TAARIFA
KWA VYOMB O VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu Julai 14, 2014 amekutana na
kundi la wasanii kutoka Marekani lililowasili nchini usiku wa Alhamisi, Julai
10, 2014, kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa wasanii wa Tanzania kwenye Ukumbi
wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mjini Dar es Salaam.
Wasanii hao ni pamoja na
Terrence J. (Jenkins), mwendeshaji wa kipindi cha muziki kwenye
televisheni ya E! Entertainment, mwigizaji wa filamu na mtunzi wa vitabu na
Revi Shelton, Mtendaji wa Shughuli za Muziki katika Kampuni ya Outlet Media
Group.
Wengine ni Chaka Zulu, Mtendaji
wa Shughuli za Muziki kutoka Kampuni ya
Disturbing The Peace Records na Davis Banner, mwigizaji,
mwanamuziki, mtunzi na msimamizi wa shughuli za muziki ambaye amepata kushinda
tuzo maarufu ya Grammy.
Kiasi cha wasanii 250
walishiriki semina hiyo inayoitwa Mafunzo ya Uendelezaji Usanii. Hiyo ilikuwa
ni kutimiza ahadi aliyotoa Rais Kikwete kwa wasanii wa Tanzania kuwa atachangia
kuinua kiwango cha ujuzi na weledi wao kwa kuwaandalia mafunzo yatayoendeshwa
na magwiji wa sanaa kutoka Marekani sasa imetimia.
Akizindua Kampeni ya Uzalendo
kwa Vijana inayoendeshwa na Muungano wa Wasanii Tanzania kwenye Uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma mwezi uliopita, Juni 14, 2014, Rais Kikwete aliahidi
kuchangia kuinua kiwango cha usanii na weledi wa wasanii wa Tanzania kwa
kusaidia kuandaa mafunzo yatakayoendeshwa na wasanii maarufu kutoka Marekani.
Mbali na kuendesha shughuli za
mafunzo ya wasanii ambazo wamekuwa wakizifanya kwa makundi madogo madogo tokea
walipowasili nchini, pia wanamuziki hao wa Marekani na kundi la wapiga picha
watatembelea sehemu mbali mbali nchini, hasa kwenye vivutio vya watalii,
ambako watapiga picha na kuandaa vipindi vya kuitangaza Tanzania katika vyombo
vya habari vya Marekani.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES
SALAAM.
15 Julai,2014
Post a Comment