WATU watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia kituo cha mafuta cha EAFCO kilichopo eneo la Mwenge mjini Singida, na kupora shilingi laki tano baada ya kufyetua risasi moja hewani kwa lengo la kuwaogofya wafanyakazi.
Watu hao wanadaiwa walikuwa wamebeba bunduki
moja ya kienyeji inayodhaniwa kuwa ni aina ya gobore na bastola moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,Geofrey
Kamwela,alisema tukio hilo limetokea Septemba tisa mwaka huu saa 11.00 jioni
eneo la Mwenge mjini Singida.
Alisema awali watu hao waliteka taksi yenye
usajili T.637 AGL aina ya Toyota mark 11 iliyokuwa ikiendeshwa na Ernest Joseph
(32) mkazi wa Misuna mjini Singida,na kisha kuitumia katika kutekeleza azma
yao.
“Huyu dereva wa taksi baada ya
kutekwa,alifungwa kamba ya katani na kuweka kwenye buti ya nyuma na kwenda naye
kwenye eneo la tukio na wakati uporaji huo unafanyika,dereva huyo alikuwa ndani
ya buti la gari lake”,alisema Kamwela.
Kamanda huyo alisema majambazi hayo yalipofika
kwenye kituo hicho cha mafuta,walifyetua risasi moja hewani kwa kutumia bunduki
aina ya gobore kwa lengo la kuogofya watumishi na wateja waliokuwa kwenye kituo
hicho.Baada ya hapo,ndipo yalipofanikiwa kupora shilingi 500,000.
Alisema polisi walipopata taarifa ya tukio
hilo,walifika mara moja kwenye kituo hicho na kukuta majambazi hayo kwa kutumia
taski waliyoiteka,waliishatoroka lakini hawakufika mbali walipata ajali na
kuitekeleza taksi hiyo na wao kukimbilia kusikojulikana.
“Wakati majambazi hayo yanatoroka,moja
lilidondosha bunduki aina ya gobore ambalo limeokotwa na polisi.Kwa sasa
tunaendelea na msako wa kuyasaka majambazi hayo ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake”alisema Kamwela.
Wakati huo huo,Kamanda Kamwela alisema dereva
Ernest alifikiwa katika hospitali ya mkoa na kupata matibabu na kisha
kuruhusiwa.
MWISHO.
Post a Comment