Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, imemuachia huru
aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala, John Lubuva na
wenzake wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la
kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.7.
Mbali na Lubuva washtakiwa wengine ni Mhandisi Mkuu wa Idara ya Maji,
Idd Kisisa, Mkuu wa Idara ya Sheria na Ulinzi, Anderson Msumba na
Mwanasheria Andrew Kanonyele.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi, Juma Hassan alisema kuwa upande wa
mashtaka ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
umeshindwa kutoa vielelezo vinavyoonyesha ni kwa jinsi gani ubomoaji wa
nyumba zilizopo Tabata Dampo ulikuwa ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa Lubuva na wenzake walikuwa na kibali kinachoruhusu
bomoabomoa ya eneo hilo kwani walitekeleza agizo la Mahakama ya Ardhi
iliyotaka wakazi hao wahame katika eneo hilo kwani walikuwa wanaishi
kinyume na sheria.
“Pamoja na upande wa mashtaka kuleta malalamiko ya watu walionewa lakini
hakuna mlalamikaji hata mmoja aliyekuja kuthibitisha kuhusu madai ya
uvunjwaji wa nyumba zao kama wameonewa,” alisema Hakimu Juma.
Alisema kuwa pamoja na kwamba wakazi 88 wa eneo hilo walilipwa fidia ya
Sh milioni 20 kila mmoja licha ya kuwa kila nyumba ilikuwa na thamani
yake, fedha hizo zililipwa kimakosa kwani hawakuwa na hati inayoonesha
umiliki halali wa eneo hilo.
Mkurugenzi Lubuva na wenzake walikuwa wanakabilikwa na shtaka la
kubomoabomoa nyumba za wakazi wa eneo la Tabata Dampo kinyume na sheria
pamoja na kutumia vibaya madaraka yao, kula njama na kuisababishia
hasara Serikali.
Washtakiwa kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Julai, 2011,
wakidaiwa kuwa Februari 28, 2008, walikula njama na kutenda kosa la
kuvunja nyumba za makazi ya watu katika kiwanja namba 52 kilichopo
Barabara ya Mandela, eneo la Tabata, Dar es Salaam.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne , Julai 1 Mwaka 2014.
Post a Comment