Rais Jakaya
Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pole Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kuuawa kwa mtu mmoja
na wengine sita kujeruhiwa akiwemo mhubiri wa amani ajulikanaye kama
Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar, kutokana na kurushwa kwa Bomu
katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika katika eneo la Darajani
tarehe 13 Juni,2014, mjini Unguja.
‘Hicho ni
kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na
Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala
hakikubaliki katika dunia ya sasa’ Rais amesema na kuongeza kuwa; ‘Hiki
ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina
yeyote ile’.
Rais amekemea na kuwataka watu
kuwa wastaarabu, wavumilivu na kuheshimu imani na mitizamo ya watu
wengine hata kama hawakubaliani nao.
Rais
amesema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu ambao
wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini ambapo
ndipo mahali panapostahili Amani, Uvumilivu na Unyenyekevu zaidi kwa
kuwa ni wakati ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba wake.
Rais
Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya haki wale wote waliohusika katika tukio hilo lisilo la
kistaarabu.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu-Dodoma
15 Juni, 2014
Post a Comment