Ndoto ya Watanzania kupata katiba mpya inazidi kufifia kadri siku zinavyokwenda. Wachambuzi wengi wanatabiri kuwa itakuwa ni vigumu sana kwa Tanzania kupata katiba mpya kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015. 

Tulidhani tungeweza kupata katiba mpaya, lakini hali ilivyo sasa hilo linaonekana ni sawa na ngamia kupita katika tundu ya sindano. Labda hatukufikiria kwa makini, tulijidanganya na tulidhani kuwa zoezi hili ni rahisi sana. Ukweli ni kuwa zoezi hili ni gumu na tumekwishaonyesha kila dalili za kushindwa mtihani huu. 
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba

Mchakato wa kuandika katiba mpya unakabiliwa na changamoto nyingi, baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha mchakato huu ni ukweli kuwa kuandika katiba mpya haijawahi kuwa ni agenda ya chama kilichopo madarakani. Suala hili hawalikubali na hawaliungi mkono kwa dhati na hakuna dhamira ya kweli katika kuwapatia Watanzania katiba mpya. Suala la kuandika katiba mpya halipo katika maandiko yoyote ya chama tawala ikiwa pamoja na ilani ya uchaguzi. 

Hakuna mahali popote ambapo kiongozi wa ngazi yoyote amewahi kulisemea kuwa wangependa kuandika katiba mpya.

Harakati za kudai katiba mpya hazikuanza leo, zilianza toka miaka ya 1980. Na juhudi za kupinga kuandika katiba mpya, nazo hazikuanza leo. Viongozi wa chama Tawala walipinga kwa nguvu zao zote. Katika miaka hiyo, walisikika wakihoji: “Ni kipengele kipi katika katiba kina mapungufu?” Aidha walidiriki kuwaambia wanasiasa kutoka vyama vya ushindani kuwa, hawana ridhaa ya wananchi, hawajachaguliwa, hivyo hawawezi kuwasemea wananchi.

 Ila wao ndio waliochaguliwa na wana ridhaa ya wananchi. Hoja hizi zilionekana kuwa na mashiko hasa ukizingatia kuwa vyama vya ushindani vilikuwa havina wabunge wala madiwani.

Tume ya Nyalali pamoja na mambo mengine ilipendekeza iundwe Tume ya Katiba (Constitutional Commission) ili iweze kuandika katiba mpya itakayokidhi mazingira mapya ya kisiasa. Tume pia ilipendekeza kufutwa kwa sheria kandamizi 40. Ilipendekeza kutolewa kwa elimu ya mfumo wa vyama vingi; pia ilipendekeza mali zote ambazo chama tawala kilizipata kwa nguvu za wananchi wote zirejeshwe Serikali. 

Mapendekezo haya na mengine, pamoja na pendekezo muhimu la kuandika katiba mpya yalikataliwa na serikali. Pendekezo moja tu ambalo lilikubaliwa nalo ni kuingia katika mfumo wa vyama vingi.

Mwaka 1992, Tanzania tuliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Bunge la Chama kimoja lilifanya mabadiliko kwa kuweka kiraka na kuruhusu mfumo wa vyama vingi. Madai ya katiba mpya yaliendelea na chama kilichoko madarakani kilijibu madai haya kwa kuunda Tume iliyojulikana kama Tume ya Jaji Kisanga mwaka 1998. Tume ya Jaji Kisanga ilipendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu; kupunguza madaraka ya Rais; matokeo ya Urais yaweze kupingwa mahakamani, wagombea binafsi waruhusiwe. Kwa mara nyingine tena, mapendekezo haya yalikataliwa.

Wakati wa uchaguzi wa 2010, chama kikuu cha upinzani, Chadema, kiliwaahidi wananchi kuwa kitaanzisha mchakato wa kupata katiba mpya ndani ya siku 100, na si kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanasiasa kuwa eti waliahidi kupatikana kwa katiba mpya ndani ya siku 100.

 Ilani ya Chadema ilisema kuanzisha mchakato ndani ya siku 100, jambo ambalo linawezekana kabisa, kwani unaweza kuanzisha mchakato hata ndani ya siku kumi tu. Suala hapa ni kuanzisha mchakato na si kupatikana katiba.

Vuguvugu la kudai katiba mpya lilizidi kuongezeka na hasa kutoka kwa Chama kikuu cha upinzani, asasi za kiraia, baadhi ya vyombo makini vya habari,  taasisi za elimu ya juu, wasomi na mashirika yasiyo ya kiserikali. 

Chama kikuu cha upinzani kiliyakataa matokeo ya Urais na kueleza masikitiko yao kuwa kwa mujibu wa katiba iliyopo hakiwezi kuyapinga matokeo ya Urais katika chombo chochote kile. Pia walitoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais alipokuwa akilizindua Bunge jipya na wakaweka wazi msimamo wao kuwa agenda yao ni kuandika katiba mpya.

Mwanasheria mkuu wa serikali alijitokeza hadharani na kupinga kwa kusema kuwa hatutaandika katiba mpya bali itafanyiwa marekebishao katiba iliyopo. Siku zote chama tawala kimekuwa kikiamini kuwa hakuna haja ya kuandika katiba mpya bali kuendelea kuifanyia marekebisho katiba iliyopo.

 Ndio maana hadi sasa kuna mabadiliko 14 yamekwishafanyika. Waziri wa Sheria na Katiba naye akasema kuwa hakuna fedha za kuendesha zoezio hili. Haya yote yanadhihirisha kukosekana utashi wa kisiasa wa kuandika katiba mpya. Licha ya majibu haya, wadau mbalimbali wakaendelea kushinikiza, wasomi wakaanda makongamo na mijadala kujadili kwa nini tunataka katiba mpya? Je katiba iliyopo ina mapungufu gani? Pia wakaanza kujadali mchakato utakaofaa katika kuandika katiba mpya.

Baadae, tukashuhudia serikali ikisalimu amri na kukubali madai ya wadau mbalimbali juu ya umhimu wa kuandika katiba mpya. Hii ilikuwa ni mabadiliko makubwa ya msimamo wa serikali (Big U-turn).

 December 31, 2010, Rais, alilihutubia Taifa katika hotuba yake ya mwaka na akawaambia Watanzania kuwa Serikali imedhamiria kuwapa fursa Watanzania kuandika katiba mpya. Aliahidi kuwa katiba mpya itakuwa tayari kufikia tarehe 26 April 2014, tukio ambalo litaambatana na sherehe za kutimiza miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Watanzania waliahidiwa kuwa na katiba mpya kabla ya uchaguzi wa 2015.

Ni muhimu tujiulize je, Kwa nini serikali ilibadili msimamo wake ghafla namna hii? Baadhi ya sababu zilizosababisha u-turn hii kwa maoni yangu ni kama zifuatazo: Kwanza, haikuwezekana kabisa, kuendelea kukipuuza chama kikuu cha upinzani, kwani kimekuwa kikipata mafanikio kwa kuongeza idadi ya Wabunge na Madiwani; Pia, Kimekuwa kikiongeza kukubalika kwake na kupata wafuasi wengi wengi zaidi; Mfumo wa vyama vingi umekuwa ukizidi kueleweka miongoni mwa Watanzania wengi na hasa vijana; 

Nchi majirani nazo zilikamilisha zoezi la kuandika katiba mpya na kuachana na katiba zilizoachwa na wakoloni. Nchi hizo ni kama vile Uganda, Kenya, Rwanda, Ghana.  Hivyo basi, Tanzania haikuweza kuwa kama kisiwa wakati jirani zake wamekamilisha zoezi hilo. Tulikuwa tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa majirani zetu na hasa Kenya; Sababu nyingine, ni ukweli kuwa Chama Tawala kilipoteza viti kadhaa katika uchaguzi uliopita na pia umaarufu wake na kukubalika kwake kunaendelea kushuka siku hadi siku kutokana na kuandamwa na kashfa mbalimbali, matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi, rushwa na minyukano ndani ya chama. 

Aidha mitandao ya kijamii nayo imechangia kwa kuongeza wigo wa majadiliano na kubadilishana taarifa juu ya masuala mbalimbali; Zanzibar ilikuwa imefanya mabadiliko ya Katiba kuruhusu serikali ya umoja wa kitaifa na pia kuitambua Zanzibar kama nchi, ina bendera yake, vikosi vya majeshi yake, Rais wa Zanzibar alipewa mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika sehemu ndogondogo kama mikoa, Wilaya;  Pia imekuwa ikiaminika kuwa Rais aliyoko madarakani alidhamiria kuwaachia zawadi Watanzania ya katiba mpya ambayo itawafanya wakumbuke utawala wake (Legacy). 


Kwa hali ya mchakato ilivyo sasa, hili bado tunasubiri kuliona iwapo kweli litatimia. Hizi ni baadhi tu ya sababu zilizosababisha chama tawala na serikali kusalimu amri na kukubali shinikizo la kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya. Ifahamike kwamba, mchakato huu ulianza si kwa mapenzi au hiari ya chama tawala bali kwa shinikizo.

Kutokana na kukosekana kwa dhamira ya kweli ya kuwapatia Watanzania katiba mpya, ndio maana, serikali mwaka 2011, ilitaka kuwasilisha Bungeni muswada wa Mabadiliko ya Katiba ambao ulikuwa na mapungufu mengi. Moja ya mapungufu hayo: ulitayarishwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo Watanzania wengi hawaijui; muswada huu ulitaka kuwasilishwa chini ya hati ya dharura (under certificate of emergency); Zanzibar ilisahaulika kabisa; ulimpa madaraka makubwa Rais na ulizuia baadhi ya masuala yasijadiliwe (limit constitutional debate to certain issues).
 Muswda huu ulipingwa kila kona na huko Zanzibar ulichwanwa hadharani.

 April 2011, Serikali iliamua kuondoa muswada huu kwa ajili ya kuandikwa upya. Muswada uliondolewa na kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili, lakini wadau wengi walistaajabu muswada huu kwenda kusomwa kwa mara ya pili badala ya kusomwa kwa mara ya kwanza ili kutoa nafasi kwa watanzania kujadili kwani sasa wanaelewa maudhui. Suala hili lilipitishwa kibabe bila maridhiano. 


Novemba 2011, Bunge lilipitisha muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba licha ya chama kikuu cha upinzani kupinga na kutoka nje ya Bunge. Tarehe 27 November 2011, Rais alianza kukutana na vyama vya siasa na wadau mbalimbali ili kusikiliza malalamiko yao na mnamo February 2012, Bunge lilifanya marekebisho katika sheria ya mabadiliko ya Katiba. Ukiangalia kwa makini, utaona mchakato huu unasonga mbele kwa shinikizo na si utashi wa kisiasa, na sababu kuu ni kuwa suala la kuandika katiba mpya, halijawahi kuwa agenda ya chama tawala.

Yapo mapungufu mengi katika sheria hii ya mabadiliko ya katiba, lakini yalio wazi kabisa na ambayo yalipigiwa kelele na wadau wengi ni kosa la kugeuza Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kuwa ni Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Hili lilikuwa ni kosa kubwa na sasa tunalipa gharama za makosa hayo, hasa tukikumbuka lugha za matusi, kejeli, dhihaka na kibaguzi zinatumika katika Bunge maalumu la katiba. Ndio maana, Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka chama tawala wanapinga rasimu ya pili na hasa katika maeneo yote yanayogusa maslahi yao. 

Mathalani, wanapinga kuwapo ukomo wa vipindi vya ubunge, yaani vipindi vitatu (Limited tenure for MPs), wanapinga pendekezo la wabunge kutokuwa mawaziri, wanapinga pendekezo la Spika asiwe miongoni mwa Wabunge, wanapinga mamlaka waliyopewa wananchi ya kumkataa Mbunge ambaye amedhihirika ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya ubunge (power of recall). Wabunge ambao wamekuwa wakitumia rushwa, hila, vitisho, ujinga na umaskini wa wapiga kura kuhakikisha kuwa wanabaki kuwa Wabunge daima, wataweza vipi kuafiki pendekezo la kuwa na ukomo wa vipindi vitatu tu? Ni wazi kuwa hili watalipinga kwani linagusa maslahi yao. 

Ni ujinga kutarajia wajumbe wa aina hii wataunga mkono mapendekezo ambayo yanagusa maslahi yao na kuwaondolea ulaji.
Tatizo hapa ni sheria ya mabadiliko ya katiba, tatizo hapa ni muundo wa Bunge maalum la katiba. Ndio tatizo. Tunayoshuhudia sasa ni matokea ya ubovu wa sheria hiyo iliyozaa muundo mbaya wa bunge maalaum la katiba. 

Wajumbe wameacha kujadili Rasimu iliwasilishwa na wamejikita katika ubabe wa kutukanana na kupigana vijembe. Kwa kuwa hakuna dhamira ya kweli, hawajali hata pale Wajumbe kutoka vyama vya upinzani walipoamua kutoka nje, hawajali hata kama  Bunge litavunjika. Kwani kwa mujibu wa sheria, tukishindwa kupata katiba mpya, tutarudi katika katiba ya zamani, na hili hasa ndio wanalolitaka na wamekwishaanza kulisema mara kadhaa. Hatuna budi kujiuliza, ni athari zipi tutazipata iwapo tutarudi katika katiba ya zamani? Je hatuna jambo lolote la kujifunza kutoka kwa majirani zetu wa Kenya?

Tujiulize, tunaweza vipi kupata katiba mpya kwa aina ya wajumbe wa Bunge maalum la katiba ambao wana tofauti za kiitikadi na kivyama? Ambao wanaligeuza suala la muundo wa muungano kuwa ni suala la imani? Kama dini! Eti kuna waumini wa serikali mbili! Tunaweza vipi kupata katiba mpya wakati tuna tofauti na misimamo mikali juu ya muundo wa Muungano? Hapa muafaka utapatikana vipi? Ingekuwa busara sana suala la muungano kushughulikiwa lenyewe peke yake na kwa uwazi na uhuru kabla ya kuanza zoezi la kuandika katiba. 

Lakini, kwa bahati mbaya watawala wetu waliona wanaweza kulipiga danadana na kupuuza kero na malalamiko ya muungano kwa miaka 50!! Wanahitaji miaka mingine mingapi kumaliza kero za muungano kwa muundo huu wa serikali mbili?
Bunge maalum la katiba lilitakiwa liwe ni chombo huru na lichaguliwe moja kwa moja na wananchi wenyewe kwa ajili ya kazi hiyo badala ya kuligeuza baraza la wawakilishi na bunge la sasa ambalo limehodhiwa na chama tawala. Kosa hili ndio limeufanya mchakato huu kufikia hapa ulipo.

 Hata idadi ya wajumbe ni wengi mno na hivyo kushindwa kuwa na mijadala ya afya.
Ushahidi mwingine unaodhihirisha mapungufu ya sheria hii ni mvutano na tafsiri tofauti juu ya mamlaka ya Bunge maalum la katiba ambapo wanasheria wamebaki wakibishana iwapo Bunge Maalumu lina mamlaka ya kufanya mabadiliko makubwa.

 Mabishano haya ni ushahidi tosha kuwa sheria hii si nzuri sana kiasi cha kutoa tafsiri tofauti.Tume ya Mabadiliko ya Katiba Iliundwa na kuanza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi. June 3 2013, Tume ilitoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Rasimu hii ilijadiliwa na Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Taasisi zenye malego sawa. Hapa pia tuliona kukosekana kwa dhamira ya dhati katika kuwapatia wananchi katiba mpya na wanayoitaka. Uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya katiba uligubikwa na rushwa na wajumbe wengi walilishwa maoni ya chama tawala. Kitendo hicho nacho kinanipa wasiwasi kama kweli kuna nia thabiti ya kuwapa Watanzania katiba wanayoitaka.
 
Pigo lingine katika mchakato huu, ni pale Bunge kwa mabavu lilipoamua kubadili sheria na kufupisha ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuamua kuwa ukomo wa Tume uishe mara tu baada ya kuwasilisha rasimu ya pili katika Bunge maalumu katiba. Hali hii imefanya kuwe na ombwe kwani Tume ingefanya kazi nzuri ya kutoa ufafanuzi na hata ushauri ambao ungesaidia mchakato kusonga mbele. Lakini, kutokana na kukosekana dhamira ya kweli serikali ya chama tawala ilifupisha ukomo wa Tume hii licha ya suala hili kupingwa kila kona. Ilikuwa ni vyema kwa Tume hii kuendelea kuwapo na kuwa na nguvu ya kisheria.


Dhamira ya kweli pia haikuonekana katika uundwaji wa Bunge maalum la katiba ambapo tulishuhudia wajumbe wengi wanaonekana kutoka chama tawala ikiwa ni pamoja na mwakilishi wa waganga wa kienyeji. Baada ya hapo tukashuhudia sarakasi ndani ya Bunge maalum. Bila aibu wala soni, utaratibu ukabidilishwa, Rais akapangiwa kuongea baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sote tukashuhudia, hotuba yake ikijikita katika kujibu hotuba ya Mwenyekiti wa Tume, si hivyo tu, akatumia nafasi hiyo kueleza msimamo wa chama chake, kupinga serikali tatu na kutoa vitisho kuwa eti jeshi litapindua serikali kwa kuwa serikali ya muungano haitakuwa na mapato ya kutosha kwalipa wanajeshi!!
Kwa kiasi kikubwa mchakato wa kuandika katiba mpya ulianza kuvurugika kuanzia hapo.

 Baadae yakafuata maneno ya kejeli, matusi, dhihaka na vitisho kutoka kwa wajumbe wa Bunge maalum wa kutoka chama tawala. Wengine wakadiriki kufanya kampeni na vitisho katika nyumba za ibada, eti Jeshi linaweza kupindua nchi endapo mfumo wa serikali tatu utapitishwa!! na wengine wakauwambia umma wa Watanzania kuwa eti zikipita serikali tatu, wataingia msituni! Kiburi na jeuri iliyopilitiza kiasi. 

Na wapo wanaosema serikali mbili ni lazima! Kama hiyo haitoshi, wenyeviti na manaibu wa kamati mbalimbali za Bunge takribani wote, wakatoka chama tawala. Huu nao ni ushahidi tosha kuwa hakuna dhamira ya dhati ya kufikia maridhiano bali ni mbinu na hila za chama tawala kutaka kuhodhi mchakato huu ili kupitisha matakwa yake.

Kumekuwa pia na kauli mbalimbali zinazodhihirisha kuwa hakuna dhamira ya dhati ya kuandika katiba mpya. Wapo viongozi wamesikika wakisema, “hivi katiba mpya ndio inapiga kura”? Wengine wakisema, “kipaumbele cha Watanzania sio katiba bali ni maji, barabara, elimu bora na afya.”

 Na wapo waliosema kirahisi tu, bila kujali gharama kubwa tulizokwishaingia katika mchakato huu kuwa, “tukishindwa kupata katiba mpya, tutarudi katika katiba ya zamani” bila kujali athari za hilo na bila kujiuliza mafundisho yapi tunaweza kuyapata kutoka kwa majirani zetu wa Kenya.  

Ninapoangalia mchakato huu, historia yake, tulipotoka, tulipo na tunapokwenda, ni wazi kuwa suala la kupata katiba mpya ni ndoto. Wapo ambao walitabiri hili. Lakini walipuuzwa. Itawezekana tu kupata katiba mpya kwa kuelendelea kushinikiza serikali na chama tawala, isihodhi mchakato, tukikumbushe kuwa hatuandiki katiba ya chama tawala, hawana hati miliki ya Tanzania na mawazo yao wao si mawazo ya Watanzania wote. 

Tuna haki ya kutoa mawazo yetu na ni lazima yasikilizwe na kuheshimiwa.Tunaweza kupata katiba mpya kwa kuwa na ubia mtakatifu kati ya vyama vya ushindani, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu, vyombo vya habari, sekta binafsi na wananchi, kuendelea kushinikiza na kulitaka Bunge lijadili Rasimu ya Warioba na si vinginevyo. Tukubali kuwa jambo hili si rahisi na halipendwi na chama tawala ambccho malengo yake ni kulinda na kutetea hadhi yake (Status quo).

 Hatuna budi kujiuliza, chama ambacho kimekuwa madarakani kwa miongo mingi, kikishinda chaguzi mbalimbali, kikihodhi Bunge na Taasisi mbalimbali, kikinufaika na katiba iliyopo ambayo inakifanya kiwe chama dola, kina sababu gani za kuandika katiba mpya? Msukumo wa kuandika katiba mpya kwa chama tawala ni upi? Ili iweje? 



Na Selemani Rehani
0654 00 20 82

Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.