NDOA nyingi za utotoni husababishwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwalazimisha watoto wao wa kike kuolewa katika umri mdogo kwa tamaa ya kujipatia fedha ama utajiri katika familia zao jambo ambalo linawanyima haki ya kusoma watoto wengi kwani watoto hawa wanakuwa wako katika umri chini ya miaka kumi na nane.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Wailesi Wilaya ya Temeke Bw. Abdul Kidege
wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Jamvi la Vijana linalofanyika kila mwisho wa
mwezi katika kituo cha vijana UMATI jijini Dar es Salaam.
Bw.
Kidege amesema kuwa kuna baadhi ya wazee na vijana wenye tabia ya kuwarubuni
wasichana wadogo kwa kuwapa pesa na vitu vya thamani kwa lengo la kuwashawishi
kuolewa nao na pia kuna baadhi ya wazazi ambao wakati mwingine ushirikiana
katika kufanikisha azma hiyo jambo ambalo ni kinyume na haki za watoto katika
jamii.
“Kuna
baadhi ya wasichana wenye umri mdogo wamekuwa wakinyanyaswa kijinsia kwa
kubakwa na wengine kulazimishwa na wazazi wao wenyewe kuolewa na watu wazima
ambao wamewazidi umri, jambo hili halikubariki na vijana nawaasa msikubali
kurubuniwa kwa pesa au vitu toka kwa watu wa namna hiyo”. Alisema Bw. Kidege.
Kwa
upande wake Afisa Vijana Msaidizi Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania
(UMATI) Bi. Upendo Daud amewaeleza vijana waliohudhuria tamasha hilo kuwa
vijana wanapohudhuria matamasha katika kituo cha UMATI wanapata fursa kubwa ya kupata
elimu bure juu ya afya ya uzazi, athari za mimba za utotoni, kupima Ukimwi,
ushauri nasaha, uzazi wa mpango pamoja na uelimishaji rika jambo ambalo
linawafanya vijana wengi waweze kujitambua na kujikinga.
“Hili ni Tamasha kwaajili ya vijana
linaloandaliwa kila mwisho wa mwezi na Youth Action Movement (YAM) kwa lengo la
kuwaelemisha vijana juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na afya na mada kuu
ya tamasha hili kwa leo ni Ndoa za umri mdogo na athari zake”. Alisema Bi. Upendo.
Youth
Action Movement (YAM) ni kikundi cha Vijana ambacho kilianzishwa na chama cha
uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI) kwa ufadhili wa Internationa Planned
Parenthood Federation (IPPF). Chama hiki cha vijana kinapatikana katika kila
tawi la UMATI nchi nzima na kwa tawi la Dar es Salaam ndiyo waandaaji wa Jamvi
la vijana kila mwezi ambapo husaidia kutoa huduma bure kwa vijana kuhusu afya
ya uzazi, kupima Ukimwi, ushauri nasaha, uzazi wa mpango pamoja na uelimishaji
rika.
Post a Comment