IMEGUNDULIKA kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye mfadhili mkuu na mpanga mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya cha siasa, Allaince for Change and Transparency (ACT-Tanzania).

Lowassa aibukia ACT
Mbunge wa Monduli, Mh Edward Lowassa
Kwa wiki kadhaa za hivi karibuni, makundi ya wanachama, washauri na wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi ya kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mapande ili kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Lowassa amejiaminisha kwamba ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia CCM. Kazi kubwa anayoona mbele yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani wakati wa kampeni utakapofika.
Zitto naye, ambaye uanachama wake kwa CHADEMA umebaki kwenye makaratasi tu, anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT, na amekuwa na uhusiano wa “kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matata ya wazi na chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo vyake vyote vya uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.
Katika hatua mojawapo, chanzo kimoja kilicho karibu na Lowassa kimesema kwamba mapema mwaka juzi, Zitto alimwendea Lowassa na kumwambia kuwa mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA si mzuri, na kwamba alikuwa tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake, lakini kwa sharti kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais, basi amteue kuwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kauli hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa sababu ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye mwaminifu, ambaye yupo tayari kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo lilimfanya Lowassa atilie shaka lengo la ombi hilo.
Jambo la pili lililomshtua Lowassa ni cheo kilichopendekezwa na Zitto, maana kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu lazima atokane na wabunge wa majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge wengi.
Kwa kuwa hoja hiyo ilitolewa katika mazingira ya Katiba ya sasa, na kwa kuwa haikujulikana wakati ule kama Zitto alikuwa bado ni mwanachama na kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata nafasi kauli hiyo, lakini amekuwa anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.
Hata hivyo, taarifa zinasema uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku wapambe wa Lowassa wakipita huku na kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila Zitto inakufa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga rasmi na ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, na timu ya Lowassa imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA, na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya ishindwe kumfuatilia na kumshambulia Lowassa.
Katika kikao cha mwisho kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na “Vijana wa Zitto” kilijumuisha baadhi ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye kauli ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu wa karibu kifamilia na Lowassa na washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ajenda zao nje nje 
Moja ya ajenda zao kuu ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo wa CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi za uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama, na baadaye wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta msisimko wa kitaifa.
Gazeti hili lina taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa CHADEMA ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa wakiwapigia simu na wakati mwingine kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha na vyeo ili wajiondoe CHADEMA.
Baadhi hao ni viongozi wa majimbo na mikoa ambao katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hawana uhakika wa kuchaguliwa kutokana na upinzani mkubwa unaojitokeza baada ya chama kukua na kuvutia wasomi na wafanyabaishara wenye mvuto katika maneo yao.
Baadhi ya viongozi walioendewa au kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje ya chama.
Mbinu mojawapo ambayo imekuwa inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu kuvunja ngome za CHADEMA ni kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi kubwa ya wabunge wa CHADEMA wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja majina kama njia ya kujenga ushawishi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi hao wameliambia gazeti hili kuwa wanajua hizo ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi ya wabunge wanaotajwa wamesema hizo ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na chama chao na kujitafutia njia mpya kwa kutumia majina yao.
Mmoja wao alisema, “Zitto mwenyewe ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia ya kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu kadhaa tumeshasikia, ni ile ile roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye amekosana na chama, anatafuta watu wa kufa naye.”
Mbali na kupandikiza wagombea nafasi za uongozi na kuvizia viongozi wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya chama, wamekuwa pia na mbinu ya kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa” katika baadhi ya majimbo, wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia CHADEMA.
Makada kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti hili na kutumia kauli zijazofanana. Kwa mfano, makada sita walioweka nia ya kugombea ubunge katika majimbo kadhaa ya kanda ya Ziwa Mashariki na Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili mkakati huu na “Vijana wa Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya kupewa pesa zote za kufanyia kampeni.
Vile vile, baadhi yao wamesema kuwa wanaambiwa kwamba iwapo watakubaliana na mpango huo wa ACT, moja kwa moja watakuwa wamepitishwa, maana chama hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa kutumia kura za maoni.
Taarifa zinasema sehemu ya malengo ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.
Zipo taarifa zisizothibitishwa kwamba mwezi uliopita Lowassa aliambatana na Zitto katika ziara ya kimya kimya ya Mkoa mmoja wa kanda ya Ziwa ambako anasemekana anataka kujenga ngome nzito ya ACT.
“Ninachojua ni kwamba iwapo ACT itafanikiwa kupunguza makali ya CHADEMA, Mzee atapita kirahisi, maana kikwazo kikubwa alichonacho hadi sasa hakipo ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa taarifa wetu aliye karibu na Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili hao walisafiri pamoja kwenda Kanda ya Ziwa.
Mkono mrefu wa CCM ndani ya ACT
Mbali na ufadhili wa Lowassa, imebainika pia kwamba makada wengi wa CCM wamewekeza raslimali zao katika kuinua ACT na kudidimiza CHADEMA.
Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa mbali na Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, mmoja wanaoratibu kazi ya Zitto ni kada wa CCM, ambaye ni mdogo wa mmoja wa mawaziri waliojiuzulu katika sakata la Operesheni Tokomeza, anayetokea kanda ya Kusini.
Wengine wanaotuhumiwa kujihusisha na mradi huu wa Tokomeza CHADEMA ni Naibu Waziri mmoja ambaye ni bingwa wa propaganda za CCM, na ambaye amewahi kutangaza hadharani kuwa ifikapo 2015 CHADEMA kitakuwa kimekufa. Wamo pia wabunge na viongozi kadhaa waandamizi wa CCM, ambao licha ya kwamba hawamuungi mkono Lowassa, wanafurahia msukosuko wowote utakaokipata CHADEMA kuelekea 2015.
Mwingine ambaye anadaiwa kufadhili ACT ni mtoto wa kigogo, ambaye katika miaka ya karibuni ameingia kwenye kashfa nyingi, kabla ya kukwaa ubunge hivi karibuni.
Madiwani waliohama waomba radhi warejeshwe
Wakati huo huo, madiwani wawili waliohamia CCM kutoka CHADEMA, katika kata za Ngokolo na Masekelo, Shinyanga, Sebastian Peter na Zacharia Machafuko, wameibuka na kusema wanajutia uamuzi wao, na sasa wanafanya jitihada za kuomba warejeshewe uanachama wa CHADEMA baada ya kukerwa na hila za CCM na ACT.
Madiwani hao wanadai kuwa walihamia CCM kwa muda  kwani waliambiwa kuwa ACT kitakapokuwa kimepata usajili wa kudumu wangejiunga nacho ili kuimarisha upinzani nchini.
Madiwani hao walijiunga na CCM Februari mwaka huu na kupokelewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye. Baadaye, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa alikituhumu CCM kwa mchezo mchafu.
“Tukishawishiwa kuhamia CCM kwa muda kwa lengo la kuhamia ACT ili kikipata usajili wa kudumu tuhamie huko pamoja na baadhi ya wanachama wa CCM.
“Tuliambiwa tufanye siasa za harakati, lakini tulichobaini ni kuwa tangu tukubali mawazo hayo ya viongozi wa ACT tukijua tunaimarisha upinzani imekuwa tofauti. Mkakati huo ulianza kuratibiwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Abbakari Gulam ambaye ni mtoto wa Meya wa Shinyanga, wakiwa na Habib Mchange, kisha tuliona mkakati unatekelezwa na mbunge wa Shinyanga mjini, Stephen Masele, Nape Nauye, Januari Makamba, Mwigulu Nchemba na Ridhiwani Kikwete,” walisema katika taarifa yao mbele ya waandishi wa habari jijini Mwanza.
Wakisimulia mkakati huo walisema walifikishwa Tinde na kiongozi huyo wa UVCCM kisha wakiwa huko walipigiwa simu na Stephen Masele na kuzungumza Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyewahakikishia kuwa baada ya kuondoka CHADEMA watajiunga na ACT ili iwawezeshe kupata nafasi za uongozi wa kitaifa katika chama hicho kipya, pamoja na kupatiwa kitita kikubwa cha fedha.
Chanzo chetu cha habari kutoka Shinyanga kimeelezwa kuwa baada ya kuhamia walipatiwa kiasi kikubwa cha pesa bandia, na katika kitita hicho waliambulia laki mbili ndio zilikuwa halali, pesa hizo zimetajwa kuwa zilikuwa ziwe milioni kumi na mbili lakini bada ya kuhesabu zilipatikana halali laki mbili tu, na zinadaiwa kutolewana na msaidizi wa Masele akiwa na Mchange katika hoteli ya Karena iliyopo Shinyanga, kabla ya madiwani hao kuondolewa na gari hadi Mwanza na kusafiri kwa ndege hadi Dar es Salaam kwa maelekezo ya Nape.
Tamko hilo linaongeza kuwa “kwa kipindi chote cha kudanganywa tulidhani Zitto anaonewa, hivyo tukaamua kujiunga na Chama chake ambacho alituhakikishia lakini tumebani kuwa ACT na CCM hawana tofauti, mikakati inatengenezwa na ACT ila watekelezaji ni CCM, baada ya kubaini ghiliba hizi tumeshindwa tumetafakari kuwa hata barua zetu tuliandika zikiwa na makosa ya kikanuni hivyo sasa tumemwandikia tena Meya kumuuliza ni kwanini hajatualika kwenye vikao viwili kwa kuwa tulikuwa hatujajiuzulu kisheria.
“Ili mtu kujiuzulu udiwani, kanuni zinasema kuwa diwani anaandika barua kwa Meya, unaambatanisha na kitambulisho cha udiwani, na hati ya ushindi ya udiwani ambayo hatujawapa wala vitambulisho vyetu, tulichokifanya ni kama kuandikiana barua za kawaida tu, na mtu kutangaza kujiunga na Chama kiingine bila kuchukua kadi yao sisi sio wanachama wao na kwa kuwa Chama chetu hakijachukua hatua zozote dhidi yetu basi tunarejea kwetu upinzani kushindana na CCM,” alisema Sebastian mbele ya waandishi wa habari.
Walisema CCM na ACT waendelee na kamari zao kuhadaa watanzania, “jamaa hao wana umakini kidogo ndio maana hawakubaliani kuwa bado hatujajiuzulu kisheria wakakimbilia kutupeleka jukwaani kushangilia, sasa sisi tunarudi kutumikia wananchi wetu kwani hatujavunja sheria, hatukukiuka kanuni za kujiuzulu furaha ya CCM na ACT ni ya muda tu, tulionda huko tumewabaini.
Kufuatia hali hiyo,madiwani hao waliandika kuwa “tunapenda kuomba radhi viongozi wote wa CHADEMA, wanachama na watanzania wote watusamehe, watupokee tukapambane kufanya kazi ya siasa za upinzani wa kweli kuleta ukombozi wa kweli kwa nchi yetu, tulichokiona huku tumekijua, tunawatahahadharisha wengine wakionga inafaa wajiunge huko kwa hasara yao ya maisha yao kisiasa na kufanya kazi ya kujenga CCM.”
Mkakati huu unaratibiwa na mmoja wa wabunge wa upinzani mwenye mahusiano ya karibu na viongozi wa CCM na serikali anayedaiwa hadi sasa kuifadhili ACT mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kujiimarisha mikoani kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Kazi ya wanazi wa ACT waliofukuzwa CHADEMA
Kwa sehemu kubwa, imebainika pia kwamba nguzo kuu za ACT ni makada wa zamani wa CHADEMA ambao kwa sababu kadhaa walipata misukosuko ndani ya chama hicho na kuchukuliwa hatua kali au kufukuzwa katika maeneo kadhaa ya nchi.
“Sisi hapa Mwanza tunatambua fika kwamba. Meya Henry Matata, Diwani Adam Chagulani wa Igoma, na Mushumbusi ndio vinara wa ACT wanaotumika kujaribu kusambaza ACT kanda ya Ziwa, na kujaribu kupenya na kubomoa ngome ya CHADEMA. Kwa sasa hata Habib Mchange wa Pwani, yupo  Mwanza anaratibu mipango ya uzinduzi wa chama chao utakaofanyika mapema mwezi ujao.
“Lakini hapa kuna ukweli ambao haupingiki, kwamba watu hawa walishafukuzwa CHADEMA, na sasa wanafanya siasa za chuki na visasi, wakiajribu kurubuni wanaCHADEMA. Pili, ni ukweli kwamba CHADEMA ni imara kuliko wanavyodhani. Haiwezi kubomolewa na wanachama wake wa zamani waliaoamua kuwekeza katika Siasa za usaliti. Hata huko waendako watasalitiana tu,” alisema kada mmoja wa CHADEMA mkazi wa Mwanza, ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji.
Alipotafutwa John Nchimbi kwa simu alisema jina lake litakuwa linachanganywa kwani yeye hajishughulishi na siasa bali ni mdau wa michezo ambaye historia yake iko Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), huku Dk. Kitila naye akikana kushiriki mpango wowote wa kuhujumu CHADEMA.
Alisema kuwa yeye ni mwanataaluma ambaye hajihusishi na siasa za vyama na kwamba kama wako viongozi wa CHADEMA wanarubuniwa na kukubali badi chama kinapaswa kujiuliza walipataje uongozi.
Fred Lowassa, Mwigulu Nchemba, Nape Nnauye, Mshumbusi simu zao ziliita bila kupokelewa.

Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.