viungo vya siri vya uzazi, au kukupiga busu bila ya ridhaa ya mhusika.
Hivi karibuni, Tamwa ilizindua ripoti ya utafiti
wa unyanyasaji wa kijinsia uliofanyika Aprili mwaka huu katika wilaya 10
za Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkurugenzi wake, Valery Msoka anasema waafiti
waliwahoji watu mbalimbali katika ngazi za familia na kupata ukweli wa
hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia.
W i l a y a zilizofanyiwa utafiti ni Wete (Pemba
Kaskazini), Mjini Magharibi (Unguja Magharibi), Unguja Kusini,
Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Mvomero (Morogoro), Lindi vijijini
na Ruangwa (Lindi), Kinondoni na Ilala, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Tamwa matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa
ujumla yameshamiri nchini, na kwamba zaidi ya asilimia 39 ya wanawake
nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.
Watuhumiwa wa unyanyasaji huu kwa kiwango kikubwa ni wanaume, huku sheria zikionekana kushindwa kuchukua mkondo wake ipasavyo.
Mfano halisi ni ripoti ya Polisi Zanzibar, ambayo
inasema katika mwaka 2011, yalikuwapo matukio 268 ya unyanyasaji
yaliyoripotiwa, kesi zilizofikishwa mahakamani ni 55, hata hivyo ni kesi
moja ndiyo iliyomtia mtuhumiwa hatiani.
Je, nini kifanyike kuepusha mateso wanayofanyiwa
wanawake maofisini? Ni changamoto ambayo inapaswa kuendelea kufanyiwa
kazi ili kuepusha mabosi viwembe wanaoendelea kuwanyanyasa wanawake
wakitumia madaraka yao.
Waziri Sophia Simba wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, ametaka kuwepo usawa wa fursa kama vile elimu na rasilimali
za uchumi hasa kwa wanawake.
Waziri Simba anaamini kwamba kwa jitihada ambazo
Serikali inaendelea nazo nchini, tatizo la unyanyasaji wa kijinsia
litaendelea kupungua.
Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na uwepo wa
sheria mbalimbali ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaonekana
kushawishi watu kujali haki za kijinsia.
Post a Comment