Vijana nchini wametakiwa kuwa wa wazi, waaminifu na waadilifu kwani huo ndiyo msingi mkubwa wa kupambana na  rushwa ili waweze kuwa viongozi wazuri hapo baadaye.


Rai hiyo imetolewa leo na Kiongozi wa Mbio za Mwenge taifa Juma Ali Simai wakati akiongea na wanafunzi wa Chuo Cha Ufundi cha Veta likichopo katika  Manispaa ya Lindi mara baada kuzindua klabu ya kupinga  rushwa chuoni hapo.


Alisema kuwa hivi sasa kuna baadhi ya viongozi ambao wanakusanya mapato na kodi za wananchi na kuzitumia vibaya na hivyo  kusababisha shughuli za maendeleo kutofanyika ikiwa ni pamoja na kutojengwa kwa shule na vituo vya afya na wanaoathirika ni wananchi wote.


Simai alisema, “Vijana ni tegemeo la taifa chukueni  hatua dhidi ya rushwa, kila mtu awajibike kwa kutoa  taarifa na ushahidi ili wahusika wachukuliwe hatua ni lazima mjifunze kutokana na makosa yanayofanyika leo ili nanyi msifikie huko kwani rushwa ni mbaya na adui mkubwa wa maendeleo”


Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge Taifa  alisema mtu ukiwa muadilifu na muaminifu hata  sehemu ya  kazi utaonekana na utapanda kutoka hatua moja kwenda nyingine bila ya kutoa rushwa na kutoa mfano kwa wanafunzi hao mara baada ya kumaliza masomo yao watapata ajira  bila ya kutoa rushwa kwani ni haki yao kuajiriwa au kujiajiri.


 “Kama wananchi watapata  taarifa na haki zao kwa wakati kutoka kwa viongozi wao wataepukana na  mazingira ya rushwa lakini hivi sasa kuna baadhi ya watu wanaona kuwa hawawezi kupata haki zao za msingi hadi watoe rushwa.


Ninawaomba wale wote wenye tabia hii muiache na mtoe taarifa kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili pale mnapoombwa kufanya hivyo kwani rushwa ni adui wa haki na mfahamu kuwa kwa anayetoa na anayepokea wote wanakabiliwa na kosa la jinai”, alisema Simai.


Simai alisema kuwa ni muhimu vijana wakawajibika  na kuwa wawazi katika mambo wanayoyafanya kwa maana ya kwamba wakipata nafasi wawashirikishe na wengine pia wafuate  misingi ya utawala bora katika kupambana na rushwa.


Akisoma taarifa ya klabu ya wapinga rushwa katika chuo hicho Christina Mkolela ambaye ni mwanachama alisema kuwa ili kupambana na rushwa katika halmashauri ya Manispaa ya Lindi waliamua kuanzisha klabu hiyo ikiwa ni moja ya mkakati wa kuelimisha vijana waliopo vyuoni ili kuwajengea uzalendo wa kuchukia rushwa na baadaye kuwa raia wema wasiopenda kupokea wala kutoa rushwa.


Alisema klabu hiyo ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na wanachama 91 kati ya hao wasichana ni 21 na wavulana ni 70 ambao wanashiriki katika kutoa elimu ya kuzuia na kupambaa na rushwa kwa wenzao.

Mkolela alisema, “Klabu hii ni ya kudumu na itaendelea kupokea wanachama ambao ni wanavyuo watakaokuja chuoni hapo kila mwaka na hivyo kuifanya kuwa  endelevu”.



Kabla ya kuwasili chuoni hapo Mwenge huo wa uhuru ulipokelewa kutoka wilaya ya Lindi na  viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wa Manispaa ya Lindi akiwemo mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika eneo la Mto Mkavu – Mbanja.


Ukiwa katika Manispaa ya Lindi Mwenge wa uhuru utafungua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kati ya miradi hiyo ni mradi wa maji safi kwa matumizi ya binadamu na mradi wa samaki.


Sherehe za kilele za  mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitaenda sambamba na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na maadhimisho ya wiki ya vijana zinatarajia kufanyika tarehe 14/10/2013 katika uwanja wa Samora uliopo Manispaa ya Iringa.


Mwisho.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.